- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako azindua rasmi Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi VETA Ndolage Wilayani Muleba pamoja na kutoridhishwa na matumizi ya shilingi milioni 281,575,270.6 zilizotumika kukamilisha vyumba vya madarasa vinne ambavyo vilikuwa vimefikia hatua ya renta na ujenzi wake ulianzishwa na wananchi wa Kijiji Bushagara.
Profesa Ndalichako akihutubia wananchi wa Kijiji cha Bushagara Kata Kamachumu chuoni Ndolage alisema pamoja na kuzindua chuo hicho lakini wananchi wa eneo hilo hawakustahili kupata majengo aliyoyazindua bali walistahili kupata kilicho bora zaidi ya pale na kumwagiza Bw. Peter Maziku Maduki, Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi VETA kuchukua hatua kwa watendaji wa VETA ambao wanatekeleza miradi chini ya kiwango huku matumizi ya fedha yakiwa hayaridhishi.
"VETA mliomba wenyewe fedha shilingi milioni 281,575,270.6 na changamoto nilizozisikia mnazitaja hapa siyo changamoto kwangu kwani fedha mliomba wenyewe na mlijua kuwa mahitaji hayo mliyoyataja kama changamoto kabla ya chuo kuanza lazima yakamilike na chuo ndipo kianze. Naagiza kwenye bajeti yenu ya VETA ya mwaka 2019/2020 kata posho zote na kufikia Mwezi Juni 2020 muwe mmekamilisha majengo yote yanaohitajika katika chuo hiki." Aliagiza Profesa Ndalichako.
Taarifa ya ujenzi wa chuo cha VETA Ndolage iliyosomwa na Bw. Buruhi Mitinje Mkuu wa Chuo cha VETA Kagera aliyehusika kusimamia ukamilishwaji wa majengo ya Chuo cha VETA Ndolage ilibainisha kuwa zilitumika shilingi 177,565,000 katika ujenzi wa majengo.
Samani na vifaa vya kufundishia viligharimu shilingi 70,122,750 kuunganisha umeme shilingi 12,201,162.24 na gharama za Ramani (QS) na ulinzi shilingi 380,00 jumla shilingi 260,268,912.24 aidha, shilingi 21,600,000 zilitengwa kwaajili ya kuendeshea mafunzo.
Profesa Ndalichako alisema kuwa haiwezekani vyumba vinne vilivyokuwa vimefika hatua ya renta vikamilishwe kwa shilingi milioni 16 kila kimoja, jengo la utawal ambalo ni dogo sana haliwezi kugharimu shilingi milioni 42 pia karakana isiyokuwa na milango na madirisha gharama yake haiwezi kuwa shilingi milioni 21 na kiasi cha shilingi milioni 36 kutumika kuvuta umeme na kuweka miundombinu ya umeme katika majengo hayo.
“Haiwezekani sisi tunajenga chumba cha darasa kimoja kwa gharama ya shilingi milioni 20 katika mradi wa lipa kulingana na matokeo ambapo chumba hicho kinawekewa hadi vigae madirisha ya kisasa ya aluminium lakini hapa mlikuta vyumba vinne vimefikia hatua ya renta alafu kila chumba kigharimu shilingi milioni 16 haiwezekani.” Alisistiza Profesa Ndalichako
Katika hatua nyingine Mbunge wa Muleba Kasikazini Charles Mwijage aliuomba uongozi wa VETA kuhakikisha wanaendesha mafunzo ya fani ambazo zitalenga vijana na wananchi wa eneo la Ndolage kujiajili ambapo fani hizo alizitaja ikiwemo namna ya kusindika ndizi, upambaji, usindikaji wa nyanya pamoja na maparachichi.
Chuo cha VETA Ndolage kitafunguliwa na kuanza kutoa mafunzo rasmi mwakani 2020 na kitakuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi wa mafunzo ya muda mrefu 80 na wanafunzi wa kozi fupi fupi 300 katika fani mbalimbali kwa mwaka.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa