- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum M. Kijuu aliagiza Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Ngara kuchukua hatua zinazostahili kwa watumishi na wadau wote wa Halmashauri waliosababisha kwa namna yoyote ile Halmashauri kuwa na hoja za miaka ya nyuma ambazo majibu yake hayakumridhisha Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
Mkuu wa Mkoa Kijuu alitoa agizo hilo katika kikao maalum cha Baraza la Madiwani cha kujadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizoishia tarehe 30 Juni, 2017 ambapo kwa mwaka 2016/ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ngara ilipata hati safi.
Pamoja na Halmashauri hiyo kupata Hati Safi mwaka 2016/2017 Mkaguzi alionesha udhaifu wa kutozingatia Sheria na kanuni za Usimamizi wa Fedha, Manunuzi, Usimamizi wa watumishi, Usimamizi wa mali za Halmashauri, Usimamizi wa Mikataba na kutozingatia maagizo mbalimbali ya Serikali.
Katika ukaguzi wake Mkaguzi alionesha kuwa Menejimenti ya Halmashauri haitekelzi kikamilifu baadhi ya hoja za miaka ya nyuma na hivyo kuendelea kubakia bila kufungwa. Halmashauri ilikuwa na hoja za nyuma 108 ambapo kati yake 30 zilizotekelezwa kikamilifu na kufungwa, 38 ziko katika hatua mbalimbali za utekelezaji, hoja 9 hazijatekelezwa kabisa na hoja 31 ziliondolewa na Mkaguzi kwa sababu mbalimbali.
Aidha, katika utekelezaji wa maagizo ya Kamati ya Bunge yaliyotolewa tarehe 30/08/2017 Mkaguzi ameonesha kuwa agizo moja tu liko katika hatua za utekelezaji na maagizo mawili hayajatekelezwa. Miongoni mwa hoja za miaka ya nyuma zilizobakia bila kutekelezwa kikamilifu na kufungwa ni kama ifutavyo;
Moja, Mawakala kutowasilisha mapato yenye thamani ya shilingi 38,550,000 kulingana na mikataba yao (2012/2013) na shilingi 3,000,000 (2013/2014). Pili, Kutokamilisha utaratibu wa kufuta vitabu vya wazi vya mapato (open receipt book) 4 ambavyo havikuwasilishwa wakati wa ukaguzi (2012/2013). Tatu, Kutokamilisha utaratibu wa kufuta hasara ya mapato ya ndani ya shilingi 4,308,030 ambazo hazikuwekwa benki na mtumishi ambaye sasa ni marehemu (2012/2013).
Nne, Kutothibitika kurejeshwa Hazina mishahara isiyolipwa ya jumla ya shilingi 27,613,192 (2012/2013), shilingi 8,309,656 (2013/2014), shilingi 24,080,903 (2014/2015) na shilingi 47,011,670 (2015/2016). Tano, Kutochangia kikamilifu katika Mfuko wa Wanawake na Vijana na hivyo kubakia na deni la shilingi 42,501,143 kwa mwaka 2013/2014 na shilingi 53,757,770 mwaka 2014/2015.
Sita, Kutokamilika kwa maabara za sayansi katika shule za sekondari Mabawe na Ndomba zenye thamani ya shilingi 35,477,173 (2013/2014). Saba, Kutorejesha shilingi 2,260,000 (2014/2015) na shilingi 228,415,951 (2015/2016) zilizokopwa kutoka katika akaunti ya Amana.
Nane, Kutotumika kwa nyumba ya watumishi (2 in 1) katika zahanati ya Kabalenzi iliyogharimu shilingi 53,895,426 (2014/2015).
Tisa, Kutumika kwa kazi nyingine shilingi 75,000,000 zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi wa eneo la kuegesha malori BENACO (2015/2016). Kumi, Kutothibitika matumizi ya mafuta ya thamani ya shilingi 1,204,060/= katika vitabu vya magari (logbooks) (2015/2016). Na mwisho, Kutopatikana kwa hati za malipo zenye thamani ya shilingi 76,163,888 (2015/2016).
Pamoja na mapungufu mengine katika kuhitimisha kikao hicho Mkuu wa Mkoa Kijuu alitoa maagizo yafuatayo; Halmashauri zote za mkoa wa Kagera zihakikishe kuwa hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuwa ajenda ya kudumu katika vikao mbalimbali vya Halmashauri za Wilaya.
Halmashauri za Wilaya zihakikishe zinatumia Mfumo wa Kielektroniki katika kukusanya mapato ya Halmashauri na kuhakikisha mifumo hiyo inatumika na kusimamiwa kiamilifu pia Halmashauri ziepuke kuwatumia Mawakal katika kukusanya mapato ya Serikali na kuwatumia Watumishi na fedha zinapokusanywa zisitumike bila kuwasilishwa benki.
Halmashauri za Wilaya ziwaalike Watendaji mbalimbali wa Serikali mfano TANESCO, TARURA, na wengine katika vikao mbalimbali vya Halimashauri kama Mabaraza ya Madiwani ili kupata taarifa za utekelezaji wa miradi mbalimbali katika Halmashauri husika.
Halmashauri zote za Mkoa wa Kagera zihakikishe zinatekeleza agizo la Serikali la kupeleka asilimia 10 ya mapato yake kwa vikundi vya Akinamama, Vijana na Walemavu na kuhakikisha vikundi hivyo vinasimamiwa na vinakuza mitaji yake na kuondokana na umasikini.
Mwisho Mhe. Kijuu alitoa rai kwa wananchi wote wa mkoa wa Kagera hasa Halmashauri za Wilaya kuchangamkia fursa mpya ya utalii ambayo imeapatika sasa baada ya Serikali kuyatangaza Mapori ya Biharamulo, Burigi na Kimisi kuwa hifadhi za Taifa. Fursa hizo ni pamoja kujenga Mahoteli ya Kitalii, Kujifunza Uongozaji wa Watalii, Vituo mbalimbali vya Utamaduni vya Kitalii pamoja na mengineyo mengi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa