- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Waziri Mhagama Asitisha Awamu ya Pili ya Ujeshaji wa Miundombinu ya Huduma za Jimii Baada ya Tetemeko la Ardhi Kagera Septemba 2016
Hatimaye Serikali yahitimisha awamu ya pili ya urejeshaji miundombinu ya huduma za jamii iliyoharibiwa na Tetemeko la Ardhi lililotokea Septemba 10, 2016 baada ya kuridhishwa na kazi iliyofanyika kuonekana inaendana na thamani ya fedha zilizotolewa katika maeneo mbalimbali kwenye Halmashauri za Wilaya Mkoani Kagera.
Akiwa Mkoani Kagera katika ziara ya siku mbili Julai 11 hadi 12, 2017 Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Ajira na Watu Wenye Ulemavu Jenista Mhagama alitembelea miradi mkubwa mitano katika Halmashauri za Bukoba, Karagwe, Kyerwa Misenyi na Manispaa ya Bukoba ambayo imekuwa ikitekelezwa ili kurejesha huduma za jamii baada ya kuharibiwa na Tetemeko mwaka 2016.
Akiwa Wilayani Kyerwa Mhe. Mhagama alitembelea na kukagua ujenzi wa Zahanati mpya ya Rwele inayojengwa katika Kijiji cha Kikuru Kata Kikuru itakayogharimu zaidi ya milioni 125. Wilayani Karagwe pia alitembelaea na Kukagua ujenzi wa wodi mpya ya wazazi, chumba cha kuhifadhia maiti na chumba cha jenereta katika Kituo cha Afya Kayanga ambapo aliridhika na maendeleo ya ujenzi kulingana na kiasi cha fedha kilichotolewa.
Katika Kituo cha Afya kayanga wodi ya wazazi, chumba chumba cha kuhifadhia maiti na chumba cha jenereta vitagharimu jumla ya shilingi 170,714,521/= ujenzi utakapokamilika. Aidha, Waziri Mhagama alihaidi kuongeza kiasi cha shilingi 100,000,000/= ili kujenga wodi nyingine katika kituo hicho kutokana na kutoa huduma kwa wananchi wengi. Miradi ya afya ya Kyerwa na Karagwe itakamilika Mwezi Septemba na Octoba 2017.
Baada ya kukagua na kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi Waziri Mhagama alikabidhi majukumu yote ya ujenzi kwenye Halmashauri za Wilaya za Karagwe na Kyerwa chini ya Usimamizi wa Ofisi ya mkuu wa Mkoa ambapo alisitisha awamu ya pili ambayo usimamizi ulikuwa unafanywa na ofisi yake lakini kwasasa majukumu yote yamerudishwa kwa Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri na hiyo ndiyo awamu ya tatu ya urejeshaji miundombinu.
Katika Wilaya ya Missenyi Kikosi Kazi cha Jeshi la Wananchi Tanzania kilichokuwa kinajenga Kituo cha Afya Kabyaile kilikabidhi Majengo 11 ambayo yamekamilika tayari kwa kutumika ambapo majengo hayo yalikabidhiwa kwa Katibu Tawala wa Mkoa Bw. Diwani Athuman naye akamkabidhi Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi mbele ya Waziri Mhagama Viongozi wa Mkoa na Wananchi.
Waziri Mhagama akiongea na wananchi alimwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi kuhakikisha anamalizia kazi ndogo ndogo ambazo zimebakia na kufikia mwezi Desemba 2017 kazi zote zinatakiwa kuwa zimekamilika ili wananchi wapate huduma kikamilifu. Naye Mwakilishi wa Jeshi la Wananchi Tanzania kutoka Makao Makuu Kanali Sylvester Ghuliku aliwaasa wananchi kuyatunza majengo hayo ili yadumu na kutoa huduma kwajili ya kupata huduma.
Katika Wilaya ya Bukoba Waziri Mhagama alitembelea kituo cha Kulelea Wazee Kiilima na kujionea ukarabati wa majengo ya kituo hicho ambao uligharimu zaidi ya milioni 70 ambapo aliridhishwa na ukurabati huo ambapo aliagiza Mkoa na Halmashauri kuendelea kukiangalia kwa karibau kituoa hicho. Aidha, alimwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Bukoba kutenga bajeti ya kujenga nyumba za watumishi katika kituo hicho.
Waziri Mhagama pia alishuhudia makabidhiano ya Mabweni mawili katika Shule ya Sekondari Omumwani kati ya Kikosi kazi cha Jeshi la Wananchi wa Tanzania na Katibu Tawala wa Mkoa pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba pia na makabidhiano ya shule hiyo iliyokuwa inamilikiwa na Jumuiya ya Wazazi wa Chama cha Mapinduzi na kurudishwa Serikalini na Rais John Pombe Magufuli Januari 2, 2017.
Waziri Mhagama akiwa katika ziara hiyo ujumbe mkubwa alioutoa kwa viongozi na wananchi wa Mkoa wa Kagera ni kutumia vizuri fedha zinazotolewa na Serikali kurejesha miundombinu ya huduma za jamii kwa kuzingatia matumizi na maelekezo ya fedha hizo bila kuzichezea fedha hizo kwani ni za moto na mtu akizichezea moto utamchoma .
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum M. Kijuu akitoa pongezi kwa Waziri Mhagama aliishukuru Wizara yake kuwa karibu na uongozi wa Mkoa wa Kagera kuhakikisha Miundombinu ya huduma za jamii zinarejea tangu Tetemeko lilipotokea Mwezi Septemba 2016. Pia alimhakikishia Waziri Mhagama kuwa miradi yote itaisimamia ikamilike ili iweze kutoa huduma safi kwa wananchi.
Aidha, Mkuu wa Mkoa aliwashukuru wananchi kwa uvumilivu wao tangu Tetemeko litokee hadi sasa na aliwashukuru kwa ushirikiano waliounesha kwa Kikosi Kazi cha Jeshi la Wananchi Tanzania kilichokuwa kinajenga Kituo cha Afya Kabyaile. Pia alikishukuru kikosi hicho kuwa kufanya kazi kwa weledi mkubwa aidha, kuto msaada kwa wananchi hasa wa huduma za afya na maji safi na salama katika eneo linalozunguka kabyaile.
Mwisho Mkuu wa Mkoa wa Kagera alimwomba Waziri Mhagama kuusaidia Mkoa katika kufuatilia vifaa vya afya kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuletwa katika kituo cha Afya Kabyaile ili Majengoi hayo mapya yasiake bila vifaa ambavyo ni vya kisasa jambo ambalo linaweza kupelekea majengo hayo kuharibika kabla ya muda wake.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa