- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti azindua rasmi maadhimisho ya Wiki ya Sheria nchini Mkoani Kagera kwa kupokea maandamano ya wadau mbalimbali wa Sheria wakiongozwa na Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Bukoba Mhe. Lucia Gamuya Kairo.
Katika hotuba yake ya uzinduzi Mkuu wa Mkoa Gaguti alitoa kilio chake kwa Mawakili hasa wale wa kujitegemea kuwa wakweli na kumtanguliza Mungu katika kutekeleza majukumu yao ya huduma kwa wananchi katika masuala ya kisheria.
“Kwa moyo wa dhati kabisa niwaombe Mawakili hasa wa kujitegemea muwe wakweli kwa wateja wenu, mwananchi anapokuja kwako na hoja yake msikilize kwa umakini ukiona hoja yake haina mashiko mbele ya sheria mwambie ukweli kuwa hata akienda Mahakamani hawezi kushinda kesi hiyo kuliko kumdanganya na kupoteza muda na fedha zake Mahakamani. “ Alisisitiza Mkuu wa Mkoa Gaguti.
Pia Mkuu wa Mkoa gaguti aliwataka Mawakili hao kumtanguliza Mungu katika kazi zao ili wanapokuwa wanatoa msaada wa kisheria kwa wananchi wasiongozwe na tama za kibinadamu ili wateja wanaowatetea washinde mashauri yao kwa haki bila dhuruma au kupindisha haki.
Kwa upande wa wananchi Mkuu wa Mkoa Gaguti alitoa rai kwao hasa katika Mkoa wa Kagera kuwa nao wanapaswa kuridhika na maamuzi ya Makama pale yanapotolewa. “Unakuta kesi ilishaamuliwa mpaka Mahakama ya Rufani lakini mwananchi haridhiki akiona huko hakushinda anakuja kwa Mkuu wa Mkoa au Mkuu wa Wilaya kushinikiza kufuta hukumu jambo ambalo si sawa.” Alisema Mhe. Gaguti.
Katika hatua nyingine Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Bukoba Mhe. Lucia Gamuya Kairo alisema kuwa katika Maadhimisho ya Wiki ya Sheria Mahakama itatembelea maeneo mbalimbali mkoani Kagera kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi na maeneo hayo ni Magereza, Shule mbalimbali za Sekondari, na maeneo ya wazi kama soko kuu na kituo kikuu cha Mabasi Bukoba.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa Gaguti alivitaka Vyombo vya Habari Mkoani Kagera hasa Redio za Kijamii kuitumia Wiki ya Sheria nchini iliyozinduliwa rasmi Mkoani Kagera Februari 1, 2020 kurusha vipindi mubshara kutoka katika maeneo mbalimbali wadau wa Sheria watakakokuwa wanatoa misaada ya kisheria ili kutoa elimu kwa wananchi walioko manyumbani.
Mwisho Mkuu wa Mkoa Gaguti akizungumzia Kaulimbiu ya Mwaka huu 2020 isemayo “Uwekezaji na Biashara: Wajibu wa Mahakama na Wadau kuweka Mazingira Wezeshi ya Uwekezaji.” Aliwasisitiza wadau wote wa uwekezaji wanaopenda kuja kuwekeza katika mkoa wa Kagera kuhakikisha wanafuata na kukamilisha taratibu zote za kisheria ili kuepuka migogoro isiyokuwa ya lazima hapo mbeleni.
Maadhimisho ya Wiki ya Sheria imezinduliwa leo Februari 1, 2020 na kilele chake kitakuwa tarehe 6/02/2020. Ikumbukwe kuwa mkoa wa Kagera unahitaji watendaji wa kutosha katika masuala ya kisheria kutokana na wingi watu. Kagera ni mkoa wa tatu kwa wingi wa watu ukiacha mikoa ya Dar es Saalam na Mwanza kwa takwimu za mwaka 2019 ambazo zimetolewa hivi karibuni, Kagera kuna jumla ya watu 3,127,908 ukilinganisha na takwimu za mwaka 2012 watu 2,458,023.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa