- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Naibu Waziri Ndungulile Achangisha Zaidi ya Milioni 17 Kujenga Nyumba za Watumishi Kituo cha Wazee Kiilima Mkoani Kagera
Naibu Waziri wa Afya , Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Dk. Faustine Ndungulile afanikisha kupatikana kwa zaidi ya shilingi milioni 17 kwenye harambee ya kuchangia ujenzi wa Nyumba ya Watumishi katika Kituo cha Wazee Kiilima Kata ya Nyakato Wilayani Bukoba Mkoani Kagera.
Katika Harambee hiyo iliyofanyika Februari 22, 2018 katika Kituo cha Wazee Kiilima Dk. Ndungulile akiwa Mgeni Rasmi alichangisha fedha taslimu milioni 7,000,000/= na kiasi cha shilingi milioni 11 zikiwa ahadi kutoka kwa wadau mbalimbali pamoja ahadi za vifaa kama magodoro, saruji, baiskeli za wazee na mabati.
Katika hotuba yake kwa wananchi na wadau mbalimbali waliohudhuria harambee hiyo Naibu Waziri Dk. Ndungulile aliwasisitiza wananchi kuwa na moyo wa kujitolea kuchangia kituo hicho ili watumishi wanaowatunza wazee wapate mazingira mazuri ya kuishi baada ya kufanya kazi yao ya kuwahudumia wazee hao.
“Serikali itaendelea kuwaunga mkono wananchi kwa kuleta fedha katika kituo hiki ili kikamilike ujenzi wake na Wazee wetu waweze kuhudumiwa na watumishi ambao watawaza ni wapi pa kuishi au kukaa salama mara baada ya kufanya kazi yao ya kuwahudumia Wazee wetu,” Alisisitiza Dk. Ndungulile.
Kituo cha Kutunza Wazee Kiilima ni kituo cha Serikali kilichopo chini ya Wizara ya Afya , Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto. Kituo Hicho kilijengwa upya na Serikali baada ya kuathiriwa na Tetemeko la Ardhi lililotokea Septemba 10, 2016 Mkoani Kagera.
Majengo yaliyojengwa upya na Serikali ni pamoja na Mabweni mawili ya Wanaume na Wanawake, Jiko, stoo ya kutunzia chakula, Sehemu ya kulia chakula, sehemu ya kupumzikia wazee, vyoo viwili vya wanawake na wanaume. Changamoto iliyokuwa imebaki ni nyumba za watumishi ambazo kwa sasa zina hali mbaya ya uchakavu na hazistahili tena kuishi watu.
Fedha zilizopatikana zinatarajiwa kujenga nyumba mbili za watumishi (Two in One) ili kutatua changamoto ya watumishi wanaoishi na kufanya kazi ya kuwahudumia wazee ili wapate mahali salama pa kuishi na kutimiza wajibu wao kikamilifu bila kuwa na changamoto za sehemu za kuishi.
Katika Hatua nyingine Naibu Waziri Dk. Ndungulile alimshukuru Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum M. Kijuu kwa juhudi zake za kuipatia Bohari ya Dawa (MSD) kiwanja cha kujenga Bohari ya dawa katika Manispaa ya Bukoba na Mkoani Kagera ili kurahisisha upatikanaji wa dawa zote hapa Kagera.
Pia Dk. Ndungulile alimuomba Mkuu wa Mkoa kuhamasisha wananchi kuitikia wito wa kuwapeleka watoto wa kike miaka 4 hadi 9 kwenda kwenye vituo vitakavyokuwa vimepangwa kupata chanjo ya kansa ya shingo na uzazi kwani imeonekana kuwa kuna ongezeko kubwa la Kansa ya Shingo na uzazi katika mkoa wa Kagera.
Akimshukuru Naibu Waziri kwa kuamua kufanya ziara ya kukagua shughuli za afya Mkoani Kagera Mkuu wa Mkoa Kijuu aliomba Wizara ya Afya kuangalia upya tatizo la ugonjwa wa Malaria katika Mkoa wa Kagera kwani pamoja na juhudi zote zinazofanyika laikini kiwango cha ugonjwa huo kinazidi kupanda ambapo Naibu Waziri Dk. Ndungulile alisema tayari Wizara imeliona hilo na linafanyiwa kazi.
Naibu Waziri Dk. Ndungulile akiwa Mkoani hapa katika ziara yake ya siku mbili alivitembelea pia vituo vya Afya Kabyaile Wilayani Missenyi, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera, Kituo cha Afya Kaigara na Kituo cha Afya Kimeya Wilayani Muleba ili kukagua huduma za Afya zinavyotolewa kwa wananchi na kuongea na watumishi katika maeneo hayo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa