- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
KAGERA YAADHIMISHA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI KWA KUWAINUA WAJANE NA KUWAHIMIZA WAJASILIAMALI KUFIKIA TANZANIA YA VIWANDA
Mkoa wa Kagera waadhimisha Siku ya Wanawake Duniani kwa kuwatia moyo na kuwahimiza wanawake wanaojishughulisha katika shughuli za ujasiliamali kuongeza juhudi kufikia lengo la Serikali la Tanzania kuwa nchi ya viwanda. Aidha, wanawake wenyewe wamehamasishana kuwasaidia wenzao ambao ni wajane na wenye matatizo hasa ya kukosa makazi kutokana na sababu mbalimbali.
Maadhimisho hayo yaliadhimishwa kimkoa Wilayani Karagwe katika Mji mdogo wa Kayanga na kuhudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum M. Kijuu ambaye alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo ambayo huadhimishwa Machi, 8 kila mwaka.
Katika maadhimisho hayo Mkuu wa Mkoa Kijuu alimtembelea Mama Cineth Patrick katika eneo la Omulushaka ambaye ni Fundi Seremala na anamiliki kiwanda cha kutengeneza samani za kisasa zikiwemo sofa. Mama Cineth ameajili vijana wakiwemo wasichana ambao ni mafundi aliowafundisha kazi yeye mwenyewe na anashirikiana nao kutengeneza samani katika kiwanda chake.
Mama Cineth anasema mara baada ya kuhitimu ufundi wa uselemala katika Chuo cha Ufundi Karagwemwaka 2014 aliamua kujiajili mwenyewe ambapo tayari amepata faida ya kazi yake kwani kwasasa anasomesha watoto wake watatu, amejenga nyumba ya kuishi na familia yake na ameweza kujenga vyumba vinne vya kupangisha ili kuongeza kipato.
Mkuu wa Mkoa baada ya kutembelea na kukagua kiwanda pamoja na samani anazozitengeneza alimshukuru kwa kujituma kuliko hata wananume. Pia alimweleza kuwa viwanda vinavyohimizwa na Serikali kila siku vinaanzia katika viwanda vidogo vidogo na baadae vinakuwa vikubwa. Aidha alimsistiza kuongeza juhudi ili kiwanda chake siku moja kiwe kiwanda kikubwa zaidi ya kilivyo sasa na kutoa ajira zaidi.
Mara baada ya kumtembelea mama Cineth alimtembelea Mama Mjane ambaye nyumba yake ilingushwa na upepo mkali uliombatana na mvua tarehe 21/02/2017 na kumfanya mama huyo kukosa makazi na kuishi kwenye hema. Wanawake Wilayani Karagwe wakishirikiana na Mfuko wa Maafa wa Wilaya waliamua kumchangia mama huyo fedha na kuanza kumjengea upya nyumba yake.
Wakati alipofika kwa mama huyo mjane Juliana Novath Kayanga katika kitongoji cha Nsheshe Mkuu wa Mkoa alikuta ujenzi wa msingi unaendelea ambapo alimchangia bati ishirini ili kuunga mkono juhudi za akina mama kwa mama Juliana apate makazi imara ambapo nyumba yake ili ikamilike itagharimu shilingi 8,700,000/=
Pamoja na michezo na ushuhuda wa akina mama wajasiliamali katika maadhimisho hayo pia wananchi mbalimbali walihamasishwa na kuchangia damu kwa ajili ya wahitaji ambao wapo katika Hospitali mbalimbali na wana uhitaji wa damu ili kunusuru maisha yao.
Katika hatua nyingine akiwahutubia wananchi waliohudhuria katika maadhimisho hayo Mhe. Kijuu aliwaasa wanawake kuchapa kazi kwa bidii kwani wao ni msingi wa mabadiliko ya uchumi kama kaulimbiu isemavyo. Pia aliagiza kila Wilaya kuhakikisha inapambana na wale wote wanaojihusha na madawa ya kulevya kuwakamata na kuwachukuila hatua kali za kisheria.
Kaulimbiu ya mwaka huu inasema “Tanzania ya Viwanda Wanawake ni Msingi wa Mabadiliko ya Uchumi.” Maadhimisho ya Siku ya Wanawake yalianza kuadhimishwa tangu mwaka 1911 huko nchini Marekani, wanawake walipoandamana kudai haki zao na tangu haposiku hiyo huadhimishwa kote duniana tarehe 8 Machi kila mwaka ili kupima ufanisi wa matamko mbalimbali ya wanawake duniani.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa