- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Wanaushirika Kagera Wapewa Changamoto ya Kufufua Ushirika Ili Kukuza Uchumi wa Mkoa Kama Miaka ya Nyuma
Wadau wa Vyama vya Ushirika Mkoani Kagera wakumbushwa kuvifufua Vyama vya Ushirika ili kukuza uchumi pia kutumia fursa ya ushirika kuanzisha viwanda ili kuendana na Sera ya Serikali ya Awamu ya Tano ya uchumi wa viwanda
Rai hiyo ilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum M. Kijuu aliyewakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Deodatus Kinawilo katika mkutano wa Jukwaa la Wadau wa Ushirika lililoandaliwa Mkoani Kagera na kuwakutanisha wadau wa Ushiriki ili kujadili fursa za Ushirika na kuona jinsi ya kutatua changamoto zinazovikumba Vyama vya Ushirika ambapo Jukwaa hilo lilifanyika katika Hoteli ya Bukoba Coop Julai 18, 2017.
Katika hotuba yake ya ufunguzi wa Jukwaa hilo la Wadau wa Ushirika Mkoani kagera Mkuu wa Mkoa Kijuu alikemea tabia ya baadhi ya viongozi wa Vyama vya Ushikia kuacha mara moja tabia ya ubadhirifu kwenye manunuzi mazao hasa kahawa ili Ushirika uweze kukua na kuinua uchumi wa wananchi pamoja na Mkoa kwa ujumla kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Pia aliwaagiza Maafisa Ushirika wote wa Mkoa wa Kagera kuhakikisha wanavisimamia Vyama vyote vya Ushirika hasa katika kutoa taarifa za mapato na matumizi na kudhibiti ubadhilifu katika vyama hivyo kwa kuzingatia sheria namba 6 ya mwaka 2013 pamoja na vi pengere vyake.
Aidha, Mkuu wa Mkoa Kijuu aliwaasa wanachama wote wa Vyama vya Ushirika Mkoani Kagera kuhakikisha wanawachagua viongozi wenye maadili na maono ya kuendeleza Ushirika na sio viongozi walafi, ikiwa mwaka huu 2017 ni mwaka wa uchaguzi wa viongozi kwa Vyama vya Ushirika mkoani Kagera.
Mkuu wa Mkoa pia alivitaka Vyama vikuu viwili vya Ushirika Mkoani Kagera ambavyo ni Kager Co-operative Union 1990 Limited (KCU 1990 Ltd) na Karagwe Development Co-operative Union Ltd (KDCU Ltd) kuangalia upya vitega uchumi vyake kama mashamba, magari, maghara na uwekezji mwingine ambao hauna hati za umiliki kwani vimekuwa vikisababisha migogoro kwa wadau wegine ambapo vinatakiwa kuingiza kipato katika vyama hivyo ila badala yake havizalishi chochote.
Katika hatua nyingine Mrajisi wa Vyama vya Ushirika Tanzania bara Bw. Tito B. Haule aliwaasa Wanaushirika wa Mkoa wa Kagera kuvisisimamia Vyama vyao vya Ushirika kwani wao ndio waamuzi wakuu na siyo Serikali bali Serikali ni msimamizi na mlezi wa Vyama hivyo.
Mkoa wa Kagera una jumla ya vyama vya ushirika 665, kati ya hivyo 393 vipo hai na 272 vimesinzia. Vyama vya Ushirika vya mazao (AMCOS) ni 230 na vina jumla ya wanachama 67,506 wenye jumla ya hisa 289,156. Pia Vyama vya Ushirika wa Akiba na mikopo (SACCOS) vina jumla ya wanachama 57,905 na vina Hisa za shilingi 1,517,369. Akiba za shilingi10,586,894 na Amana za shilingi 1,892,086.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa