- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Mkoa wa Kagera Wazindua Utoaji wa Chanjo Mpya ya Kujikinga na Saratani na Mlango wa Kizazi Kwa Wasichana Waliotimiza Umri wa Miaka 14
Mkoa wa Kagera wazindua rasmi utoaji wa Chanjo Mpya ya Kujikinga na Saratani ya Mlango wa Kizazi kwa wasichana waliotimiza umri wa miaka ya 14 na uzinduzi huo umefanywa na Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum M. Kijuu Katika Kituo cha Afya Kaigara Wilayani Muleba Aprili 23, 2018.
Akiwahutubia wananchi na wanafunzi waliohudhuria kituoni hapo kupata chanjo ya Saratani ya Mlango wa Kizazi Mhe. Kijuu alisema kuwa kila mwaka wiki ya mwisho ya mwezi Aprili huwa ni wiki ya chanjo ulimwenguni, lakini kwa mwaka huu 2018 maadhimisho ya Wiki ya chanjo Serikali imeamua kuanza kutoa chanjo mpya ya kinga ya Saratani ya Mlango wa Kizazi.
Mhe. Kijuu alisema kuwa Serikali inatarajia kutoa chanjo ya kinga ya Saratani ya Mlango wa Kizazi kwa wasichana waliotimiza miaka 14 na waliosajiliwa ambao jumla ni 35,917 kwa Mkoa wa Kagera na chanjo hiyo ya kinga itatolewa bure na Serikali bila mwananchi kuchangia chochote.
“Saratani ya Mlango wa Kizazi ni ugonjwa unaoongoza kwa kuwaua akina mama katika nchi yetu, Serikali imegharamia chanjo ya kinga ya ugonjwa huo itatolewa bure kwa watoto wetu wasichan waliotimiza umri wa miaka 14 nipende kuwahamasisha wazazi wa watoto kuhakikisha watoto wanachanjwa kujikinga na Saratani ya Mlango wa Kizazi,” Alisisitiza Mhe. Kijuu
Katika hatua nyingine Mkuu wa Wilaya ya Muleba akitoa salamu za Wilaya alisema kuwa Wilaya ya Muleba imejipanga vizuri kutekeleza zoezi hilo kwa ufanisi kwa kuwahamasisha wananchi ambao ni wazazi na katika Wilaya hiyo ya Muleba wanatarajiwa kuchanjwa wasichana waliotimiza umri wa miaka jumla 5,911.
Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Dk. Siliacus Mtabuzi amabaye ni mwangalizi wa zoezi hilo alisema kuwa alifurahishwa na mwamko wa wasichana katika uzinduzi Kaigara pia Wilaya zote alizopita kuona maandalizi ya utoaji wa chanjo hiyo aliridhishwa na maandalizi katika vituo ambapo aliupongeza mkoa na kusema kuwa anaona dalili za Kagera kufanya vizuri katika chanjo hiyo.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera Dk. Thomas Rutachunzibwa alisema kuwa Idara ya Afya imejipanga vizuri kuhakikisha wasichana wote 35,917 watapatiwa chanjo mpya ya kujikinga na Saratani ya Mlango wa Kizazi na tayari timu mbalimbali za ufutailiaji zimeundwa kuhakikisha kila Halmashauri ya Wilaya inafanya vizuri katika zoezi zima na kutatua changamoto zitakazojitokeza kwenye zoezi.
Angalizo, Mkuu wa Mkoa wa Kagera alitoa angalizo katika uzinduzi huo kwa watu ambao watajaribu kupotosha maana ya zoezi hilo kuwa watachukuliwa hatua kali za kisheria ambapo pia aliwaagiza na Wakuu wa Wilaya ambao ni Wenyeviti wa Kamati za Ulinzi na Usalaama katika maeneo yao kuhakikisha wanashughulika na wote watakaojaribu kupotosha maana ya zoezi la utoaji wa chanjo hiyo.
Chanjo Mpya ya Kujikinga na Saratani ya Mlango wa Kizazi ambayo husababishwa na virusi vijulikanavyo kama Human Papilloma Virus inatolewa kwa wasichana waliotimiza umri wa miaka 14, majaribio ya chanjo hiyo yalifanyika mkoani Kilimanjaro tangu mwaka 2014. Chanjo hiyo inatolewa mara mbili kwanza msichana anapofikisha umri wa miaka 14 pia dozi ya pili ni baada ya miezi sita.
Aidha, zoezi la utoaji Chajo Mpya ya Kujikinga na Saratani ya Mlango wa Kizazi ni zoezi endelevu kwa wasichana watakaokuwa wanatimiza miaka 14 kila mwezi. Kagera chanjo hiyo inatolewa katika vituo 1,182 ambavyo ni vya kawaida vya kutolea huduma za afya, baadhi ya shule zilizochzguliwa na katika baadhi ya maeneo ya kijamii yaliyochaguliwa chanjo hiyo itatolewa kwa njia za huduma za mkoba.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa