- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Afanya Ziara Mkoani Kagera Kuona Utendaji wa Mahakama Kanda ya Bukoba
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Ferdinand L. K. Wambali afanya ziara Mkoani Kagera kukagua mwenendo wa mashauri katika Mahakama kuona kama mashauri hayo yanaendeshwa kulingana malengo yaliyowekwa ambapo Mhe. Wambali atatembele Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Bukoba, Mahakama ya Hakimu Mkazi, Mahakama za Wilaya za Karagwe na Muleba pamoja na Mahakama za Mwanzo mbili katika Wilaya hizo.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Meja Jenerali Mstaafu Salum M. Kijuu akiongea na Jaji Kiongozi Mhe. Wambali alipowasili ofisini kwake kumsalimia leo January 6, 2018 alimweleza Mhe. Jaji Kiongozi kuwa katika Mkoa wa Kagera kuna changamoto katika Wilaya mbili za Kyerwa na Missenyi kutokuwa na Mahakama za Wilaya na kusababisha kesi nyingi kutoka katika Wilaya hizo kupelekwa Bukoba na Karagwe.
Mheshimiwa Wambali katika kueleza lengo kuu la ziara yake Mkoani Kagera alisema kuwa amekuja kuona kama Nguzo kuu tatu zilizowekwa na Mahakama katika utoaji wa haki zinasimamiwa kikamilifu katika Mkoa wa Kagera ambapo Nguzo ya kwanza ni Utawala Bora, Uajibikaji na Usimamizi wa Raslimali Watu.
Katika Nguzo hiyo ya kwanza Mhe. Wambali alisema kuwa Mahakama zinatakiwa kusikiliza kesi za wananchi na kutoa maamuzi kwa muda muafaka mfano Kesi katika Mahakama ya mwanzo haitakiwi kuzidi miezi sita bila kutolewa maamuzi, Mahakama ya Wilaya mwaka mmoja, na Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani miaka miwili.
Aidha, ukumu katika Mahakama ya Mwanzo inatakiwa kutolewa ndani ya siku 90, nakala ya hukumu inatakiwa kutolewa ndani ya siku 21 na mwenendo wa kesi unatakiwa kutolewa ndani ya siku 30.
Nguzo ya pili, ni kuboresha miundombinu ya Mahakama ili watumishi na wananchi waweze kutoa na kupata huduma za Mahakama katika mazingira yanayoridhisha. Mhe. Wambali pia alimweleza Mkuu wa Mkoa kuwa Mahakama zinendelea kujengwa nchi nzima lakini kwa kutoa vipaumbele hasa katika maeneo yenye tatizo kubwa.
Nguzo ya tatu aliyoitaja Mhe. Wambali ni Mahakama kuimarisha imani ya wananchi juu ya Mahakama hasa watumishi katika Mahakama kuzingatia maadili na kuepukana na vitendo vya rushwa. Mhe. Wambali alisema hilo llinafanyika kupitia matangazo mbalimbali kama vipeperushi, kuwauliza wananchi juu ya huduma za Mahakama wakati wa maadhimisho ya Siku ya Sheria na Kuunda Kamati za Maadili ya Mahakama ambapo Mwenyekiti wake ni Mkuu wa Mkoa katika Mkoa husika.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Ferdinand L. K. Wambali amefika Mkoani Kagera tarehe 6 Januari, 2018 na anatarajia kuhitimisha ziara yake mkoani hapa tarehe 9 Januari, 2018 siku ya Jumanne.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa