- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
LENGO LA SEHEMU YA UTAWALA NA RASILIMALI WATU
Kutoa usaidizi wa utaalam na huduma za utawala na Menejimenti ya Utumishi kwenye Sekretarieti ya Mkoa
Sehemu hii inafanya kazi zifuatazo:-
UTANGULIZI
Wakati tunapata UHURU, mkoa wa Kagera ulikuwa na jumla ya wilaya nne (4), wilaya hizo ni Ngara ambayo ilianzishwa mwaka 1947, Biharamulo, Bukoba, na Karagwe mwaka 1958 ambayo ilizinduliwa rasmi na gavana wa kiingereza Sir Richard Turnbul. Aidha, mwaka 1975 wilaya mpya ya Muleba ilianzishwa kutoka kwenye wilaya ya Bukoba na mwaka 2007 wilaya ya Chato na Missenyi zilianzishwa na kuunda jumla ya wilaya 7 za mkoa wa Kagera.
Mwaka 2011, Wilaya ya Chato ilihamishiwa mkoa mpya wa Geita. Aidha, mwaka huo huo wa 2011 mkoa wa Kagera ulipata wilaya mpya ya Kyerwa ambayo ilipatikana baada ya kuigawa Wilaya ya Karagwe. Kwa sasa mkoa wa Kagera una jumla ya wilaya saba (7) na halmashauri 8. Wilaya hizo ni Bukoba, Muleba, Biharamulo, Ngara, Kyerwa, Karagwe, Missenyi na Ngara. Halmashauri ni Bukoba Manispaa, halmashauri ya wilaya ya Bukoba, Muleba, Biharamulo, Ngara, Kyerwa, Karagwe na Missenyi.
Kisiasa mkoa una jumla ya majimbo 10 ya uchaguzi (Muleba 2, Karagwe 1, Ngara 1, Biharamulo 1, Missenyi 1, Bukoba Manispaa 1, Bukoba Vijijini 1 na Kyerwa jimbo 1).
Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 1967 mkoa ulikuwa na watu 658,712, mwaka 1978 watu 1,009,379, mwaka 1988 mkoa ulikuwa na watu 1,326,183 na mwaka 2002 watu 2,033,888. Ongezeko la idadi ya watu lilikuwa kwa wastani wa asilimia 2.7. Aidha, mwaka 2012 kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 mkoa ulikuwa na jumla ya watu 2,458,023.
Mkoa unayo majimbo ya Uchaguzi 10 na wapo Wabunge 9 wa kuchaguliwa na Wabunge 3 wa viti maalum. Jumla ya Wabunge 11 wanatoka chama cha Mapinduzi (CCM) na Mbunge 1 anatoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo.
Uchumi wa mkoa unategemea zaidi kilimo ambapo zaidi ya asilimia 70 ya watu wanajishughulisha na kilimo cha mazao ya chakula na biashara. Shughuli za uvuvi, mifugo,viwanda na madini zinachangia pia katika uchumi wa mkoa.
Kwa kuzingatia malengo ya Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (MKUKUTA) , Dira ya Taifa ya mwaka 2025 na malengo ya Milenia, Mkoa wa Kagera unaendelea kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo na umepiga hatua katika sekta za uchumi, miundo mbinu na huduma za jamii. Hata hivyo pamoja na hatua hizi zilizopigwa, juhudi za wananchi mkoani za kujiletea maendeleo zinakumbana na matatizo na vikwazo mbalimbali ambavyo vimeendelea kupatiwa ufumbuzi kwenye mipango ya maendeleo ya Mkoa.
Mkoa wa Kagera umetenganishwa katika Kanda tano za kilimo kuzingatia mwinuko wa maeneo hayo kutoka usawa wa bahari na kiwango cha unyeshaji wa mvua.
•Ukanda wa kwanza : Ukanda huu unajumuisha maeneo ya mashariki ya wilaya ya Bukoba na Muleba yanayoambaa kandokando ya ziwa victoria na uko katika mwinuko wa mita 1,300 mpaka 1,500 kutoka usawa wa bahari. Mvua zinanyesha kwa wastani wa milimita 800 - 1,750 kwa mwaka. Shughuli kuu za kiuchumi katika eneo hili ni kilimo cha ndizi, maharagwe, mahindi na kahawa. Eneo la ukanda huu ni asilimia 17 ya eneo la Mkoa.
Ukanda wa pili : Huu ni ukanda wa juu ulioko kwenye mwinuko wa mita 1,400 mpaka 1,800 kutoka usawa wa bahari. Ukanda huu unajumuisha maeneo ya juu ya wilaya ya Karagwe na Ngara na mvua zinanyesha kwa wastani wa milimita 800-1,000 kwa mwaka. Mazao yanayolimwa kwenye ukanda huu ni ndizi, maharagwe, mahindi na kahawa. Eneo la ukanda huu ni asilimia 19 ya eneo la mkoa.
Ukanda wa Tatu : Ukanda huu uko katika mwinuko wa mita 1,000 kutoka usawa wa bahari na unajumuisha wilaya ya Ngara ,Biharamulo. Mvua zinanyesha kwa wastani wa milimita 750-800 kwa mwaka. Shughuli kuu za kiuchumi ni uzalishaji wa mazao ya mahindi, mihogo, mpunga, mtama, karanga na pamba. Eneo la ukanda huu ni asilimia 27 ya eneo la mkoa.
Ukanda wa Nne : Ukanda huu upo kwenye mwinuko wa mita 1,000 kutoa usawa wa bahari na unajumuisha maeneo ya mashariki ya wilaya ya Karagwe,wilaya ya Misenyi na maeneo ya magharibi ya wilaya ya Bukoba. Mvua zinanyesha kwa wastani wa milimita 800-1,000 kwa mwaka. Shughuli kuu za kiuchumi ni kilimo cha mazao ya mahindi,maharagwe na ufugaji. Eneo la ukanda huu ni asilimia 10 ya eneo la mkoa.
Ukanda wa Tano :Ukanda huu unajumuisha maeneo ya kaskazini ya wilaya ya Karagwe na Misenyi na uko kwenye mwinuko wa mita 1,000 kutoka usawa wa bahari .Ukanda huu unapata mvua za wastani wa milimita 750-800 kwa mwaka.Sehemu kubwa ya ukanda huu ni misitu ya hifadhi na mapori ya akiba. Eneo la ukanda huu ni asilimia 27 ya eneo la mkoa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa