- Home
- About Us
- Administration
- Districts
- District Councils
- Investment Opportunities
- Services
- Publications
- Media Center
Mkuu wa Mkoa wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Elisha Gaguti anawajulisha wananchi wote wa Kagera kuwa Mkoa utapokea Mwenge wa Uhuru tarehe 24 Aprili, 2019 katika eneo la Murusagamba mpakani mwa Mkoa wa Kigoma na Kagera na baadae Mwenge wa Uhuru utaanza mbio zake katika mkoa wa Kagera katika Wilaya ya Ngara.
Mwenge wa Uhuru ukikimbizwa Mkoani Kagera unatarajiwa kuzindua, kuweka Mawe ya Msingi, na Kukagua miradi ya maendeleo jumla 74 yenye thamani ya shilingi bilioni 18,894,323,585.90 Ambapo katika fedha hizo Serikali Kuu imechangia shilingi bilioni 10,262,407,160.86 sawa na asilimia 54.31%. Halmashauri za Wilaya na Manispaa ya Bukoba zimechangia shilingi milioni 282,853,162.91 sawa na asilimia 1.5%. Wahisani wamechangia shilingi bilioni 2,472,529,017.96 sawa na asilimia 13.09%. Pia wananchi wamechangia shilingi bilioni 5,876,534,244.17 sawa na asilimia 31.10%.
Miradi 74 ya Maendeleo katika sekta za Afya, Elimu, Maji, Kilimo, Barabara, Ujasiliamali kwa Watu wenye ulemavu Vijana na Wananwake, Viwanda, Mapambano dhidi ya Rushwa na Madawa ya Kulevya itatembelewa, kukaguliwa, kuzinduliwa na Kuwekewa Mawe ya Msingi na Mwenge wa Uhuru Mkoani Kagera. Aidha, Miradi 21 itazinduliwa, Miradi 12 itawekewa Mawe ya Msingi, na Miradi 38 itatembelewa na kukaguliwa na Mwenge wa Uhuru pia miradi 3 ni ya shughuli nyinginezo.
Aidha, Kauli Mbiu ya Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu 2019 ni “Maji ni Haki ya Kila Mtu, Tutunze Vyanzo Vyake na Tukumbuke Kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa”. Kauli mbiu hii inawahamasisha wananchi hususani wa Mkoa wa Kagera kuhakikisha wanalinda vyanzo vya maji na kutunza mazingira kama ilivyo haki ya kila mtu kupata maji na iwe haki ya kila mtu kutunza vyanzo vya maji ili kurahisisha upatikanaji wa maji.
Pia, Mkoa wa Kagera tayari umeanza na unaendelea kuwahamasisha wananchi pamoja na vijana ambao watakuwa wametimiza umri wa miaka 18 (umri wa kupiga kura) ili washiriki katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu 2019. Mkoa wa Kagera unatarajia kuandikisha wananchi 1,277,776 watakaopiga kura katika vituo vipatavyo 3,798.
Pamoja na Kauli Mbiu tajwa hapo juu Mbio za Mwenge wa Uhuru katika Mkoa wetu zitaendelea kuwahamasisha wananchi kuhusu Mapambano dhidi ya Rushwa, VVU/UKIMWI, Matumizi ya Dawa za Kulevya aidha, mapambano dhidi ya Malaria.
Mkuu wa Mkoa Gaguti anatoa wito kwa wananchi wote wa Mkoa wa Kagera kujitokeza kwa wingi wakati wa mapokezi ya Mwenge wa Uhuru Murusagamba Wilayani Ngara na maeneo yote ya mkoa Mwenge wa Uhuru utakapopita kutembelea, kukagua, kuzindua na kuweka Mawe ya Msingi ili tuweze kupata ujumbe wa Mwenge wa Uhuru wa mwaka 2019 kuufurahia na kuushangilia Mwenge wa Uhuru kwa pamoja kama kiunganisho cha umoja wetu sisi Watanzania hasa Wanakagera ili tuendelee kuishi kwa amani, utulivu, upendo, umoja na mshikamano.
Mwenge wa Uhuru utapokelewa Murusagamba Wilayani Ngara tarehe 24 Aprili, 2019 na utakimbizwa katika Halmashauri za Wilaya zote za Mkoa wa Kagera ukianzia Ngara, Karagwe, Kyerwa, Missenyi, Bukoba Manispaa, Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, Muleba na utahitimisha mbio zake katika Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo Mei Mosi, 2019. Mimi Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Elisha Gaguti nitaukabidhi Mwenge wa Uhuru kwa Mkuu wa Mkoa wa Geita tarehe 2 Mei, 2019.
Mwenge wa Uhuru karibu Mkoani Kagera ewe mwananchi shiriki katika mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2019, “Maji ni Haki ya Kila Mtu, Tutunze Vyanzo Vyake na Tukumbuke Kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa”.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Postal Address: S.L.P 299 BUKOBA
Telephone: 255 28 2220215/17
Mobile:
Email: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 GWF . All rights reserved.