- Home
- About Us
- Administration
- Districts
- District Councils
- Investment Opportunities
- Services
- Publications
- Media Center
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti awaongoza Wadau wa Elimu Mkoani Kagera kuweka mikakati ya muda mfupi na mda mrefu ili kuhakikisha wanafunzi 14,046 kati ya wanafunzi 39,545 waliofaulu Mtihani wa Darasa la Saba mwaka 2018 na kukosa Vyumba vya Madarasa wanaanza masomo yao kama wenzao 25,499 ifikapo Januari 7, 2019.
Mikakati hiyo iliwekwa katika kikao cha Wadau wa Elimu wa Mkoa wa Kagera kilichofanyika Mkoani hapa Desemba 18, 2018 katika ukumbi wa Halmashauri Wilaya ya Bukoba na kuongozwa na Mhe. Gaguti ambapo baada ya majadiliano ya muda mrefu katika kikao hicho wadau walikubaliana kuwa na mikakati ya muda mfupi na muda mrefu ili kuokoa jahazi la wanafunzi 14,046 ambao wamefaulu kuingia kidato cha kwanza na wangekosa vyumba vya madarasa shule zinapofunguliwa Januari 7, 2018.
Mikakati ya muda mfupi ni pamoja na Shule ambazo zipo maeneno ya mijini ambapo wanafunzi hawatoki mbali na shule hizo uwekwe utaratibu wa ufundishaji kwa awamu mbili, awamu ya kwanza asubuhi na awamu ya pi mchana wakati vyumba vya madarasa vikiendelea kukamilishwa. Pili, Mamlaka za Serikali za Mitaa zihakikishe zinakamilisha vyumba 351 pamoja na samani zake ifikapo Januari 7, 2019 wanafunzi wote waliofaulu waweze kuingia madarasani.
Mkakati mfupi wa tatu ni Fedha za mifuko ya Majimbo zielekezwe katika ujenzi wa madarasa ili kukamilisha haraka ujenzi wa miundombinu hiyo na kuruhusu wanafunzi 14,046 kuingia madarasani. Aidha, mipango ya muda mrefu ni pamoja na Mkoa kupadisha asilimia ya kiwango cha ufaulu cha sasa cha asilimia 84.42% hadi asilimia 95% ifikapo Desemba 2019.
Pili, Mipango ya Halmashauri za Wilaya izingatie uhalisia wa takwimu ili kuweka maoteo sahihi ya miundombinu ya elimu.Tatu, Mkoa wa Kagera kupunguza mimba za utotoni kwa asilimia 50% ifikapo Desemba 2019. Mwisho Kikao cha Wadau kifanyike mwezi Machi 2019 kujadili namna ya kutatua changamoto za Elimu Mkoani Kagera na kuona mikakati iliyowekwa ya muda mfupi kama imetekelezeka.
Matokeo ya Wanafunzi wanaotarajiwa Kujiunga Kidato cha Kwanza mwaka 2019
Mwaka 2018 Mkoa wa Kagera ulikuwa na jumla ya watahiniwa 47,197 waliotarajiwa kufanya mtihani wa kumaliza Elimu ya Msingi. Kati ya hao wavulana walikuwa 22,124 na wasichana 25,073. Watahiniwa waliohitimu ni 46,795 sawa na asilimia 99.11 ya wanafunzi waliotarajiwa. Vile vile kuna jumla ya Wanafunzi 86 wenye mahitaji maalum, kati yao wavulana ni 50 na wasichana ni 36.
Watahiniwa waliofaulu ni 39,545 sawa na asilimia 84.42 ya watahiniwa waliofanya mtihani, ambapo miongoni mwao ni wavulana ni 18,553 na wasichana ni 20,992. Kiwango cha ufaulu kimepanda kwa asilimia 0.02 ukilinganisha na kiwango cha ufaulu cha asilimia 84.4. kwa mwaka 2017. Kiwango cha ufaulu kilichokuwa kipangwa katika mkoa kilikuwa ni 88%.
Jumla ya wanafunzi 25,499 ambapo miongoni mwao wavulana 12,356 na wasichana 13,143 sawa na asilimia 64.48, ndio waliopata nafasi ya kujinga kidato cha kwanza kwa awamu hii ya kwanza kwa kuzingatia vyumba vya madarasa vilivyopo. Aidha wanafunzi 14,046 wakiwemo wavulana 6,257 na wasichana 7,789 sawa na 35.52% wamefaulu lakini kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa wanasubiri ujenzi wa vyumba vya madarasa kukamilika.
Mahitaji ya Miundombinu katika Shule za Sekondari
Vyumba vya Madarasa vinavyohitajika ni 791, vilivyopo ni 546, Upungufu ni vyumba 245 sawa na asilimia 30.96%. Vyumba hivyo vilivyopo vya madarasa vitachukua wanafunzi wa kidato cha kwanza 25,499 wavulana wakiwa 12,356 Wasichana 13,143 sawa na asilimia 64.5. Vyumba vya Maabara katika Shule za Sekondari Mahitaji ni 570 vilivyopo 218 upungufu 352 sawa na asilimia 61.75 (Taarifa nyingi za kitakwimu Tembelea Tovuti ya Mkoa wa Kagera www.kagera.go.tz)
Pamoja na Mkoa wa Kagera kuweka mikakati ya kuhakikisha wanafunzi wote waliofaulu mtihani wa darasa la saba wanakwenda Shule za Sekondari mwaka 2019 lakini Mkuu wa Mkoa Mhe. Gaguti aliwapongeza wadau wote wa Elimu pamoja na wananchi wote wa Kagera kwa kutambua umuhimu wa elimu na kuufanya Mkoa kushika nafasi za juu katika ufaulu kwenye mitihani mbalimbali ya Kitaifa.
“Nawapongeza sana wote mliopo hapa pia na wananchi wote wa Mkoa wa Kagera kwa kutambua umuhimu wa Elimu kwani Mtihani wa Darasa la Saba mwaka huu 2018 Mkoa umeshika nafasi ya 5 kati ya Mikoa 26, Matokeo ya Kidato cha Nne mwaka 2017 Mkoa ulishika nafasi ya 9 kati ya Mikoa 26, Matokeo ya Kidato cha Sita Mkoa ulishika nafasi ya 5 kati ya Mikoa 26, na Mkoa wa Kagera umeongoza kwa kushika nafasi ya kwanza kwa miaka miwili mfurulizo katika Matokeo ya Darasa la Nne.” Alitoa Shukrani Mkuu wa Mkoa Gaguti.
Mhe. Gaguti alimalizia kwa kuwataka Wadau wa Elimu na wananchi wote katika Mkoa wa Kagera kuhakikisha wanashirikiana na kuendelea kuinua zaidi kiwango cha elimu kufikia asilimia 95% kutoka asilimia ya sasa 84.42% pia Mkoa wa Kagera kuongoza kwa kushika nafasi za kwanza katika mitihani yote ya Kitaifa.
Ufaulu katika Mkoa wa Kagera ngazi ya Halmashauri, Halimashauri ya Wilaya ya Biharamulo imekuwa ya 1 kimkoa (Kitaifa ya 11) mwaka huu 2018, mwaka 2017 ilikuwa ya 2 Kimkoa (Kitaifa ya 19). Bukoba Manispaa imekuwa ya 2 Kimkoa na 20 Kitaifa na mwaka 2017 ilikuwa ya 1 Kimkoa na ya 12 Kitaifa. Ngara imekuwa ya 3 Kimkoa na ya 30 Kitaifa mwaka 2017 ilikuwa ya 8 Kimkoa na ya 52 Kitaifa. Muleba imekuwa ya 4 Kimkoa nay a 38 Kitaifa na Mwaka 2017 ilikuwa ya 3 Kimkoa na Kitaifa ya 23.
Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi imekuwa ya 5 Kimkoa na Kitaifa ya 48 na mwaka 2017 ilikuwa ya 5 Kimkoa na ya 35 Kitaifa. Bukoba Vijijini imekuwa ya 6 Kimkoa na ya 66 Kitaifa na mwaka 2017 ilikuwa 4 na ya 25 Kitaifa. Kyerwa imekuwa ya 7 Kimkoa na ya 91 Kitaifa na mwaka 2017 ilikuwa ya 7 Kimkoa na ya 49 Kitafa. Karagwe imekuwa ya mwisho ya 8 Kimkoa na ya 96 Kitaifa na mwaka 2017 ilikuwa ya 6 Kimkoa na ya 36 Kitaifa ambapo Karagwe ilikabidhiwa kinyago na Mkuu wa Mkoa kwa kushika nafasi ya mwisho Kimkoa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Postal Address: S.L.P 299 BUKOBA
Telephone: 255 28 2220215/17
Mobile:
Email: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 GWF . All rights reserved.