- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa akihitimisha ziara yake ya siku nne Mkoani Kagera iliyoanza Oktoba 6, 2018 na kuhitimishwa Oktoba 9, 2018 atoa onyo kali kwa Maafisa Elimu pamoja na Maafisa mbalimbali wa Serikali nchini wanaohusika na usimamizi wa mitihani ya Kitaifa kutojihusisha na vitendo vya kuiba mitihani kwa ajili ya kuwatafutia majibu wanafunzi ili wafaulu.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema kuwa Serikali haitasita kuwachukulia hatua kali ikiwa ni pamoja na kuwasimamisha kazi Maafisa wote watakaojihusisha na njama za kuiba mitihani ili kuwafaulisha wanafunzi badala ya kuwaandaa kwa kuwafundisha kwa bidii ili wafanye mtihani wenyewe bila kupewa majibu.
“Vitendo vya kuiba Mitihani na kuwapa wanafunzi ili wafaulu, kwanza ni kuwadumaza akili wanafunzi ili wasijishughulishe kutafuta majibu wenyewe, pili mnawaumiza wanafunzi wenyewe na wazazi wao kwa kitendo cha kurudia mitihani, Serikali haitavumilia vitendo hivyo itachukua hatua kwa yeyeyote atakayehusika, kamatulivyochukua hatua katika Wilaya za Chemba na Kondoa Mkoani Dodoma.” Alifafanua Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitoa onyo hilo akiwa katika Shule ya Msingi Nyakato Wilaya ya Bukoba mara baada ya kupokea mradi wa vyumba sita, ofisi mbili na matundu ya vyoo 16 kutoka kwa mwakilishi wa Balozi wa Japani nchini Tanzania Bw. Katsutoshi Takeda katika Shule za Msingi Nyakato na Kashozi ambapo ujenzi huo uligharamiwa na nchi ya Japani kupitia Balozi wake nchini baada ya shule hizo kuharibiwa vibaya na Tetemeko la Ardhi lililotokea Septemba 10, 2016.
Baada ya Tetemeko la Ardhi kutokea mwaka 2016 nchi ya Japan kupitia Balozi wake nchini Tanzania ilitoa kiasi cha shilingi Milioni 228 kwa Halamshauri ya Wilaya Bukoba ili kurekebisha miundombinu iliyotajwa hapo juu katika Shule za Msingi Nyakato na Kashozi ili Wanafunzi warejee katika shule zao na kuendelea na masomo pamoja na Walimu kuendelea kutekeleza majukumu yao ya ufundishaji.
Mwakilishi wa Balozi wa Japani nchini Bw. Katsutoshi Takeda baada ya kukabidhi mradi huo kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema kuwa baada ya nchi yake kutoa kiasi cha fedha Milioni 228 anafurahi kuona fedha hiyo imefanya kazi iliyokusudiwa na wanafunzi sasa wamerejea madarasani na wanaendelea na masomo yao.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa baada ya kupokea mradi huo na kumkabidhi kwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nyakato kwa niaba ya Shule zote mbili Nyakato na Kashozi aliishukuru Serikali ya Japani kwa kuisaidia Seriakali ya Tanzania hasa Mkoa wa Kagera wakati ule wa matattizo ya Tetemeko na kurejesha miundombinu ya Shule hizo ili wanafunzi warejee madarasani na Walimu kutekeleza majukumu yao ya kufundisha.
Pia Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliwahakikishia Wananchi, Walimu na Wanafunzi waliohudhuria hafla fupi ya makabidhano kuwa Serikali itaendelea kuboresha Sekta ya Elimu nchini kuanzia ngazi ya Awali mpaka Vyuo Vikuu. Katika shule za Msingi Serikali inatoa shilingi bilioni 23.5 kila mwezi ili kugharamia elimu bila malipo na watoto wameongezeka kutokana na kutokewepo na michango mbalimbali iliyokuwa inalipwa na wazazi hapo awali.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitoa wito kwa wazazi kuwaandaa watoto wao ikiwa ni pamoja kununua sare za shule, kufuatilia mienendo na maendeleo ya watoto wao shuleni kwa kushirikiana na walimu ili kujua kama watoto wao wanafika shule na wapatiwa elimu stahiki inayotakiwa kutolewa kwa mwanafunzi husika.
Serikali imeendelea kuboresha Sekta ya Elimu kwa kulipa maslahi ya watumishi wa umma wakiwemo walimu na kuhakikisha yanapatikana kwa wakati. Pili kuajiri walimu wa Shule za Sekondari 11,000 na Walimu wa Shule za Msingi 6,000 ambapo bado walimu wataendelea kuajiliwa ili kukidhi upungufu uliopo na utakaoendelea kujitokeza.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema pia Serikali mara baada ya kumaliza ujenzi wa maabara nchini sasa imetoa fedha za kujenga mabweni ili wanafunzi waweze kupata elimu na kulala shuleni. Pia Serikali imehakikisha upatikanaji wa vitabu katika shule za Sekondari kutoka uwiano wa kitabu kimoja kwa Wananfunzi 15 hadi kitabu kimoja kwa Wanafunzi wawili na Shule za Msingi kitabu kimo kwa Wanafunzi 8 hadi kitabu kimoja kwa Wanafunzi watano na mwelekeo ni kitabu kimoja kwa uwiano wa mwanafunzi mmoja.
Wanafunzi nchini wameaswa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuvitunza vitabu vinavyletwa na Serikali kwajili ya kuwasaidia katika masomo yao wasivichore michoro ya hovyo hovyo ndani au kukunja kurasa za vitabu hivyo na kupelekea uharibifu jambo ambalo litavikosesha vizazi vijavyo kupata elimu kwa kusaidiwa na vitabu hivyo.
Pamoja na Waziri Mkuu Kupokea mradi wa Elimu Kutoka Ubalozi wa Japani katika Shule ya Msingi Nyakato lakini pia alitembelea kiwanda cha AMIMZA kinachosindika na kuongeza thamani ya zao la kahawa kilichopo Kibuye Manispaa ya Bukoba. Aidha, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitembelea kituo cha Utafiti wa Kilimo Maruku ambapo alitoa wito kwa wakulima kupanda aina mpya ya mibuni inayozalisha kahawa kwa wingi na kuvumilia magonjwa inayozalishwa katika kituo hicho cha Utafiti Maruku.
Mwisho Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitembelea Shule ya Msingi Rweikiza yenye Mchepuo wa Kiingereza inayomilikiwa na Mbunge wa Bukoba Vijijini Jasson Rweikiza na kumaliza ziara yake ya siku nne Mkoani Kagera kwa kufanya majumuisho katika ukumbi wa Hoteli ya ELCT Bukoba. Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano Tanzania alianza ziara yake Mkoani Kagera Oktoba 6, 2018 na kuhitimisha ziara hiyo Oktoba 9, 2018.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa