- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
MAPATO YA SERIKALI YASIONDOKE~RC SHIGELA
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kagera ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe Martine Shigela amewataka wafanyabiashara wanaotumia kituo cha forodha cha mpaka wa Mutukula kuwa wavumilivu na kuendela kufuata utaratibu wa ulipaji wa kodi unaotakiwa kwenye mazao na bidhaa, wakati Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi na Uongozi wa Mkoa wakipitia sheria ndogo za Halmashauri na kuja kuweka makubaliano ya ukusanyaji wa tozo hizo.
Akizungumza na wafanyabiashara hao, leo tarehe 28.06.2023 baada ya kukagua mpaka wa Tanzania na Uganda eneo la Mutukula ameeleza kuwa kutokana na sintofahamu kati ya Wafanyabiashara na Halmashauri ya Missenyi ni vema Mkurugenzi na Afisa Biashara wakatoa ufafanuzi kwa Kamati ya Usalama ya Mkoa ili kuwa na uelewa wa pamoja kama viongozi na kisha kuja kutoa mrejesho na elimu kwa wafanyabiashara hao.
“Nimefarijika sana kuona wafanyabiashara wa Wilaya ya Missenyi mko tayari kuchangia Halmashauri. Kwahiyo Halmashauri itakapoleta mrejesho ni vizuri mkakaa kwa pamoja na kukubaliana kuwa mnauwezo wa kuchangia mapato ya Serikali kwa viwango hivi ili mapato ya Serikali yasiondoke”, ameeleza Mhe. Shigela
Ameendelea kueleza kuwa Halmashauri ikitoa kabisa ushuru, Halmashauri haitaweza kujiendesha na haitaweza kutoa huduma kwa wananchi. Hivyo ni vema ukawekwa utaratibu ambao Halmashauri itapata mapato na wananchi wakafanya biashara bila kuwa na kikwazo chochote
Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Wilaya ya Missenyi, Ndg. Bakuza Hassan ameeleza kuwa tozo zinazotozwa hawazielewi,ushuru ni mkubwa ukilinganisha na maeneo mengine na Halmashauri haitoi elimu ya kutosha juu ya tozo hizo ili kuwapa uelewa wafanyabishara hao.
Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Ndg. Toba Nguvila ameeleza kuwa kutokana na agizo la Mheshimiwa Rais kuruhusu mazao kuendelea kusafirishwa nje ya Nchi kwa masharti ya mfanyabiashara awe amekidhi vigezo na kutekeleza taratibu zote za vibali vinavyotakiwa uongozi umefika mpakani hapo ili kuona shughuli za kiutendaji na kupokea changamoto za wafanyabiashara zinazotokana na agizo hilo.
Katika ziara hiyo Mhe. Shigela amezungumza na watumishi wa kituo hicho na kukagua eneo la mpaka kati ya Tanzania na Nchi ya Uganda.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa