- Home
- About Us
- Administration
- Districts
- District Councils
- Investment Opportunities
- Services
- Publications
- Media Center
Familia ya Mwanafunzi Marehemu Spelius Erdius (13) aliyefariki baada ya kupigwa na Mwalimu wa nidhamu Respecius Patrick (50) Shule ya Msingi Kibeta Manispaa ya Bukoba yaridhika na hatua zilizochukuliwa na Serikali baada ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti kuwasili kwenye familia ya Mwanafunzi huyo na kutoa ufafanuzi wa hatua zilizochukuliwa na Serikali baada ya tukio hilo kutokea pia na kuwapa pole wafiwa na wananchi wa Kibeta.
Mara baada ya kuwasili katika familia ya Marehemu Spelius Eradius leo Agosti 30, 2018 majira ya saa 6:00 mchana Mkuu wa Mkoa Gaguti alitoa pole kwa wafiwa na kuongea na familia pia na wananchi wa Mtaa wa Nyamurugo Kata ya Kibeta na kusema kuwa Serikali inaendelea kufanya uchunguzi wa tukio hilo pia itahakikisha haki inatendeka kwa kuwachukulia hatua za kisheria wale wote watakaobainika kushiriki katika tukio hilo.
“Sisi Serikali hatukumtuma Mwalimu Respicius Patrick kufanya aliyoyafanya kwahiyo sheria itachukua mkondo wake na haki itatendeka kwa kila mhusika aliyehusika katika tukio hilo lililosababisha kifo cha Mwanfunzi Spelius Eradis katika Shule ya Msingi Kibeta.” Alisistiza Mkuu wa Mkoa Gaguti.
Aidha, Mhe Gaguti alisema kuwa kutokana na taarifa ya uchunguzi ya kifo cha Spelius Eradius iliyotolewa na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera kuleta manunguniko kwa familia na baadhi ya wananchi, Serikali iliamua kumleta Mtaalam wa uchunguzi kutoka nje ya mkoa na tayari uchunguzi ulikuwa umefanyika kwa kuwahusisha familia ambayo imekubaliana na uchunguzi huo.
Mara baada ya Mkuu wa Mkoa Gaguti kuongea na familia ya Marehemu Spelius Eradius na wananchi wa Mtaa wa Nyamurugo baba mlezi wa marehemu Mchungaji Justus Balilemwa alisema kuwa anaishukuru Serikali hasa Mkuu wa Mkoa kuchukua hatua za haraka na kulifuatilia suala hilo kwa karibu ambapo alikubali kuwa sasa familia itaendelea na utaratibu wa mazishi ya Mwanafunzi Spelius Eradius.
Naye Diwani wa Kata ya Kibeta Mchungaji Islael Mlaki kwaniaba ya wananchi wa Kata Kibeta aliushukuru uongozi wa Mkoa ukiongozwa na Mkuu wa Mkoa Mhe. Gaguti katika kulishughulikia suala la kifo cha Mwanafunzi Spelius Eradius ambalo lilileta taaharuki katika Kata hiyo na alisema kuwa baada ya Mkuu wa Mkoa kutoa ufafanuzi wananchi wameidhika na wataendelea na taratibu za kumuaga mpendwa wao.
Hatua Zilizochukuliwa kwa Watendaji
Mkuu wa Mkoa Mhe. Gaguti pia alifika Shuleni Kibeta na kukutana na Walimu, Kamati ya Shule na Wanafunzi ambapo mara baada ya kuongea na kamati ya Shule alisema pamoja na uchunguzi wa Jeshi la Polisi kuendelea lakini pia alimwagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba kuunda Kamati ya Uchunguzi ili kuchunguza mwenendo wa utoaji wa adhabu shuleni, Pili kuchunguza kama viongozi waliopewa dhamana ya uongozi kama walikuwa wanawajibika ipasavyo.
Katika Agizo hilo Mkuu wa Mkoa Mhe. Gaguti alimwagiza Mkurugenzi wa Manispaaya Bukoba kuwasimamisha kazi Mwalimu Mkuu Bi Renatha Isidory, Mwalimu Mkuu Msaidizi Sunday Elisha na Afisa Elimu Kata Bw. Hashim Mponda ili kupisha uchunguzi wa Kamati iliyoudwa. Kama waliotajwa wakikutwa hawakuwajibika ipasavyo watachukuliwa hatua kwa mujibu wa na kanuni, taratibu na Sheria za nchi.
Aidha, Mkuu wa Mkoa Mhe. Gaguti alimwagiza Mkurugezi wa Manispaa ya Bukoba pia kuisimamisha mara moja Kamati ya Shule hiyo nayo kupisha uchunguzi kama ilikuwa ikiwajibika na kutekeleza majukumu yake ipasavyo katika Shule ya Msingi Kibeta Manispaa ya Bukoba.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa Gaguti aliwataka wazazi na walezi wa wanafunzi wanaosoma katika Shule ya Msingi Kibeta kuwaruhusu watoto wao kuendelea kuhudhuria masomo katika shule hiyo kwani hakuna tena tishio katika shule hiyo. Pia wanafunzi wa Darasa la Saba wanatakiwa kujiandaa na Mtihani wa kuhitimu Elimu ya Msingi na hakuna sababu ya wazazi kuwazuia wanafunzi wasihudhurie masomo yao.
Vilevile aliwataka Walimu kuzingatia weledi katika kutekeleza majukumu yao kwa kufauata Sheria, Kanuni na Miongozo ya kazi zao. Na alisema kuwa baadhi ya walimu wamekuwa na tabia zisizoendana na maadili ya ualimu kwani kufuatia tukio hilo pia alipokea malalamiko ya Mwalimu Respicius Patrick mtuhumiwa kuwa kabla ya tukio hilo alikuwa akiwapa adhabu wanafunzi za kuwatoa ngeu na makovu jambo ambao halikubaliki katika utumishi wa umma.
Marehemu Spelius Eradius (13) aliyekuwa mwanafunzi wa Shule ya Msingi Kibeta Kata Kibeta Manispaa ya Bukoba anayesadikiwa kufariki dunia Agosti 27, 2018 baada ya Mwalimu wa nidhamu wa shule hiyo Mwalimu Respicius Patrick kumpiga na kumsbabishia maumivu yaliyopelekea kifo chake mwili wake utaagwa Agosti 31,2018 nyumbani kwa walezi wake Mtaa wa Nyamurugo Kata kibeta na baadae utasafirishwa kuzikwa nyumbani kwa baba yake Mubunda Kijiji Kitoko Wilaya ya Muleba.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Postal Address: S.L.P 299 BUKOBA
Telephone: 255 28 2220215/17
Mobile:
Email: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 GWF . All rights reserved.