- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Vijiji 321 Mkoani Kagera Kunufaika na Nishati ya Umeme Baada ya Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA III) Kuzinduliwa Rasmi na Utagharimu Bilioni 45.43
Wananachi Mkoani Kagera wapata neema ya nishati ya umeme baada ya Serikali kuzindua Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA III) utakaogharimu jumla ya shilingi bilioni 45.43 na kuvinufaisha vijiji 321 ambavyo havikupata nishati ya umeme kwenye awamu ya kwanza na ya pili.
Akizindua Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA III) Kijijini Rwabigaga Kata Kamuli Wilayani Kyerwa Naibu Waziri wa Wizara ya Nishati na Madini Dkt. Medard Kalemani alisema mradi huo wa Umeme vijijini Awamu ya Tatu umelenga kuvifikia vijiji na vitongoji vyote na kila mwananchi ambaye hakupata umeme kwa awamu zilizopita.
“Mradi utavilenga vijiji vyote ambavyo havikufikiwa kabisa katika awamu ya kwanza na ya pili. Pili, mradi utavifikia vitongoji vyote ambavyo viliachwa kwenye vijiji katika awamu ya kwanza na ya pili. Tatu, mradi huo umelenga kufukisha umeme kwenye maeneo ambayo hayafikiki kirahisi kama visiwani ambapo Kagera visiwa 176 vitafikishiwa umeme wa jua.” Alisistiza Dkt Kalemani
Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA III) Mkoani Kagera utatekelezwa kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza jumla ya vijiji 141 vitafikishiwa umeme na kazi hiyo inaanza kuanzia sasa mpaka mwezi Machi 2019. Awamu ya pili itafuata mara baada ya awamu ya kwanza kukamilika na vijiji 180 katika awamu ya pili vitafikishiwa umeme na awamu hiyo itakamilika mwaka 2021.
Naibu Waziri Dkt. Kalemani alisema kuwa katika awamu ya tatu kila mwananchi atafikishiwa umeme katika nyumba yake bila kubagua aina ya nyumba hata iwe ya tembe kwani lengo la Serikali ni kuhakikisha kila mwananchi ananufaika na umeme.
Baada ya uzinduzi huo Naibu Waziri Dkt. Kalemani alimkabidhi Mkandarasi ambaye ni NAKUROI CONSTRUCTIONS COMPANY LIMITED atakayetekeleza Mradi huo Mkoani Kagera na kumwagiza ahakikishe anawaajili Wakandarasi wadogo wadogo kutoka katika maeneo husika ili kupunguza gharama na kutoa ajira kwa wazawa wa maeneo husika.
Pili, aliwaagiza Shirika la TANESCO kuhakikisha wanafungua madawati katika Tarafa na kata kwa maeneo ambayo ofisi zao zipo mbali ili kuwaondolea wananchi usumbufu wa kulipia gharama za kuwekewa umeme. Aidha, aliagiza viongozi wote wa Serikali kushirikiana na Mkandarasi kuhakikisha Tasisi zote za Serikali zinafikiwa na umeme huo katika vijiji vitakavyotekelezewa mradi.
Kitaifa Mradi wa Umeme Vijijni Awamu ya Tatu (REA III) unatarajia kutekelezwa kwenye vijiji 7,873 na tayari umezinduliwa katika Mikoa ya Simiyu na Kagera pia utazinduliwa katika Mkoa wa Geita. Aidha, kwa upande wa mkoa Mkuu wa Mkoa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum M. Kijuu kwaniaba ya wananchi alimshukuru Naibu Waziri Dkt. Kalemani kwa kuzindua mradi huo na alihaidi kumsimamia kikamilifu Mkandarasi ili utekelezwe na kukamilika kwa wakati.
Baada ya uzinduzi huo uliofanyika Julai 11, 2017 Mkoani Kagera wananchi waliaswa kutumia fursa hiyo ya kupata umeme kwa kujiajili kwa kuanzisha viwanda vidogo vidogo na kujipatia ajira ili wajiingizie kipato.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa