- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Mkoa wa Kagera Waadhimisha Kilele Cha Wiki ya Sheria Kwa Wadau Kuchambua Ufanisi wa Matumizi ya Tehama Katika Mahakama
Mkoa wa Kagera waadhimisha kilele cha wiki ya Sheria kwa wadau mbalimbali kuchambua, kutoa ufafanuzi na uelewa kwa wananchi juu ya kaulimbiu ya mwaka huu isemayo “Matumizi ya TEHAMA Katika Utoaji Haki kwa Wakati na Kuzingatia Maadili”
Akitoa salamu za Serikali Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum M. Kijuu wakati wa kilele cha wiki ya Sheria katika viwanja vya Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba alisema kuwa ni Muhimu sana Mahakama kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kuwafanya wananchi wasipoteze muda mwingi Mahakamani badala yake watumie muda huo kufanya shughuliza kiuchumi.
Mhe. Kijuu aliwaomba Viongozi wa dini kuendelea kuhubiri amani katika nyumba za ibada ili wananchi waendelee kuwa na upendo na kudumisha amani na kuacha vurugu za kupelekana Mahakamani ili zibakie kesi au mashauri ya msingi tu na yashughulikiwe na kumalizika kwa wakati.
Pia Mhe. Kijuu alitoa wito kwa wananchi kuacha kujichukulia sheria mikononi pia kuheshimu maamuzi ya Mahakama na waache tabia za kukata rufaa za kesi zilizoamuliwa kihalali jambo ambalo linazifanya Mahakama kuwa na msongamano wa kesi na kuchelewesha maamuzi kwa kesi ambazo tayari zilishaamuliwa.
Aidha, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba Mhe. Salvatory Bongole alisema kuwa Mpango Mkakati mkuu uliowekwa na Mahakama wa mwaka 2016 hadi 2020 umejikita katika shabaha kuu sita za TEHAMA Katika Mahakama. Shabaha ya kwanza ni kufunga au ujenzi wa miundombinu ya TEHAMA katika Majengo ya Mahakama.
Pili ni kuwa na Mahakama ya Kielektroniki (E-Judiciary), Tatu kuwa na mtoa huduma mmoja wa internet ambaye ataziunganisha Mahakama zote nchini, Nne ni kununua vifaa vya Video Conferencing pamoja na mobile recording system kwa Mahakama zilizochaguliwa, Tano kuanzisha mfumo wa kuratibu nyaraka za kielektroniki, Sita kuanzisha mfumo utakaoratibu raslilimali za Mahakama. Jaji Bongole alisema kuwa shabaha zote sita zipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji kwa sasa.
Naye Mwanansheria Mkuu wa Serikali Mkoa wa Kagera Hashim Ngole alisema kuanzishwa kwa TEHAMA katika Mahakama kutaleta faida nyingi ikiwa ni pamoja na kupunguza muda wa kushughulikia mashauri mahakamani na kupunguza matumizi makubwa ya karatasi (Paper work), Kurahisisha utumaji wa taarifa kwa wakati na kwa kipindi maalum.
Mhe. Ngole pia alisema kuwa TEHAMA katika Mahakama itarahisisha utaratibu wa kurekodi mienendo ya mashauri Mahakamani kwa kumbukumbu sahihi za baadae kuliko ilivyo sasa. Pia Kuwafanya mashahidi wa kesi kutoa ushahidi mahala papote walipo kwa njia ya Video Conference kuliko ilivyo sasa kuwa lazima shahidi afike mahakamani.
Faida nyingine zilizotajwa za kuanzisha TEHAMA katika Mahakama ni Mawakili kuwawakilisha wateja wao mahakamani bila wao kuwepo, kupunguza mianya ya rushwa Mahakamani. Hukumu, machapisho na sheria mbalimbali kupatikana kwa urahisi katika mitandao ili kuwasaidia Mawakili katika kuendesha mashauri Mahakani.
Katika Hatua nyingine Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (Tanganyika Law Society) Mkoa wa Kagera Wakili Aron Kabunga alishauri kuwa ili kuifanya Mahakama kuwa ya Kielektroniki lazima baadhi ya vifungu vya sheria virekebishwe ili kuruhusu matumizi ya TEHAMA kuwa na ufanisi katika Mahakama.
Vilevile Wakili Kabunga alisisitiza kuwa na tahadhari kubwa kuhusu madhara ya TEHAMA kama udukuzi wa nyaraka kwa njia za mitandao, Vifaa kama kompyuta kuingiliwa na wadudu (Virus) au wataalamu na kuharibu mfumo mzima na kupelekea nyaraka muhimu kama hukumu au ushahidi kupotea au kubadilishwa kwa matakwa ya upande mmoja.
Maadhimisho ya Kilele cha Wiki ya Sheria Mkoani Kagera yaliadhimishwa katika Viwanja vya Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba na Mgeni Rasmi alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa