- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti awataka watumishi wa Sekta ya Afya Mkoani Kagera kutoa huduma bora kwa wananchi kulingana na hadhi na ubora wa majengo yaliyojengwa ama kuboreshwa kwa fedha za Serikali kwa kiwango cha kuridhisha katika Vituo mbalimbali vya Afya ili kuhakikisha huduma muhimu zinapatikana katika vituo hivyo hasa huduma za upasuaji kwa mama wajawazito.
“Nimeridhika na ubora wa majengo yaliyojengwa katika kituo hiki pamoja na thamani ya fedha inaonekana katika majengo haya, rai yangu kwenu watumishi wa Kituo hiki cha Afya na vituo vyote vilivyoboreshwa Mkoani Kagera ni kutoa huduma zinazofanana na majengo yalivyo, huduma safi kwa wananchi zenye kuwafariji wanapokuja kupata huduma za afya hapa.” Alisisitiza Mhe. Gaguti
Mkuu wa Mkoa Gaguti alitoa rai hiyo Augusti 24, 2018 katika Kituo cha Afya Kimeya Wilayani Muleba alipofanya ziara ya kujitambulisha katika Wilaya hiyo na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo ambapo alitembelea na kukagua ujenzi wa majengo matano yaliyogharimu kiasi cha shilingi milioni 456 zilizotolewa na Serikali pamoja na wananchi kuchangia kiasi cha shilingi milioni 11.7
Majengo yaliyojengwa ni pamoja na jengo la Mama na Mtoto, Jengo la Maabara, Nyumba moja ya Mtumishi, Jengo la upasuaji, na Jengo la kuhifadhi maiti. Mhe. Gaguti aliwashukuru wananchi kuchangia miradi ya maendeleo na kuwataka kuendelea kuchangia miradi mbalimbali ili kujiletea maendeleo na kuitunza pia miradi hiyo.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa Gaguti alitembelea shamba la kahawa lenye ekari 45 la Mkulima Bw. Shakiru Yahya lililoko Kijijini Karutanga kata ya Magata Karutanga na kujionea kilimo cha Kahawa cha kisasa na chenye tija ambapo shamba hilo ni la mfano kwa wakulima wengine ambao wanajishughulisha na kilimo hasa zao la Kahawa.
Akitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa Mkulima wa shamba hilo Bw. Shakiru Yahya alisema kuwa alihamasishwa kulima kahawa na baba yake mzazi wakati akiwa mdogo baada ya baba yake kuwa analima Kahawa na kuuza na kupata fedha za kuendesha familia ikiwa ni pamoja na kuwapatia matumizi mbalimbali ya kifamilia na karo za shule.
Baada ya kujitegemea Bw. Shakiru mwaka 2000 alianza kulima kidogo kidogo na mpaka sasa amefikisha ekari 45 za shamba la mibuni aina ya Arabika na Robusta na amepata mafanikio makubwa kwani kwa msimu uliopita aliweza kuvuna tani 40 za kahawa na kupata fedha za kitanzania shilingi milioni 60, anasomesha watoto wake, ameajili zaidi wafanyakazi 50, amenunua magari ya kusafirisha mizigo, amenazisha kiwanda cha kusindika kahawa chenye gaharama ya milioni 650.
Mara baada ya kutembelea na kukagua shamba hilo . Gaguti aliwataka wananchi wa Wilaya ya Muleba hasa wanaozunguka shamba hilo kwenda kwa Bw. Shakiru kujifunza kilimo cha Kahawa badala ya kuendelea kumtazama tu. Aidha, Mhe. Gaguti alimshukuru mkulima huyo kwa kuwekeza katika Sekta ya Kilimo na sasa kuanzisha kiwanda ambapo alimhakikishia kuwa Serikali itaendelea kushirikiana naye ili kuhakikisha lengo alilokusudia linatimia.
Katika Ziara hiyo pia Mkuu wa Mkoa aliweza kuongea na Watumishi wa Serikali, Wazee na Wadau mbalimbali wa Maendeleo ya Wilaya ya Muleba ambapo aliwakumbusha watumishi wa umma kuhakikisha wanatatua kero za wananchi kila Mtumishi katika nafasi yake ili kupunguza migogoro mbalimbali katika jamii na kuwafanya wananchi waiamini Serikali yao.
Mwisho Mhe. Gaguti alitoa msisitizo wa kulipa kodi ya Serikali kwa wadau mbalimbali na wafanyabiasha ambapo alisema kuwa bado hajaridhishwa na kiwango cha ulipaji kodi katika Mkoa wa Kagera. Mhe. Gaguti alisema suala hilo ni kipaumbele chake katika Mkoa na anataka kuona Kagera inaongoza katikaulipaji wa kodi bila shuruti.
Mkuu wa Mkoa Gaguti anaendelea na ziara ya kujitambulisha katika Wilaya za Mkoa wa Kagera ili kuufahamu vizuri mkoa wake na maeneo yake ya utawala lakini paia anaendelea na ukaguzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika Halmashauri za Wilaya.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa