- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Marco E. Gaguti awaagiza Maafisa Kilimo na Maafisa Ugani kutokaa Ofisini bali wakawatembelee kuwafundisha na kutoa elimu ya kilimo chenye tija wakulima katika Mkoa wa Kagera wenye fursa ya kustawisha mazao ya aina mbalimbali na masoko ya mazao hayo yapo ya kutosha.
Mkuu wa Mkoa Gaguti aliyasema hayo akifunga Maonesho ya Wakulima ya Nane Nane yaliyoadhimishwa kimkoa katika viwanja vya Kyakailabwa Manispaa ya Bukoba ambapo mara baada ya kutembelea mabanda mbalimbali ya wadau wa kilimo alisema sasa umefika wakati wa Wataalam wa kilimo kuwafuata wakulima na kuwapa elimu katika maeneo yao kuliko wakulima kuwafuata wataalam.
“Ninayo taarifa kuwa Kagera tunavyo viwanda vikubwa tisa lakini vinazalisha chini ya kiwango kutokana na kukosa mali ghafi zinazotakiwa kuzalishwa kutokana na kutopatikana kwa wingi. Sasa umefika wakati wakulima kuachana na kilimo cha mazoea cha kulima ekari kumi na kupata gunia 10 bali mkulima alime ekari moja avune gunia 20 za mazao, pia kuachana na ufugaji wa kufuga ng’ombe kumi na kupata lita 10 za maziwa bali mfugaji afuge ng’ombe mmoja apate lita 20 za maziwa.” Alifafanua Mhe. Gaguti
Mkuu wa Mkoa Gaguti alifafanua zaidi kuwa mkoa wa Kagera unayo fursa kubwa zaidi ya kilimo kwani hali ya hewa na ardhi yake inaruhusu kilimo cha zao lolote kwa hiyo wananchi wanatakiwa kuitumia fursa hiyo kuhakikisha wananlima mazao mbalimbali kwa wingi na masoko ya mazo hayo yapo kwakuwa Kagera inapakana na nchi tano ambazo ni fursa ya masoko ya mazao yanayolimwa.
Aidha, Mkuu wa Mkoa Gaguti aliwahakikishia wananchi katika maonesho hayo kuwa sasa Serikali inafanya upya tathimini ya Vyama vya Ushirika kuhakikisha vinamsaidia mkulima na vinakuwa na nyenzo kubwa ya kuhakikisha mazao ya wakulima yanapata masoko kwa wakati lakini si Vyama hivyo vya Ushirika kushiriki kuwanyonya wakulima.
Katika Hatua nyingine Mwenyekiti wa Maandalizi ya Maonesho ya Nane Nane Mkoa wa Kagera Bw. Isaya Tendega ambaye ni Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji Ofisi ya Mkuu wa Mkoa alisema kuwa changamoto kubwa katika maonesho hayo ni baadhi ya Taasisi muhimu za Serikali kutoshiriki katika maonesho hayo na wananchi wangependa kupata elimu kutoka kwao.
Akizitaja baadhi ya Taasisi hizo Bw. Isaya alisema kuwa ni pamoja na Taasisi ya Bima, Wakala wa Vipimo Tanzania, Wakala wa Majengo, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Wakala wa Barabara Tanzania (TANROAD), Poilsi na Wengineo. Bw. Isaya alisisitiza kuwa Taasisi hizo ni muhimu sana kushiriki katika maonesho hayo kwani zinatoa huduma kwa wananchi na wangependa kupata elimu juu ya huduma zao.
Mkuu wa Mkoa Gaguti akifafanua namna ya kutatua changamoto ya Taasisi mbalimbali sa Serikali kushiriki katika Maonesho ya Nane Nane alitoa agizo kuwa lazima mwakani 2019 Taasisi za Serikali zinazotoa huduma kwa wananchi zishiriki ili kuwaelimisha wananchi kuhusu huduma wanazozitoa ili iwe rahisi kwao kupata elimu juu ya huduma hizo muhimu.
Kaulimbiu ya maonesho ya Nane Nane mwaka 2018 ilikuwa inasema “Wekeza katika Kilimo kwa Maendeleo ya Viwanda” na Mkoa wa Kagera ulikuwa unaadhimisha Maonesho ya Nane Nane kwa mara ya 11 mfurulizo ambapo wadau mbalimbali walishiri na mshindi wa kwanza katika maonesho hayo ni Kampuni ya Kagera Sukari inayotekeleza vizuri sera ya Tanzania ya Viwanda kwa kulima kisasa na kuzalisha Sukari.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa