- Home
- About Us
- Administration
- Districts
- District Councils
- Investment Opportunities
- Services
- Publications
- Media Center
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti atekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli la kugawa vitambulisho kwa Wajasiliamli Wadogo ili waweze kufanya shughuli zao za ujasiliamali na kujiingizia kipato chao cha kila siku bila kusumbuliwa na mtu yeyote.
Mkuu wa Mkoa Gaguti ametekeleza agizo hilo la Rais Magufuli Desemba 20, 2018 katika Uwanja wa Uhuru (Maarufu kama Mayunga) Manispaa ya Bukoba ambapo alivigawa vitambulisho hivyo kwa Wakuu wa Wilaya zote za Mkoa wa Kagera na Halmashauri zake nane.
Kabla ya kugawa vitambulisho hivyo kwa Wakuu wa Wilaya na Baadhi ya wajasiliamali wachache wa Manispaa ya Bukoba Mkuu wa Mkoa Gaguti alisema kuwa Mkoa wa Kagera ulipewa vitambulisho jumla 25,000 vilivyotolewa na Rais Magufuli na kusisitiza kuwa vitambulisho hivyo vikigawiwa na kuisha uongozi wa mko utaomba vingine zaidi ili kuhakikisha kila Mjasiliamali Mdogo anapata kitambulisho hicho.
Mkuu wa Mkoa Gaguti alitoa angalizo kuwa vitambulisho hivyo vinawalenga Wajailiamali au Wafanyabiashara Wadogo na wanatakiwa kuwa walinzi wao wenyewe kujilinda ili waweze kujiingizia kipato chao bila kusumbuliwa lakini wasiwe mawakala wa wafanyabiashara wakubwa ili kuwafanyia biashara kwa kutumia vitambulisho hivyo.
“Rais Magufuli alitoa maelekezo kuwa hakuna Mjasiliamali yeyote ambaye atakuwa na kitambulisho na kusumbuliwa, pia na mimi Mkuu wa Mkoa wa Kagera narudia na kuagiza kuwa Mjasiliamali Mdogo yeyote ambaye atakuwa na kitambulisho na kusumbuliwa na mtu yeyote katika mipaka ya Mkoa wa Kagera.” Alisisitiza Mkuu wa Mkoa Gaguti
Aidha, Mkuu wa Mkoa Gaguti aliwatahadharisha wafanyabiasha wadanganyifu kuwa tayari ofisi yake imepata taarifa kuwa kuna baadhi ya Wafanyabiashara wasio waaminifu kuwa wameanza kupunguza bidhaa kwenye chanja za maduka yao ili waweze kutambuliwa kama Wajasiliamali Wadogo wakilenga kupata vitambulisho. “Ukibainika umefanya mchezo huo hatua kali zitachukuliwa kwa kuzingatia sheria na katika zoezi hili Serikali itasimaia sheria ipasavyo.” Alitahadharisha Mkuu wa Mkoa Gaguti.
Hatua zitakazochukuliwa ni pamoja na wafanyabiashara watakaogundulika kufanya mchezo wa udanganyifu ni pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzani kuwafutia moja kwa moja leseni za biashara. Aidha, Viongozi wa Serikali za Mitaa na Watendaji wa Kata walitakiwa kutenda haki katika utambuzi wa Wajasiliamali Wadogo katika maeneo yao. Pia wananchi walitakiwa kupaza sauti pale watakapoona zoezi hilo linaendeshwa bila kutenda haki.
Naye Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kagera Bw. Adam Ntoga alitoa ufafanuzi wa ni Mjasiliamali yupi Mdogo anatakiwa kupata kitambulisho ambapo alisema kuwa ni Wajasiliamali wadogo ambao hawajawahi kutambuliwa na mfumo wa kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania na mzunguko wao wa fedha haufikii kiasi cha shilingi milioni nne. Pia Bw. Ntoga alisema kuwa malipo ya kitambulisho hicho ni shilingi 20,000/- tu.
Katika Mkoa wa Kagera Wilaya ya Bukoba ilipatiwa jumla ya vitambulisho 3,580 na Wilaya za Missenyi, Karagwe, Kyerwa, Ngara, Biharamulo na Muleba kila Wilaya kupitia Wakuu wa Wilaya zilipatiwa vitambulisho 3,570 na kukamilisha jumla ya Vitambulisho 25,000 vilivyotolewa katika Mkoa wa Kagera na Rais Magufuli Desemba 10, 2018
Ikumbukwe kuwa Desmba 10, 2018 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli akiwa Ikulu Jijini Dar es Salaam alitoa vitambulisho vya wajasiliamali wadogo 670,000 kwa Wakuu wa Mikoa yote na kila Mkoa ulipatiwa vitambulisho 25,000 na Mkoa wa Kagera ukiwemo ambapo Rais Magufuli alisema kuwa kila Mkuu wa Mkoa atakusanya shilingi 500 milioni kupitia vitambulisho hivyo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Postal Address: S.L.P 299 BUKOBA
Telephone: 255 28 2220215/17
Mobile:
Email: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 GWF . All rights reserved.