- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Wawekezaji wazawa Mkoani Kagera wametakiwa kuchangamkia fursa ya uwekezaji katika Mapori ya akiba Biharamulo, Burigi, Kimisi, Ibanda na Rumanyika yaliyotangazwa hivi Karibuni kuwa hifadhi za Taifa ambapo mapori hayo yalikuwa chini ya Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA) na sasa tayari Mapori hayo yanasimamiwa na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA).
Rai hiyo ilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti akiwa katika Pori la Burigi eneo la Nkonje mara baada ya kupita katika pori hilo na kujionea wingi wa wanyama pori mbalimbali ambao wameongezeka kwa kasi na uoto wa asili kurejea katika hali yake baada ya kuondolewa wavamizi na mifugo katika Mapori hayo.
Katika hatua za awali Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limeanza mikakati mbalimbali ya uboreshaji wa Mapori hayo ili kuyapandisha hadhi na kuwa Hifadhi za Taifa Tanzania. Kwanza TANAPA imewaleta watumishi 16 Mkoani Kagera ili kurahisisha mchakato wa upandishwaji hadhi wa Mapori hayo na kuongeza doria kwa kishirikiana na watumishi waliokuwepo wa Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania TAWA.
Watumishi hao 16 wa TANAPA wanaongozwa na Bw. Damian Salu ambaye ni Mkuu wa Hifadhi na Mratibu wa mchakato wa upandishwaji hadhi wa Mapori ya Akiba matano Mkoani Kagera ambapo akiongea na Mkuu wa Mkoa Gaguti katika Pori la Burigi alisema kuwa pamoja na TANAPA kuwa na watumishi hao 16 lakini imeanza kuchukua mbalimbali hatua za kuboresha mapori hayo.
Bw. Salu alisema kuwa tayari TANAPA imeanza kutengeneza miundombinu ya barabara na tayari Kilometa 35 za barabara zimerekebishwa ili kuweka urahisi wa Watalii wa nje na ndani kupita katika Hifadhi hizo kwa urahisi wakati wa kutalii. Pili ni kuongeza doria katika mapori hayo ili kukomesha ujangiri katika Hifadhi za Taifa tarajiwa.
Mikakati mingine ni kuelimisha wananchi wanaozunguka Hifadhi tarajiwa juu ya umuhimu wa kutunza Hifadhi na jinsi ya wao watakavyonufaika na Hifadhi hizo katika masuala ya maendeleo ya jamii pamoja na ulinzi shirikishi kati yao na Shirika la Hidhi za Taifa Tanzania. Aidha, TANAPA wanaendelea na mikakati ya kuzitangaza Hifadhi mpya zilizoko Mkoani Kagera ili wawekezaji wa ndani nje kuja kuwekeza Kagera.
Bw. Salu pia alisema kuwa TANAPA wanao mpango wa kupandikiza aina mbalimbali nyingine za wanyama katika Hifadhi tarajiwa ili kuongeza vivutio ambavyo ni muhimu kwa Watalii wa ndani na nje kuja katika Hifadhi hizo kuona.
Fursa za Nchi Tatu Katika Pori la Ibanda
Katika Pori la Akiba la Ibanda Wilayani Kyerwa kuna eneo ambalo ni mipaka ya nchi tatu za Afrika Mashariki ambapo kwa upande wa Tanzania eneo hilo la pori la akiba linajulikana kama Kagaga, Nchi ya Uganda eneo hilo linaitwa Sophia au “Mirama Hill” na Upande wa Rwanda panaitwa Kajitumba. Eneo hili linatenganishwa na Mto Kagera na Mtalii anapata fursa ya kuona mipaka ya nchi tatu kwa wakati mmoja.
Mara baada ya kutembelea eneo hilo Mkuu wa Mkoa wa Kagera Gaguti alitoa wito kwa wawekezaji kuona fursa hiyo ikiwa ni pamoja na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kujenga Hoteli na vituo vya Utalii ili kutoa fursa kwa Watalii kutoka nchi za Rwanda na Uganda kuingia katika Hifadhi ya Taifa tarajiwa ya Ibanda kupitia mipaka hiyo kwa kuvuka mto Kagera na kuingia katika Hifadhi bila kupita Mipaka ya Mulongo na Rusumo.
“Hapa tukipata wawekezaji tunatakiwa kujenga Hoteli za kisasa, vituo vya utalii ili kama mtalii anataka kutoka Uganda au Rwanda kuja katika Hifadhi ya Taifa ya Ibanda apite hapa na hakuna ulazima wa kupita Mulongo au Rusumo, hii ni fursa kubwa sana lazima tuitangaze kwa nguvu zote ili tutumie nafasi ya uwepo wa mipaka hii mitatu kupata watalii ambapo tunaweza kujenga vivuko au kupata boti za kitalii za kuwavusa katika Mto huu wa Kagera. Alisistiza Mkuu wa Mkoa Gaguti.
Wito kwa wananchi wa Mkoa wa Kagera
Wito unatolewa kwa vijana Mkoani Kagera kuanza kuchangamkia fursa kwa kuanza kujiandaa katika masomo ya utalii ambapo watapata ajira za kuongoz Watalii, kujiandaa kusomea uhotelia ili kufanya kazi katika Hoteli za Kitalii zitakazojengwa katika Hifadhi hizo za Taifa Mkoani Kagera, hayo ni pamoja na kusomea lugha mbalimbali ili kupata fursa nzuri ya kuongoza Watalii kutoka nchi mbalimbali na kuelezea vizuri juu ya maliasili katika hifadhi hizo.
Wawekezaji mbalimbali hasa kwa Mkoa wa Kagera wanatakiwa kuchangamkia fursa hii ya utalii kwa kujenga Hoteli nzuri, hususani katika Halmashauri zetu za Wilaya zinazozunguka Hifadhi hizo tarajiwa za Taifa lakini pia Hoteli hizo kujengwa ndani ya Hifadhi hizo pamoja na vivutio na vituo mbalimbali vya kitalii ili kuvuti watalii wa ndani na nje ya mkoa kwa ujumla.
Utamaduni, wananchi wanaozunguka katika Hifadhi tarajiwa za Taifa wanakumbushwa kujiandaa kuanzia sasa hasa katika kutengeneza vitu malimbali vya kitamaduni ambavyo vinaweza kuuzwa kwa watalii hasa watakaokuwa wanatoka nchi za nje ili wananchi hawa wajipatie kipato tena kwa fedha za kigeni kupitia vivutio vya kitamaduni vitakavyokuwa vinapatikana katika hifadhi hizo.
Vyakula vya Kitamaduni, Wananchi pia wanatakiwa kuanza sasa kulima kwa wingi vyakula vya kitamaduni kulingana na utamaduni wao na kujiandaa kwa ajili ya kupata soko la vayakula hivyo vinavyopendelewa sana na Watalii na kuona ni namna gani vyakula hivyo vinapikwaje au vinaandaliwaje kitamaduni na ikumbukwe kuwa hiyo ni mmojawapo ya utalii.
Hoteli kubwa zitahitaji vyakula hivyo kwa wingi kwa maana hiyo wakulima Mkoani Kagera hasa ambako kila zao linakubalika vizuri kulimwa na kustawi wanatakiwa kuiona fursa hiyo mapema ili masoko ya mazao hayo yasije kutekwa na wakulina na wafanyabiashara kutoka mikoa jirani au pengine nchi jirani wakati fursa hiyo ingeweza kuchukuliwa na wananchi wa Mkoa wa Kagera.
Changamoto
Chanagamoto kubwa ambayo bado hasa inaikumba Hifadhi ya taifa Tarajiwa ya Ibanda Wilayani Kyerwa ni pamoja na nchi jirani zinazopakana na hifadhi hiyo kujenga Kambi ya Wakimbizi ambayo ipo karibu sana na hifadhi hiyo jambo ambalo linapelekea wakimbizi hao kuvuka mto Kagera na kufuata mahitaji muhimu upande wa pili kama kuni na kuua wanyama pori kwa ajili ya kupata kitoweo au chakula.
Pia nchi jirani zinazopakana na Hifadhi za taifa tarajiwa Mkoani Kagera zimeruhusu makazi ya wananchi kupakana na hifadhi hizo jambo ambalo linachochea ujangiri katika hifadhi pale wananchi wa nchi hizo wanapovuka na kutaka kuendesha shughuli za uwindaji kwenye hifadhi.
Mwisho bado wananchi hasa katika Mkoa wetu wa Kagera hawajachangamkia fursa ya kuwekeza katika Hifadhi hizo na kutoa nafasi kwa wawekezaji kutoka nje ambapo hapo baadae wananchi hawa wa kagera wanaweza kuanzisha migogoro kwa kutokuona manufaa ya hifadhi za taifa tarajiwa kwao. Ni muhimu sana wananchi wazawa kuanza kuchangamkia fursa hizi mara moja ili kujiongezea kipato. Karibu TANAPA Kagera, Karibu Tutalii Kagera.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa