- Home
- About Us
- Administration
- Districts
- District Councils
- Investment Opportunities
- Services
- Publications
- Media Center
Uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera unatoa rai na angalizo kwa Wakinamama Wajawazito Mkoani humo kuzingatia kanuni na ushauri wa kitaalam wanaopewa na wataalam wa masuala afya katika Hospitali hiyo na kuacha kuchanganya huduma za kitaalam na dawa za kienyeji kwa kunywa dawa hizo na kuchanganya dawa zilizoidhinishwa kisheria ili kujifungua salama na kwa haraka.
Rai hiyo ilitolewa na uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera mara baada ya kupata kesi za mara kwa mara kwa Wakinamama Wajawazito kupasuka vizazi wakati wa kujifungua au watoto kuzaliwa wakiwa wamechoka sana jambo ambalo linasababisha watoto kuwa hatarini kupoteza maisha lakini pia hata mama mwenyewe anakuwa kwenye hatari kubwa ya kupoteza maisha yake.
Sababu kubwa inayosababisha Wakinamama hao Wajawazito kupasuka vizazi au watoto kuzaliwa wamechoka ni baadhi yao wanapopewa rufaa kutoka katika vituo mbalimbali vya kutolea huduma kuja Hospitali ya Rufaa kujifungua wanakuja na dawa za kienyeji ambazo wanazipata mitaani kwa imani kuwa kuwa wakizitumia zitawasaidia kuongeza uchungu na kujifungua haraka na dawa hizo wanazitumia kwa uficho wakiwa Hospitali jambo ambalo ni hatari sana kwao wenyewe na mtoto tumboni.
“Tumegundua tatizo hili mara baada ya kuona sisi watoa huduma tunatimiza wajibu wetu kwa kutoa huduma stahiki na sahihi kwa muda muafaka kwa Wakinamama Wajawazito na wakati mwingine Mama Mjamzito anakuwa anaendelea vizuri chini ya uangalizi wa watoa huduma wetu lakini ghafla hali inabadilika mama anapasuka kizazi au mtoto anazaliwa akiwa amechoka sana au wakati mwingine kusababisha kifo ndipo tuliamua kuanza kufanya utafiti sisi wenyewe ndani ya Hospitali.” Alifafanua Bw. Kiiza Kilwanila Katibu wa Hospitali.
Bw. Kiiza alisema kuwa baada ya kufanya uchunguzi wa kina waligundua kuwa Wakinamama Wajawazito wanakuja na dawa hizo za kienyeji zikiwa za kunywa, kutafuna au kupaka ili mama ajisikie uchungu haraka na ajifungue kwa muda mfupi na wamekuwa wakizificha jikoni wenyewe wanaita “Kijanjabi” na wanakuwa wanazitumia kwa kificho jambo ambalo linasababisha matatizo makubwa hadi kupelekea vifo vya mama mwenyewe, mtoto au wate mama na mtoto.
Bw. Kiiza alisema kuwa tarehe 29 Oktoba, 2018 Uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera uliamua kuendesha msako ndani ya Hospitali ambapo walibainika Wakinamama Wajawazito sita wakiwa na dawa za kienyeji (Mushana, Kalandarugo) na nyinginezo wakitumia kwa uficho pamoja na huduma na wanazopewa na Wataalam wa Afya walioidhinishwa kisheria kutoa huduma za kitabibu katika Hospitali hiyo.
Imani hizo au matumizi ya dawa hizo za kienyeji ambazo hazikuidhinishwa kitaalamu yanarudisha nyuma juhudi za Serikali za kupunguza vifo vya Wakinamama Wajawazito na watoto na kusababisha vifo jambo ambalo linaweza kusababisha Mkoa wa Kagera kuonekana kuwa vifo vya Wakinamama Wajawazito na watoto vipo juu kumbe tatizo linasababishwa na akina mama wenyewe ambapo lawama zinaelekezwa kwa Serikali na Watoa huduma hasa waliopo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera.
Sera ya Afya ya Mwaka 2007 inasisitiza kupunguza vifo vya Wakinamama Wajawazito na Watoto lazima juhudi hizi za Serikali ziungwe mkono hasa Wakinamama Wajawazito kwa kuhakikisha Wataalam wa Afya wanatekeleza majukumu na wajibu wao wa kiweledi katika kutoa huduma na ushauri kwa wananchi.
Wito wa Uongozi wa Mkoa wa Kagera pamoja na Hospitali ya Rufaa ni wananchi kuunga mkono juhudi za Serikali katika kupunguza vifo vya Wakinamama Wajawazito na Watoto kwa kutoa elimu ya kutosha kuwa mama anapofikishwa Hospitali mapema anakuwa katika mikono salaama ya Wataalam wa Afya. Aaidha, wananchi waache imani potofu kuwa dawa za kienyeji zinasaidia katika kurahisisha mama mjamzito kujifungua, imani hizo zipuuzwe kwani zinasababisha madhara makubwa hadi kupelekea vifo vya mama na watoto.
Kama Wakinamama Wajawazito hawataacha tabia hiyo ya kuchanganya dawa za kienyeji na huduma za kitaalam uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera utachukua hatua kali kwa mama yeyote atakayebainika au kukamatwa ikiwa ni kutozwa faini au pia kuchukuliwa hatua za kisheria. Wito ni kuacha tabia hizi zisizo za busara, akina baba ni jukumu lenu pia kuwaelimisha wake zenu kuzingatia ushauri bora wa kitaalam ili kuachana na imani potofu ili mama na mtoto watoke salama katika chumba cha kujifungulia na kuendelea kujenga familia bora.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Postal Address: S.L.P 299 BUKOBA
Telephone: 255 28 2220215/17
Mobile:
Email: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 GWF . All rights reserved.