- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Rais Magufuli Ardhishwa na Uwekezaji wa Kiwanda Cha Kagera Sukari Asema Serikali Itaendelea Kukiunga Mkono
Rais Magufuli akiendelea na ziara yake Mkoani Kagera leo Novemba 8, 2017 katika siku ya tatu alitembelea Kiwanda cha Kagera Sukari kilichopo Wilayani Missenyi ambapo amempongeza mwekezaji wa kiwanda hicho Bw. Seif Seif kwa kuwekeza mtaji mkubwa katika kiwanda hicho.
Akiwa katika kiwanda hicho Rais Magufuli alitembelea mashamba ya kiwanda na kujionea jinsi mashamba yanavyoandaliwa kisasa kwa kutumia teknolojia ya hali ya juu katika umwagiliaji na jinsi sukari inavyozalishwa aidha na kujionea shehena ya sukari ambayo tayari imezalishwa tayari kuingizwa sokoni.
Aidha Rais Magufuli alipongeza uongozi wa kiwanda hicho kwa kutoa kipaumbele katika ajira kwa Watanzania wazalendo waliohitimu masomo yao katika Vyuo Vikuu vya hapa nchini na kuwaendeleza kielimu katika nchi za nje mara baada ya kuajiriwa katika kiwanda cha Kagera Sukari ili kupata ujuzi wa kilimo cha miwa ambapo hadi sasa kiwanda hicho kimeajiri wafanyakazi 5,000.
Hadi sasa Kiwanda cha Kagera Sukari kinazalisha tani 65,000 hadi tani 67,000 kwa mwaka ambapo Rais Magufuli alitoa maelekezo kiwanda hicho kizalishe tani 75,000 kufikia mwaka kesho 2018 na kuwahakikishia wenye viwanda vya sukari nchini kuwa soko la sukari lipo kubwa kwahiyo wanatakiwa kuzalisha zaidi.
“Kiwanda cha Mtibwa kinzalisha tani 30,000 TPC tani 100,000 Kilombero tani 109,000 Manyara tani 6,000 ukiunganisha na tani za Kagera Sukari kwaujumla tani zinazozalishwa nchini ni 320,000 wakati mahitaji tani 450,000 na upungufu ni tani 130,000. Ukiangalia wingi wa watu Afrika Mashariki ni milioni 165 na nchi za SADC ni milioni 400 hilo ni soko kubwa la sukari,” Alibainisha Rais Magufuli.
Rais Magufuli aliwataka wenye viwanda kumhakikishia kuwa wanao uwezo wa kuzalisha sukari kwa kiwango chote cha mahitaji tani 450,000 ili Serikali ipige marufuku uingizwaji wa sukaria nchini ambapo alisema kuwa sukari hiyo inayoingizwa nchini wakati mwingine ni ya viwandani na wafanyabiashara waroho wanaiuza kama sukari ya matumiazi ya binadamu.
“Nawataka mnihakikishie kuwa mna uwezo wa kuzalisha sukari tani 450,000 na wakati mnapofunga viwanda kama kutakuwepo na upungufu nyie wenyewe muagize sukari toka nje hapo nitakuwa tayari kufuta uingizwaji Sukari nchini. Lakini sharti ni kwamba sukari toka nje muiagize nyinyi wenye viwanda na siyo kuwapa vibali wafanyabaiashara,” Alisistiza Rais Magufuli.
Aidha Rais Magufuli aliwaagiza Mawaziri wa Kilimo, Waziri wa Viwanda Biashara na Uwekezaji kufanya upembuzi yakinifu katika viwanda vyote vinavyotumia sukari ili kujua matumizi halisi katika viwanda vyao na atakeyebainika anaagiza sukari ya viwandani zaidi ya matumizi yake afikishwe mahakamani kwa hatua za kisheria
Aidha Bw. Seif Seif kwaniaba ya Bodi ya Wakurugenzi wa Kiwanda cha Kagera Sukari na wafanyakazi wa Kiwanda hicho aliishukuru Serikali ya Rais magufuli kwa kuwapa ushirikiano katika kuendesha kilimo na kuzalisha sukari.
Aidha rais Magufuli alimwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano kuhakikisha wakandarasi wanakuwepo katika eneo linapotakiwa kujengwa daraja katika mto Kagera litakalozinganisha Wilaya za Karagwe na Missenyi ili kurahisisha usafirishaji wa miwa kutoka katika Wilaya ya Karagwe kuja kiwandani.
Raisi Magufuli alimalizia hotuba yake kwa wananchi na wafanyakazi wa Kiwanda cha Kagera Sukari kwa kuwaomba wawekezaji kuwekeza katika Mkoa wa Kagera na ili uwe Mkoa wa uwekezaji ambapo aliwataka Kagera Sukari kuanziasha Kiwanda kingine cha Kutengeneza pombe kali kutokana na morasisi na wananchi kuanzisha viwanda vidogovidogo kama vya senene na vinginevyo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa