- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Kongamano la Wiki ya Uwekezaji Kagera lafungwa rasmi na Naibu Waziri wa Wizara ya Viwanda na Biashara Mhandisi Stella Manyanya mara baada ya wanazuoni, wataalamu wa mambo ya uchumi, wafanyabiasha na wajasiliamali mbalimbali kukaa kwa siku mbili mfurulizo kuchambua kwa kina fursa za uwekezeji mkoani Kagera na kutoka na maazimio makuu sita ya kuufanya mkoa wa Kagera kukua kiuchumi.
Akifunga rasmi kongamano hilo Naibu Waziri Mhandisi Manyanya aliwakumbusha wanankagera wote sasa kuwa tayari kwa kila hali kuwapokea wawekezaji kwasababu mkakati wa kutangaza fursa uliondaliwa na uongozi wa Mkoa ukiongozwa na mkuu wa Mkoa katika Wiki ya Uwekezaji Kagera umefanikiwa kwa kiwango kikubwa sana.
“Kama mkakati huu utatekelezwa vizuri na kwa umakini mkubwa utakuza zaidi pato la mwananchi wa Kagera pato la mkoa na taifa kwa ujumla, wakati ni huu wananchi sasa amkeni msiogope fursa zimebainishwa hasa katika kitabu cha mwongozo wa uwekezaji Kagera alichozindua juzi Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa.” Alisisitiza Naibu Waziri Mhandisi Manyanya.
Naibu Waziri Mhandisi Manyanya aliendelea kusisitiza kuwa Kagera imefanikiwa kwani pamoja na fursa zilizopo za kuzungukwa na nchi jirani lakini pia gharama za kwenda huko ni ndogo sana ukilinganisha mfano kutoka Bukoba kwenda mkoani Ruvuma ni zaidi ya kilomita 2000 lakini ni nafuu kwenda nchi jirani ukitokea hapa Bukoba ambayo ni fursa ya gharama ndogo ya kusafiri au kusafirisha bidha.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti Mwenyekiti wa Wiki ya Uwekezaji Kagera akitoa taarifa fupi kwa Mgeni rasmi Naibu Waziri Mhandisi Stella Manyanya kabla hajafunga rasmi Kongamano la Uwekezaji Kagera alisema kuwa dhumuni kubwa la Wiki hiyo lilikuwa ni chagizo la kuona fursa mbalimbali zilizopo mkoani Kagera kupitia sekta zote muhimu.
Mkuu wa Mkoa Mhe. Gaguti alisema kuwa Wiki ya Uwekezaji Kagera imefnikiwa kwa kiwango kikubwa na iliandaliwa kwa sura kuu tatu kwanza maonesho ya bidhaa mbalimbali zinazozalishwa na wadau mbalimbali katika mkoa wa Kagera. Pili, kongamano ambalo lililowakusanya wanazuoni wabobezi kuchambua na kuchanganua fursa za uwekezaji na mwisho ni wadau wa uwekezaji kutembelea vivutio mbalimbali vya uwekezaji mkoani Kagera.
Mkuu wa Mkoa Mhe. Gaguti aliwashukuru wananchi wote wa Kagera na wadau mbalimbali walioshiriki katika kufanikisha Wiki ya Uwekezaji bila kuvisahau vyombo vya habari mbalimbali vya ndani na nje ya mkoa lakini pia waandishi wa habari kwa kuitangaza Wiki ya Uwekezaji Kagera na kuwahabarisha wananchi juu ya nini kilikuwa kinafanyika katika wiki hiyo.
Mara baada ya Kongamano la Wiki ya Uwekezaji Kagera wadau wote waliafikia maazimio makuu sita ili kufanya ufuatiliaji kila baada ya miezi mitatu na kuhakikisha adhima ya uwekezaji Kagera inafikiwa; Kwanza; Taratibu zifanyike ili mkoa wa Kagera upewe hadhi ya kuwa “Special Economic Zone” (SEZ) kwasababu Kagera ni lango la kibihara kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati.
Pili, Mkoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa zianzishe dawati la kuratibu utekelezaji wa mwongozo wa uwekezaji mkoa wa Kagera mwaka 2019. Tatu, Uwekezaji ufanyike katika mifumo rasmi ya ndani na mipakani (Rusumo, Kabanga, Mtukura na Murongo) ili kurahisisha biashara ndani ya mkoa na nchi jirani.
Nne, Mkoa kwa kushirikiana na umoja wa wafanyabiashara mkoani utakuwa na vikao vya mara kwa mara kuweka mikakati ya kuvutia mitaji na masoko toka ndani na nje ya nchi. Tano, Uongozi wa Mkoa uendelee na juhudi za kuimarisha stadi za fedha na uwekezaji ikiwa ni pamoja na kuwaelimisha wafanyabiashara na wananchi juu ya umuhimu wa kushirikiana kupata mitaji na usimamizi wa fedha.
Mwisho wafanyabiashara wa Mkoani Kagera kufanya ziara katika nchi za Uganda, Rwanda, Burundi, Congo DRC, na Kenya ili kuona fursa za uwekezaji au biashara zilizopo katika nchi hizo ili kuona namna wanavyoweza kunufaika na fursa hizo kwa kupeleka bidhaa mbalimbali huko.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa