- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Balozi wa Tanzania Nchini Rwanda Mheshimiwa Ernest Mangu afanya ziara ya siku mbili Mkoani Kagera na kukutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa Mkoa kuhusu kuchangamkia fursa za kiuchumi nchini Rwanda kati ya wananchi wa Mkoa wa Kagera na nchi ya Rwanda.
Balozi Ernest Mangu akiwasili Mkoani Kagera kupitia mpaka wa Tanzania na Rwanda Rusumo Julai 25, 2018 na kupokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Salum M. Kijuu aliweza kufanya mazungumzo na watumishi wa Kituo cha kutoa huduma kwa Pamoja cha Rusumo (OSBP) upande wa Tanzania na kuwaelekeza namna bora ya kuboresha huduma katika kituo hicho ili wananchi wa nchi mbili wanufaike zaidi.
Katika mpaka wa Rusumo Kituo cha kutoa huduma kwa pamoja (OSBP) kinahudumia magari 350 na watu 450 kwa siku ambapo Balozi Mangu alitaka kujua watu wanaohudumiwa kwa siku wengi wanatoka Tanzania kwenda Rwanda au kutoka Rwanda kuja Tanzania ili kama wengi wanatoka Rwanda kuja Tanzania ajue ni kwanini Watanzania hasa wa Mkoa wa Kagera hawachangamkii fursa za kibiashara nchini Rwanda.
Pia Balozi Mangu alitoa changamoto kwa uongozi wa Mkoa wa Kagera kuwa Rwanda kuna fursa nyingi za kiuchumi hasa biashara ambapo Wanyarwanda wengi wanapendelea kwenda Nchini Uganda Jijini Kampala kununua bidhaa mbalimbali kutokana na bidhaa hizo nyingi kupatikana Jijini Dar es Salaam ambako ni mbali sana kutoka Kigali.
Ili kutatua changamoto hiyo na kuwavutia Wanyarwanda Wafanyabiashara wa Tanzania hasa wa Mkoa wa Kagera wanatakiwa kuanzisha maduka makubwa ya bidhaa mbaimbali za jumla katika mpaka wa Rusumo upande wa Tanzania ili kuwavutia Wafanyabiashara kutoka Rwanda ambapo Rusumo ni karibu sana kuliko Jijini Kampala nchini Uganda. “Rusumo inaweza kuwa Dar es Salaam ya Kigali na Wanyarwanda wakaishia hapa.” Alisisitiza Balozi Mangu.
“Wanyarwanda wanapenda sana mchele kutoka Kahama, wanapenda sana dagaa na Samaki kutoka Ziwa Viktoria na si Kigali tu bali na nchi ya Kongo bidhaa hizo ni adimu sana jambo linalopelekea kuwa na soko kubwa lakini sijaona zikiuzwa kwa biashara rasmi bali kimagendomagendo tu, sasa hiyo ni fursa kwa Wafanyabiashara wa Kagera kufungua maghara makubwa hapa Rusumo ili biashara hiyo ifanyike hapa na kodi ilipwe na kunufaisha nchi zote mbili.” Alifafanua Balozi Mangu.
Katika hatua nyingine Balozi Mangu alikutana na Wafanyabiashara mjini Ngara na kusikiliza changamoto zao zinazowakwaza kufanya biashara na nchi ya Rwanda na kuhaidi kuzifanyia kazi ili pande zote mbili wananchi wake wanufaike kiuchumi kutokana na fursa ya kuwepo mpaka kati ya nchi hizo.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum M. Kijuu alimuhaidi Balozi Mangu kuhakikisha anayafanyia kazi maelekezo yake yote ili kuhakikisha wananchi wa Mkoa wa Kagera hasa Wafanyabiashara wananufaike kiuchumi na fursa ya kuwepo mpaka wa Rusumo ambao unaziunganisha nchi za Rwanda na Tanzania.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa