- Home
- About Us
- Administration
- Districts
- District Councils
- Investment Opportunities
- Services
- Publications
- Media Center
Katika kuhakikisha azma yake ya kuufanya Mkoa wa Kagera unakuwa kinara katika ukusanyaji wa kodi kwa asilimia 100% kama ambavyo alitangaza mwezi Januari 11, 2019 kuwa mwaka 2019 utakuwa mwaka wa Kodi Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti Mkuu wa Mkoa wa Kagera akishirikiana na Maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoani Kagera apita mitaani kwa Wafanyabiashara katika Manispaa ya Bukoba na kuwaelimisha juu ya kutumia mashine za Kielektroniki za kutolea risiti (EFD)
Februari 28, 2019 Mkuu wa Mkoa Gaguti na Meneja wa TRA Mkoa wa Kagera Bw. Adam Ntoga pamoja na maafisa wengine walipita kwa wafanyabiashara katika mitaa ya Rwamishenye, Kashai Mafumbo na Soko Kuu (almaarufu kama SENATE) kwa kutembelea baadhi ya maduka na kutoa elimu kwa wafanyabiashara ambao biashara zao zinaonesha kuwa wanatakiwa kuwa na mashine za EFD lakini hawana.
Mkuu wa Mkoa Gaguti alikuwa akiwaelimisha wafanyabiashara hao kuwa ni muhimu sana kutumia mashine hizo kwa kutoa risiti kwani Serikali inakosa mapato kutokana na wao kukwepa kuzitumia mashine za EFD ambapo kupitia kodi hizo zinazokusanywa ndizo zinatumika kujenga miundombinu ya kutolea huduma mbalimbali za kijamii kama barabara, shule, Hospitali pamoja na kutekeleza miradi mingi ya maendeleo kwa wananchi.
Baadhi ya wafanyabiashara waliotembelewa walikutwa wanao uwezo wa kuwa na mashine za EFD kutokana na biashara zao zinavyoonekana pia na wao wenyewe kukiri kwa vinywa vyao kiasi cha fedha wanchoingiza kwa mauzo ya siku lakini hawana mashine hizo bali wana vitabu vya risiti ambavyo navyo hawavitumii ipasavyo kutoa risiti kwa wateja wao wanaowauzia bidhaa mbalimbali.
Mfano mama Faima Sylvester mfanyabiashara ya vifaa vya shule katika mtaa wa Rwamishenye alikutwa hana mashine ya EFD lakini alikuwa na kitabu cha kutolea risiti ambacho tangu mwaka 2016 alikuwa ametumia kurasa kama tatu tu hadi mwaka huu 2019. Baada ya kuelimishwa na Mkuu wa Mkoa na timu yake alikiri kuwa baada ya wiki moja atakuwa ameshughulika na kupata mashine hiyo ya EFD ili akadiriwe vizuri baishara yake na TRA.
Akiwa Soko Kuu la Bukoba Senate Mkuu wa Mkoa Gaguti aliwaelimisha pia wananchi waliohudhuria kumsikiliza kuwa ni wajibu wao kuomba risiti pale wanaponunua bidhaa mbalimbali madukani. Pia alitolea mfano wa Bwana mmoja aliyekamatwa na alikuwepo mbele ya wananchi akisafirisha nondo, saruji na baadhi ya vifaa vingine vya ujenzi bila kuwa na risiti ya dukani alikonunua vifaa hivyo.
Naye Bw. Adam Ntoga Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kagera katika kuwaelimisha wafanyabiashara alikuwa anawaeleza kuwa kwa kila mfanyabiashara anayeingiza kiasi cha shilingi 39,000/= kwa siku na kwa mwaka ni zaidi ya shilingi milioni 14 anatakiwa kuwa na mashine ya kielektroniki ya kutolea risiti EFD.
Aidha, Bw. Ntoga aliwaeleza wafanyabiashara kuwa mashine za EFD zinatolewa bure na Serikali lakini mfanyabiashara anatakiwa kulipia kiasi cha shilingi 590,000/= mwanzoni na baada ya TRA kumkadiria kodi anayotakiwa kulipa kwa mwaka fedha hizo zinarejeshwa kwa njia ya kutokatwa kwenye kodi ambayo atakuwa amekadiriwa.
Ikumbukwe kuwa ni wajibu na haki ya kila mwananchi kudai risiti kila akinunua bidhaa yoyote na mfanyabishara anawajibu wa kutoa risiti tena yenye thamani halisi ya kiwango cha fedha zilizonunua bidhaa hizo. Aidha, mwananchi ukikamatwa na bidhaa yoyote ambayo umeinunua na huna rsisti yake utawajibishwa kwa mujibu wa sheria kwa kukwepa kodi ya Serikali lakini pia bidhaa hiyo inaweza kukuweka matatani kuwa ya wizi.
Juhudi za Mkuu wa Mkoa wa Kagera kama zikitiliwa maanani na wananchi na wafanyabiashara na kujenga utamaduni wa kulipa kodi au kudai risiti ndio chanzo cha mkoa kupiga hatua kubwa za maendeleo kwani fedha za kodi zitawasaidia wananchi katika kuwaletea huduma karibu kutoka katika Serikali yao.
Mfano mzuri ni Mkoa wa Kagera sasa tayari umepewa fedha bilioni 4.5 bilioni 1.5 kila Wilaya kwa Wilaya za Bukoba, Karagwe na Kyerwa kujenga Hospitali za Wilaya na tayari ujenzi umeanza na unaendelea. Pili Serikali imetoa bilioni 1.4 kuikarabati Shule ya Sekondari Bukoba (Maarufu kama Bukoba Sec) katika Manispaa ya Bukoba. Tatu Serikali imetoa bilioni 5.9 na kujenga vituo 14 vya afya katika maeneo mbalimbali Mkoani Kagera hizo zote ni kodi za wananchi.
Wito wa Mkoa wa Kagera ni ewe mfanyabiashara lipa kodi kwa manufaa ya mkoa wako na ustawi wa nchi yetu. Serikali ya Awamu ya Tano sasa imeamua kuleta maendeleo kwa wananchi kupitia kodi zao lakini kodi rafiki ambayo haimbugudhi mfanyabiashara bali kumfanya naye apige hatua kutoka pale alipo na kusonga mbele bila kufungiwa biashara zake bali kwa kuelimishwa na kuelekezwa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Postal Address: S.L.P 299 BUKOBA
Telephone: 255 28 2220215/17
Mobile:
Email: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 GWF . All rights reserved.