- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti awaapisha na kuwaasa wajumbe wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba Mkoani Kagera kutekeleza majukumu yao kwa uaminifu, uadilifu pia kwa kutenda haki na kufuata sheria ili waweze kuaminika kwa wananchi wanaowahudumia.
Mkuu wa Mkoa Gaguti alisema hayo April 12, 2019 wakati akiwaapisha wajumbe wanne wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya za Ngara na Karagwe ambapo aliwataka wajumbe hao kujikana wenyewe na kujitoa kikamilifu katika kazi zao ili kutenda haki kwa wananchi.
“Viongozi wengi wanaofanya kazi katika Mabaraza ya Ardhi na Nyumba Mkoani Kagera wamekosa uhalali kwa wananchi wanaowahudumia kutokana na kutotenda haki, sasa nawaasa ninyi mlioapishwa kuhakikisha mnatekeleza kazi zenu kwa kutenda haki ili muweze kuwa halali kwa wananchi wenu.” Alisistiza Mkuu wa Mkoa Gaguti
Aidha, Mkuu wa Mkoa Gaguti alisema kuwa katika Ofisi yake asilimia 80% hadi 90% ya malalamiko ya wananchi ni kuhusu migogoro ya ardhi, pia alisema kuwa hata katika ziara wilayani au viongozi wa Kitaifa wanapofika Mkoani Kagera malalamiko makubwa ya wananchi ni ya ardhi kutokana na Mabaraza ya ardhi na Nyumba ya Wilaya kutokutekeleza majukumu yake ipasavyo.
Vilevile Mkuu wa Mkoa Gaguti alisema kuwa wananchi wa Mkoa wa Kagera wamekuwa masikini kwa kupoteza fedha nyingi kwasababu ya kufuatilia kesi za ardhi katika Mahakama za chini hadi Mahakama za juu ambapo kama Mabaraza ya Ardhi na Nyumba yangekuwa yanatekeleza wajibu wake vizuri wananchi wasingekuwa wanapoteza fedha zao na muda kutafuta haki hadi Mahakama za juu.
Mwisho, Mkuu wa Mkoa Gaguti alitoa rai kwa Viongozi wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya kutoa elimu kwa wananchi kuliko kujikita sana katika mashauri, pia alisisitiza Mabaraza ya ngazi za chini mfano ya Vijiji na Kata kufanya kazi zake kupunguza migogoro ya ardhi jambo linalopelekea wananchi kujichukulia sheria mikononi kutokana kutoridhika na maamuzi yanayotolewa na kuufanya mkoa wa Kagera kuwa miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa mauaji na kujichukulia sheria mikononi.
Katika hatua nyingine Jaji Lucia Gamuya Kairo Jaji Mfawidhi wa Mhakama Kuu Kanda ya Bukoba aliwakumbusha wajumbe wanne walioapishwa kutekeleza majukumu yao kwa kutenda haki tena kwa uaminifu na uadilifu ili kutatua na kumaliza migogoro ya ardhi Mkoani Kagera
Jaji Kairo alisema kuwa Mabara ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya hayapo chini ya Mahakama lakini kwasababu yanashughulika na kutoa haki wananchi wanajua kuwa nayo ni sehemu ya Mahakama ambapo alisistiza kuwa kwa miaka minne aliyokaa Kagera ardhi imekuwa na malalamiko mengi na Mabaraza hayo yapo katika nafasi tatu za mwanzo kwa kulalamikiwa na wananchi katika kujihusisha na vitendo vya rushwa.
Jaji Kairo alisema kuwa Rushwa inapofusha utoaji wa haki na kuwataka wajumbe wasijiingize katika vitendo vya rushwa na kuwakumbusha kuwa Haki iliyocheleweshwa ni sawa na haki iliyopotea na Haki iliyoharakishwa ni sawa na haki iliyopotea ambapo aliwataka wajumbe hao kutekeleza majukumu yao kwa ulinganifu bila kuchelewesha au kuwaisha haki katika maauzi yao.
Wajumbe walioapishwa na Mkuu wa Mkoa Gaguti Aprili 12, 2019 ni Bw. Charles Mbeikya na Bi Christina Mugasha Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Ngara, wengine ni Bw. Longino Frederick na Bi Lucletia Shubilo Saulo Balaza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Karagwe. Katika Mkoa wa Kagera Kuna jumla ya Mabaraza ya Ardhi na Nyumba manne katika Wilaya za Bukoba, Muleba, Karagwe na Ngara.
Aidha, wajumbe wa Baraza la Ardhi na Nyumba huchaguliwa kila baada ya kipindi cha miaka mitatu na Baraza moja linaweza kuwa na wajumbe sita hadi saba lakini Mwenyekiti wa Baraza anatakiwa kuwa na wajumbe wasiopungua wawili wakati akisikiliza na kuendesha mashauri.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa