- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Mikoa ya Kagera na Kigoma Yapata Mafunzo ya Mifumo Iliyoboreshwa Katika Usimamizi wa Fedha na Uhitaji wa Watumishi Katika Vituo
Serikali kupitia Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) kwa kushirikiana na Washirika wa Maendeleo ambao ni Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma (PS3) waendesha mafunzo ya siku mbili mkoani Kagera kuhusu mfumo ya usimamizi wa fedha, mfumo wa kubaini mahitaji ya Watumishi ulioboreshwa kwa mikoa ya Kagera na Kigoma.
Mafunzo hayo yanahusu Mfumo wa usimamizi wa fedha za umma wa EPICOR toleo la 10.2 ambao umeboreshwa ili kuwezesha ubadilishanaji wa taarifa na Mfumo wa Mipango na Bajeti wa PlanRep na ule wa Uhasibu na kutoa taarifa za fedha za vituo vya kutolea huduma FFARS.
Aidha, mafunzo hayo yanalenga pia kupata mrejesho wa matokeo ya zoezi la kubaini mahitaji ya watumishi kwa kutumia Mifumo ya Workload Indicators of Staffing Need (WISN), na Priority and Optimization Analysis (POA) mifumo iliyorahisishwa katika matumizi na kuzingatia uzito wa kazi katika vituo vya kutolea huduma.
Akifungua mafunzo hayo Juni 4, 2018 katika Hoteli ya Bukoba ELCT Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera CP Diwani Athuman aliwakumbusha washiriki wa mafunzo kuwa usimamizi wa fedha za Umma lazima unaendane na maboresho yanayoendelea ndani ya Serikali ambapo Halmashauri zote pamoja na vituo vyake vya kutolea huduma zinatumia mifumo mingi zaidi ya Mfumo wa Epicor.
CP Athumani aliitaja mifumo hiyo kuwa ni Mfumo wa ukusanyaji wa Mapato (LGRCIS), Mfumo wa Vituo vya Kutolea Huduma za Afya, ambao unapokea mapato ya papo kwa papo (Cost Sharing) na kutunza taarifa za wagonjwa (GoT-HoMIS), Mfumo wa taarifa za kihasibu kwenye Vituo vya Kutolea huduma (FFARS) pamoja na mfumo ulioboreshwa wa kuandaa Mipango na Bajeti (PlanRep).
“Uwepo wa mifumo hiyo unapelekea uhitaji wa kuunganishwa mifumo hiyo ili iwe rahisi katika upatikanaji wa taarifa kwa ngazi zote na kwa wadau wengine wa maendeleo. Aidha, mafunzo hayo yatapunguza changamoto za utoaji taarifa hasa kutoka katika vituo vya kutolea huduma pamoja na kuunganisha taarifa hizo kwenye hesabu za Halmashauri, na kutoa taarifa za utekelezaji wa mipango na bajeti kwa kuzingatia matumizi ya fedha yaliyofanyika.” Alisistiza CP Athuman.
Katika hutua nyingine Serikali inatarajia kuajiri katika Sekta ya Afya Watumishi wapya 7,680 (6,180 wa Ofisi ya Rais TAMISEMI na 1,500 wa Wizara ya Afya) na mafunzo hayo ya siku mbili yamelenga kuziwezesha Halmashauri na Mikoa ili ziweze kutumia Mfumo wa WISN na POA iliyorahisishwa kusambaza watumishi wapya na katika kuomba watumishi wengine wapya.
Mafunzo hayo yaliwajumuisha watumiaji wa Mifumo ambao ni Waweka Hazina, Maafisa Usimamizi wa Fedha, Wahasibu, Maafisa TEHAMA, Afisa manunuzi na Wakaguzi wa Ndani. Mafunzo hayo yaliendeshwa na wakufunzi kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) wakishirikiana na Wataalam kutoka Mradi wa PS3.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa