- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Mkoa wa Kagera washiriki katika kikao cha pamoja cha kujadili mikakati ya usafirshaji samaki na mazao yake nje ya nchi kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwanza ambapo kikao hicho kilichofanyika Jijini Mwanza Juni 1, 2020 kilizishirikisha Wizara tatu za Viwanda na Biashara, Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mifugo na Uvuvi pamoja na Mikoa ya Kagera Mwanza na Mara.
Waziri wa Ujenzi , Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe ambaye aliongoza kikao hicho wakati wa ufunguzi alisema kuwa lengo la kikao ilikuwa ni kuondoa vikwazo vyote kwa kushirikisha sekta zote zikiwemo Wizara na mikoa kuhakikisha Samaki na mazao yake kutoka Tanzania yafika kwenye masoko duniani kwa wakati.
Waziri Kamwelwe alisema kuwa wanufaika wakubwa katika usafirishaji wa samaki na mazao yake ni Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, Mamlaka ya udhibiti wa Hali ya Hewa pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania lakini ikiwa ni pamoja na kuongeza ajira kwa wavuvi na kutoa fursa kwa viwanda vya ndani kusindika na kusafirisha mzigo wa kutosha kwenda nchi za Ulaya.
“Lengo kuu la kutaka kuboresha usafirishaji wa Samaki ni kutaka pia kuongeza bidhaa nyingine za mifugo na kilimo, mfano katika Safari nne ambazo Shirika la Rwanda na Ethiopia yamefanya imebainika kuwa mashirika hayo yanahitaji kiwango kikubwa cha mzigo aidha, mzigo huo uwe wa uhakika”. Alisisitiza Waziri Kamwelwe.
Katika upande wa wasafirishaji au wamiliki wa Viwanda wanaiomba Serikali kupunguza tozo za usafirishaji ili kushindana na washindani wengine katika biashara ya usafirishaji wa Samaki na mazao yake . Mkoa wa Kagera katika Kikao hicho uliwakilishwa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti
Kikao hicho kilikubaliana kuchukua hatua za haraka ili kuhakikisha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwanza unatoa huduma bora hasa katika usafirishaji wa mizigo na makubaliano hayo ni kama ifuatavyo: Ujengwe uzio kuzunguka Uwanja wa Kimataifa wa Mwanza, Kuweka mpango Mkakati wa kuhakikisha tani 200 za samaki zinazozalishwa kila siku na viwanda vyote nchini zinasafirishwa kupitia uwanja wa Ndege wa Mwanza badala ya tani 67 tu.
Aidha, wajumbe wa kikao hicho walikubaliana kupanua mnyororo wa thamani katika usafirishaji ili mashirika ya Ndege yapate mzigo wa kutosha hasa katika mazao ya kilimo na mifugo ambapo Wizara za Elimu, Mipango na fedha pamoja na Kilimo zitashirikishwa katika vikao vijavyo ili kuhakikisha wanakuwa katika mpango mzima wa mnyororo wa thamani.
Mwisho kikosi kazi cha Makatibu Wakuu wa Wizara husika waliagizwa na Kikao kuanza kazi mara moja ili kuhakikisha makubaliano yote yanatekelezwa kwa wakati bila mkwamo wowote.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa