- Home
- About Us
- Administration
- Districts
- District Councils
- Investment Opportunities
- Services
- Publications
- Media Center
Afisa Biashara wa Mkoa
IsayaTenddega
SHUGHULI ZA SEKTA YA VIWANDA NA BIASHARA
|
Shughuli za Sekta hii zimegawanyika katika sehemu ya Viwanda, Biashara/Masoko, na uwekezaji kwa lengo la kuinua na kuongeza ufanisi kwa kuweka uhusiano mpana kati ya sekta ya umma na sekta binafsi katika uzalishaji nchini sambamba na kujenga uchumi endelevu, unaohimili ushindani katika masoko ya nje kama njia ya kuchochea kasi ya maendeleo ya kiuchumi nchini. Shughuli kuu zinazofanywa na sekta ya Biashara katika Sekretarieti ya Mkoa wa Kagera ni kama ifuatavyo:-
i. Kutoa ushauri wa kitaalam kwa wadau wa maendeleo ya kiuchumi kuhusu masuala ya biashara, masoko, viwanda na uwekezaji katika mkoa.
ii. Kutoa elimu na mafunzo ya ujasiriamali kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa, watu wananchi/watu binafsi, vikundi, makampuni pamoja na mashirika yanayohudumia jamii katika mkoa wa Kagera.
iii. Kuratibu utoaji wa leseni za biashara kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa (MSM) Mkoani Kagera.
iv. Kuratibu shughuli za usajili wa majina ya biashara na makampuni kwa mujibu wa sheria ya usajili wa shughuli za biashara (Business Activities Registration Act-BARA namba 14 ya mwaka 2007) na sheria ya usajili wa makampuni namba 12 ya mwaka 2002 pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2011- (Business Laws) Misclleneuos Amendments
v. Kujenga mazingira wezeshi na yenye kuvutia wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza katika Mkoa wa Kagera.
vi. Kuratibu upatikanaji wa vibali mbalimbali vya uuzaji bidhaa nje ya nchi na uingizaji bidhaa.
vii. Kutoa ufafanuzi wa miongozo , sera, sheria na kanuni kwa wadau wa maendeleo ya kiuchumi kuhusu biashara, masoko, viwanda na uwekezaji katika Mkoa.
viii. Kuwaunganisha wakulima na wazalishaji na masoko ya bidhaa zao.
ix. Kuhamasisha wakulima/wajasiriamali na wazalishaji kuzalisha kwa wingi na kwa kuzingatia ubora na tija hatimaye kuongeza thamani. (Value Addition).
x. Kuhamasisha Watanzania kupenda bidhaa za Tanzania ili kukuza uchumi wa Tanzania.
xi. Kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo katika mkoa na kuhamasisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza katika Mkoa wa Kagera
TARATIBU ZA BIASHARA YA NDANI
|
Ili kuratibu shughuli yoyote ndani ya nchi/mkoa mfanyabiashara/mjasiriamali atatakiwa kutimiza masharti yafuatayo.
• Awe na sehemu maalum ya kufanyia biashara.
• Awe na Namba ya utambulisho wa Mlipa Kodi (TIN-Tax Identification Number) ambayo hutolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania.
• Kwa biashara zenye udhibiti mfano, usafirishaji, vituo vya mafuta, shule n.k ni lazima awe na leseni ya Mamlaka husika kama vile SUMATRA, EWURA, n.k.
• Awe na leseni ya biashara husika inayotolewa na Halmashauri husika.
• Cheti cha usajili wa kampuni (Company Certificate of Registration) kama ni kampuni au cheti cha usajili wa jina la biashara (Business Name Registration Certificate) husika kutoka BRELA.
TARATIBU ZA BIASHARA YA NJE
|
Ili kufanya biashara nje ya nchi mfanyabiashara anashauriwa kukamilisha au kuandaa vitu vifuatavyo:-
• Leseni ya biashara ya kununua na kuuza nje (Import & Export License) ambayo hutolewa na Wizara ya Viwanda na Biashara kupitia Ofisi ya Biashara Mkoa.
• Vibali vya biashara husika, mfano vibali vy akusafirisha mazao nje ya nchii.
• Chati cha Uasili (Certificate of Origin) kama kwa nchi wanachama wa jumuiya ya Afrika Mashariki. Hii humsaidia Mfanyabiashara kuondokana na kodi ya kuingiza bidhaa (Import duty 25%) ndani ya nchi husika kutoka katika nchi wananchama, na badala yake atatakiwa kulipia kodi ya ya ongezeko la thamani pekee.
• Cheti cha uanachama wa Chemba ya Wafanyabiashara wenye viwanda na biashara (TCCIA Membership Certificate.
• Cheti cha usajili wa kampuni(Company Certificate of Registration) kama ni kampuni au cheti cha usajili wa jina la biashara (Business Name Registration Certificate) husika kutoka BRELA.
• Cheti cha ubora wa bidhaa kutoka TFDA-Mamlaka ya chakula na dawa au Shirika la Viwango Tanzania TBS.
TARATIBU ZA BIASHARA ZENYE UTHIBITI MAALUM
|
Biashara zenye udhibiti zinazozungumziwa hapa ni pamoja na biashara za vituo vya mafuta ya dizeli, petrol, mafuta ya taa, biashara ya usafirishaji abiria kwa magari/mabasi, usafiri wa majini kwa meli na boti, biashara za mitandao ya mawasiliano ya simu, radio, televisheni, usafiri wa anga, biashara za madawa ya binadamu na mifugo, n.k. Leseni za biashara hizi hutolewa mara tu baada ya mamlaka husika kuwa imejiridhisha na masuala ya kitaalam na kutoa kibali/leseni ya mamlaka hiyo ndiyo Ofisi ya biashara inaweza kutoa leseni ya biashara. Changamoto iliyopo ni kuwa mamlaka zilizo nyingi bado hazijaimarishwa na kuwa na Ofisi katika kila makao makuu ya mikoa, mfano EWURA, BRELA
BEI ZA BIDHAA
|
Katika kipindi cha nyuma serikali iliwahi kuunda chombo cha kudhibiti bei za bidhaa zote, chombo kilifahamika kama tume ya bei (Price commission). Hata hivyo, serikali ilipojitoa katika masuala ya kufanya biashara na tangu kuanzishwa kwa soko huria bei za bidhaa mbalimbali ambazo hazina mamlaka maalum za udhibiti zimekuwa zikiendeshwa/kuamuriwa na nguvu ya soko pamoja na ushindani wa soko.
UTOAJI WA LESENI ZA BIASHARA
|
Kuna makundi mawili ya leseni za biashara kwa mujibu wa sheria za leseni ya leseni za biashara namba 25 ya mwaka 1972 iliyofanyiwa maboresho mwaka 1982. Makundi hayo ni: i) kundi la leseni zinazotolewa na mamlaka za serikali za mitaa (Halmashauri za Wilaya na Manispaa) ii) kundi la pili ni leseni zinazotolewa na Wizara ya Viwanda na Bisahara mfano leseni za kufungua na kuendesha Klabu za Muziki za Usiku (Night Clubs) na leseni za kununua na kuuza nje ya nchi (Import and Export License).
Masharti ya kuomba leseni za biashara kwa makundi yote mawili ni kama ifuatavyo:-
• Cheti cha usajili wa Kampuni au jina la biashara (Certificate of registration/incorporation)
• Kama ni kampuni “memorandum and article of Association''.
• Cheti cha urai (Passport ya Tanzania) au cheti cha kuzaliwa au hati ya kiapo (affidavit).
• Mkataba wa jengo analofanyia biashara husika au hati ya umiliki endapo jengo ni lake.
• Hati ya kujiandikisha kama mlipa kodi (TIN)
• Endapo wana hisa wa kampuni wapo nje ya nchi maombi yaambatane na hati ya kiwakili.
HATUA ZA KUPATA LESENI YA BIASHARA
|
Pamoja na kukamilisha masharti hayo, ili kupata leseni siku za nyuma mwombaji alitakiwa kupitisha fomu ya maombi iliyojazwa katika Ofisi za mipango miji, ofisi za afya na hatimaye Ofisi za biashara tayari kwa kupata leseni husika baada ya kuwa wote wamekagua maeneo yao kitaalam na kujiridhisha. Hatua hiyo ilionekana kuwa na urasimu mwingi na kufanya ucheleweshaji wa kutoa leseni hatimaye biashara nyingi zilikuwa zikichelewa kuanzishwa. Ikiwa ni hatua za kurahisisha uanzishaji na uendeshaji wa biashara, sharti la kupitisha fomu ya maombi ya leseni katika ofisi za afya na mipango miji limeondolewa. Aidha, baada ya kukamilisha taratibu zote pamoja na nyaraka zote zinazohusika mwombaji itamchukua muda wa siku moja hadi tatu tu kuwa amepata leseni yake kutoka katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa alipoombea leseni yake.
ADA ZA LESENI
|
Kwa kipindi kirefu ada za leseni kwa mujibu wa sheria zilikuwa kati ya shilingi 10,000 hadi 2,000,000 kutokana na aina ya leseni, eneo la biashara na aina ya biashara inayoombewa leseni. Wakati fulani ada hizo ziliondolewa na kwa kipindi kirefu leseni zilikuwa zikitolewa bure ili kurahisisha watu wengi zaidi kuhamasika na kuanzisha biashara ili kuiongezea serikali mapato kwa kuwa na vyanzo vingi vya mapato.
Hata hivyo serikali katika bunge la bajeti la mwaka 2011/2012 imerudisha utaratibu wa ada za leseni za biashara na utaratibu huu utaanza kutumika rasmi Januari Mosi, 2012. Umetolewa muda wa kutosha kuzipa Halmashauri za Wilaya muda wa kujiandaa na kuweka miundombinu vizuri ili zoezi hili litakapoanza liende kwa kasi inayotarajiwa na kuleta matunda kwa serikali za mitaa ili kupunguza utegemezi kutoka serikali kuu.
Hivyo ni muhimu kwa kila mfanyabiashara kuhamasika na kusajili biashara yake ikiwa ni pamoja na kuikatia leseni ya biashara husika ili kufanya biashara kwa haki, uhuru na amani na kuchangia kikamilifu ujenzi na uimarishaji wa uchumi wa Mkoa wa Kagera na Taifa kwa ujumla.
USAJILI WA SHUGHULI ZA BIASHARA
|
Kwa mujibu wa Sheria ya Usajili wa Shughuli za Biashara Namba 14 ya mwaka 2007 (Business Activities Registration Act - BARA No 14 of 2007) ya biashara inatakiwa kusajiliwa na kupewa cheti cha kudumu ili kutambulika kuwa ni biashara rasmi. Usajili wa jina la biashara umekuwa ukifanywa na Wakala wa Usajili wa Makampuni na Majina ya Biashara Tanzania ambaye ni BRELA. Wakala huyu ndiye mtekelezaji Mkuu wa Sheria ya BARA na 14 ya mwaka 2007.
USAJILI WA MAKAMPUNI
|
Usajili wa makampuni hufanywa na BRELA chini ya sheria ya makampuni namba 12 ya mwaka 2002 (Company Act No 12 of 2002). Ili kusajili kampuni ya aina yeyote ile unashauriwa kufika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kitengo cha Biashara ili uweze kushauriwa namna bora ya kufanikisha usajili kwa wakati. Mahitaji muhimu ya usajili wa kampuni ni kama ifuatavyo:-
• Kuandaa/Kufikiria jina la kampuni;
• Kuandaa “Memorundam and Artcles of Association”;
• Kujaza fomu za usajili namba 14a na 14b;
• Kuandaa ada ya usajili wa kampuni inayotegemea mtaji wa kampuni;
• Kuwasilisha nyaraka husika kwa Msajili na Kupata cheti cha usajili wa kampuni.
Kumbuka, BRELA iko chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara. Mamlaka nyingine zilizoko chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara ni SIDO, TBS na Wakala wa Vipimo (WMA-Weights and Measure Agency) na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (TANTRADE).
ADA YA USAJILI WA JINA LA BIASHARA (BUSINESS NAME REGISTRATION FEE)
|
Ada ya usajili wa Jina la Biashara ni shilingi za Kitanzania elfu sita tu 6,000/=. Kuna fomu maalum za kujaza ili kuweza kujisajili kama biasharar ya mtu binafsi au kama biashara ya ubia (watu zaidi ya mmoja mpaka 20). Fomu za maombi ya usajili wa Jina la Biashara zinapatikana katika tovuti ya Mkoa wa Kagera, na kwa maelezo zaidi ya msaada namna ya kusajili jina la biashara wasiliana na Ofisi ya Biashara Mkoa wa Kagera.
SOKO LA AFRIKA MASHARIKI
|
Hili ni soko la pamoja linalojumuisha nchi za Afrika Mashariki ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi. Ni soko kubwa sana lenye zaidi ya watu zaidi ya milioni 120 linaloruhusu mwingiliano wa bidhaa, watu, fedha, mitaji, huduma pamoja na masula ya forodha. Kuna fursa nyingi zinazotokana na soko la pamoja la Afrika Mashariki, ikiwa ni pamoja na idadi kubwa ya watu wanaohitaji bidhaa mbalimbali kutoka katika nchi wananchama mfano; mazao ya chakula kama mahindi, mchele, mihogo, viazi, sukari, nguo, magodoro, viatu, rasilimali watu, mitaji. Aidha Mkoa wa Kagera unayo fursa ya kipekee ya kijiografia kwa kuwa umepakana karibu na nchi zote za Afrika ya mashariki. Ni dhahili kuwa Wananchi wa Mkoa wa Kagera wanapaswa kuelewa umuhimu wa shirikisho hili kwa kuanza kuzalisha kwa wingi bidhaa na mazao mengi zaidi kwa ajili kuhudumia na kuuza kwa wingi katika nchi wananchama.
VIKWAZO NA CHANGAMOTO ZA BIASHARA MIPAKANI
|
• Uzalishaji duni wa mazao na bidhaa mbalimbali hivyo kupelekea kutokidhi mahitaji ya soko la ndani na nje.
• Ukosefu wa masoko ya mipakani.
• Ukosefu wa maghala maeneo ya mipakani kwa ajili ya kuhifadhia bidhaa/mazao.
• Maeneo ya mipakani hayana taasisi za fedha na benki kwa ajili ya kurahisisha huduma za kifedha mipakani.
• Biashara nyingi maeneo ya mipakani zipo upande wa nchi za jirani.
• Maeneo ya mipaka ya Tanzania hayana nishati ya umeme.
• Wafanyabiashara wengi wana elimu ndogo ya biashara ya kimataifa.
UHUSIANO WA MAMLKA ZA SERIKALI NA SEKTA YA BIASHARA
|
Sekta ya Biashara Mkoa wa Kagera imekuwa ikifanya kazi kwa karibu na mamlaka serikali mbalimbali kama ifuatavyo: Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na taasisi zilizopo chini ya wizara hii ambazo ni Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo SIDO (Kagera), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Wakala wa Vipimo Mkoa wa Kagera, Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), Mamlaka ya udhibiti wa Nishati (EWURA), Mamlaka ya Mapato Tanzania, Mamlakak ya Bandari, Kituo cha Uwekezaji Tanzania, Benki ya Rasilimali.
UWEKEZAJI KATIKA MKOA WA KAGERA |
Mkoa wa Kagera umekuwa na mikakati mbalimbali ya kuvutia wawekazaji kwa kushirikisha wadau mbalimbali wa maendeleo pamoja na Halmashauri za Wilaya. Mkoa umekuwa na wawekezaji mbalimbali wa ndani na nje ya nchi ingawaje uwekezaji huu unaendelea kufanyika kwa kiwango kidogo cha asilimia 5% hadi mwaka 2014
Dhana ya wananchi wengi katika uwekezaji hufikiria zaidi uwekezaji kutoka nje ya nchi badala ya wananchi wenyewe na pia hufikiria uwekezaji hufanywa na Serikali pekee. Ni wazi kuwa uwekezaji hauwezi kuendeshwa na uchumi wa Serikali na wala hakuna uchumi wa nchi yoyote unaoweza kukua kwa kutegemea uwekezaji wa umma bila kushirikisha wawekezaji binafsi. Sekta zote mbili zinabidi zishirikiane kwa pamoja kwa manufaa ya jamii.
MAENEO YA UWEKEZAJI MKOANI KAGERA
|
Wilaya zimeainisha maeneo takribani hekta 28,783 kwa ajili ya uwekezaji katika kilimo cha umwagiliaji na ujenzi wa viwanda vya kusindika mazao ya kilimo (Agro Processing Industries) ili kuongeza thamani ya mazao pamoja na uwekezaji wa biashara ndogo. Mengi ya maeneo haya bado hayajapimwa na kumilikiwa na Halmashauri zenyewe.
FURSA ZA UWEKEZAJI MKOANI KAGERA |
Mkoa wa Kagera unazo fursa nyingi na muhimu kwa ajili ya kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi. Uwekezaji unaweza kufanywa katika sekta za kilimo, viwanda, utalii, uvuvi, ufugaji na maliasili. Mkoa unayo maeneo mengi ya uwekezaji kama yalivyoainishwa hapo juu, hali ya hewa nzuri pamoja na fursa ya kijiografia ya Mkoa wa Kagera kupakana na nchi za Jumuiya ya Af rika Mashariki (Rwanda, Burundi na Uganda). Hata hivyo fursa hizo bado hazijatumika ipasavyo kutokana na hali ya uwekezaji Mkoani kuwa bado katika kiwango cha chini. Mkoa wa Kagera ni miongoni mwa mikoa 10 ya Tanzania bara ambayo uwekezaji wake uko chini ya asilimia moja (1%).
• Kutokana na uzalishaji mkubwa wa ndizi kiasi cha wastani wa tani milioni 1.4 kwa mwaka, tani 15,000 za mpunga, tani 250,000 za mahindi, tani 106,000 za maharage na tani 830,000 za mihongo; ipo fursa kubwa ya kuanzisha viwanda vya usindikaji na uongezaji thamani mazao haya ya kilimo.
• Mkoa unayo fursa ya kuanzisha mashamba makubwa ya mahindi na mpunga katika bonde la mto Nkenge na Mto ngono wilayani Missenyi kwa ajili ya uzalishaji utakaokidhi mahitaji makubwa ya chakula katika soko la Afrika Mashariki na Kati.
• Mkoa unayo fursa ya uwekezaji katika unenepeshaji wa mifugo kama ng'ombe, mbuzi na kondoo kutokana na maeneo ya malisho yaliyopo katika huria (ranches) za Kikulula, Missenyi, Kagoma, Mabale na Kitengule zenye ukubwa wa jumla ya Hekta 136,028.
• Uwekezaji katika viwanda vya kusindika nyama, ng'ozi na bidhaa zake kutokana na uwepo wa idadi kubwa ya mifugo; ng'ombe 520,000, mbuzi 580,000, kondoo katika wilaya za Ngara, Bukoba, Karagwe, Biharamulo, Muleba na Missenyi.
• Fursa ya uwekezaji katika ujenzi wa viwanda vya kusindika asali, uongezaji thamani asali na a mazao yake pamoja na viwanda vya kutengeneza vipodozi na madawa kutokana na matumizi ya asali.
• Uwekezaji katika ujenzi wa hoteli za kitalii, camping sites, kumbi za mikutano, na vivutio mbalimbali vya utalii.
• Kwa kuwa Mkoa umepataka na nchi za Uganda, Rwanda, Burundi na Kenya kwa upande wa ziwa Victoria kuna fursa ya ujenzi wa Vituo vya kubadirishia fedha (Beural De Change) kwa kuwa hadi 2014 hakuna kituo rasmi kilichoanzishwa.
• Uwekezaji katika sekta ya usafiri na usafirishaji kwa njia ya maji na ujenzi wa bandari ya kisasa katika visiwa vya Bumbile and Karebe Bukoba, Muleba na Missenyi.
• Uwekezaji katika ujenzi wa nyumba za kuishi za kisasa na majengo ya kibiashara katika maeneo ya Bukoba Manispaa, Missenyi (Mutukula) na Muleba kutokana na viwanja vipatavyo 7,000 vilivyopo ambavyo vimepimwa katika maeneo hayo.
MAENEO YA UWEKEZAJI
|
Mkoa kwa kushirikiana na Mamlaka za Serikali za Mitaa zimeainisha na kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya uwekezaji yenye ukubwa wa hekta 16,000.
Bonyeza hapa upate maeneo ya uwekezaji mkoani Kagera
UWEKEZAJI KISEKTA
|
Mkoa wa Kagera una Viwanda vikubwa saba (7) ambavyo ni Bukop Ltd, TANICA, Kagera Tea Company, Kagera Sugar Company, Amir Hamza (T) Ltd, Kagera Fish Company na Vic Fish Company. Kutokana na serikali kubinafsisha Viwanda viwili vya Kagera Sukari na Kiwanda cha Chai cha Maruku vimendelea kufanya vizuri katika uzalishaji na kuchangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi wa Mkoa na kuongeza ajira. Pamoja na viwanda hivyo vikubwa kuna viwanda vidogo mfumo wa SIDO vipatavyo 6,844 ambavyo vimeajili zaidi ya watu 80,000.
UWEKEZAJI KATIKA USAFIRISHAJI
|
Wadau wa maendeleo wamewekeza katika huduma za usafiri na usafirishaji kama ifuatavyo:
• Usafiri wa anga: Precissionair, Auric Air
• Usafiri wa majini: Marine Services Co. Ltd
• Usafiri wa Barabara: Magari ya abiria na mizigo
Uwekezaji katika mawasiliano: Mawasiliano haya ni pamoja na:
• Mawasiliano ya simu: TTCL, Vodacom, Tigo, Airtel na Zental.
• Mawasiliano ya Radio: Redio Tanzania, Radio Free Africa, Kasibante, Radio Vision, Radio Kwizela, Radio Karagwe na FADECO.
• Mawasiliano ya TV (Luninga): TBC, ITV na Chaneel Ten.
• Mawasiliano ya Mtandao (Internet providers):Yanapatikana katika kila Wilaya kupitia kampuni za Simbanet, TTCL, Vodacom,Tigo na Airtel.
ix) Uwekezaji katika mazao mbadala: Uwekezaji katika kilimo cha maua ni moja ya sekta muhimu kwa maendeleo ya taifa kutokana na kuchangia katika pato la taifa ikiwa ni pamoja na kutoa ajira kwa watu wengi.
Pamoja na uwekezaji huu, bado Mkoa unahamasisha uwekezaji katika maeneo kama vile Kilimo cha kibiashara, ujenzi wa viwanda vya kusindika mazao, huduma za kijamii zikiwemo ujenzi wa shule za sekondari na vyuo vya elimu ya juu na ufundi, zahanati na Hospitali na uzalishaji umeme.
• Miundombinu duni: Changamoto kubwa ambayo inachangia uwekezaji kuwa mdogo ni kuwepo kwa miundombinu isiyokidhi mahitaji. Ni muhimu miundombinu kuboreshwa kama vile umeme, maji mawasiliano na barabara.
• Ushiriki mdogo wa wawekezaji wa ndani: Ushiriki dhaifu wa wawekezaji wa ndani na hasa wakazi wa mkoa wa Kagera kunafanya suala zima la uwekezaji kuwa ni dhana isiyotekelezwa. Kuna umuhimu wa kujikita katika kuhamasisha kukuza uwekezaji kwa sababu una mchango mkubwa katika kufikia malengo ya maendeleo katika kuondoa umasikini, kuboresha maisha ya wananchi na kuongeza ajira katika jamii.
• Tatizo la Mitaji kwa ajili ya kuwezesha uwekezaji:Wakati serikali ikiweka mazingira mazuri ya kuwekeza ni wajibu wa benki na taasisi nyingine za fedha za hapa nchini kuwezesha wanananchi kuwekeza. Taasisi za fedha zinaweza kuchangia katika uwekezaji kwa kulegeza masharti na kupunguza viwango vya riba zinazotozwa kwenye mikopo.
• Nguvu kazi ya vijana kutotumia ipasavyo: Mkoa unaweza kufanya uwekezaji kwa kutumia vijana na kuongeza uzalishaji hatimaye kukuza uchumi na pato la Mkoa wa Kagera. Tatizo kubwa lililopo ambalo tunahitaji kupiga vita ni Uvivu na vijana wengi kukimbilia mijini kwa ajili ya shughuli za biashara ndogo za umachinga, uendeshaji pikipiki na baiskeli pamoja na uuzaji kahawa vijiweni. Hali hii imepelekea uzalishaji mashamani kushuka na hivyo uchumi wa Mkoa kukua kwa kasi ndogo.
Huko nyuma vijana wengi walikuwa wakienda jeshini kwa muda wa mwaka mmoja ambao waliutumia kufanya kazi za kilimo kwa kutumia majembe ya mikono kwenye mashamba makubwa ya Jeshi la Kujenga Taifa. Leo hii mpango huo unaweza kufanyiwa marekebisho kwa kila wilaya kuwa na mikakati ya kuwavutia vijana wasio na ajira kubuni kambi za uzalishaji wa mazao mbalimbali.
Uwekezaji ni chanzo cha maendeleo endelevu, ukuzaji ajira na kuleta mapato kwa wananchi na kupunguza umasikini. Ni muhimu kuwa na juhudi na mikakati ya pamoja katika kuvutia wawekezaji. Hakuna uchumi wa nchi yoyote duniani unaoweza kukua kwa uwekezaji wa Serikali peke yake bila kuvutia wawekezaji binafsi. Tuliujaribu mfumo huo huko nyuma na sote tunajua matokeo yake. Ni vyema sote kushikana mikono kuhamasisha jamii yetu kuwekeza katika fursa tulizonazo mkoani.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Postal Address: S.L.P 299 BUKOBA
Telephone: 255 28 2220215/17
Mobile:
Email: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 GWF . All rights reserved.