- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Mkoa wa Kagera wazindua rasmi mradi Tija Tanzania mradi ambao unaolenga kuongeza uzalishaji na Usalama wa chakula pia na kuinua kipato cha wakulima kwenye mazao matatu ya Maharage, Mihogo na Mahindi katika Halmashauri za Wilaya za Karagwe, Missenyi, Muleba na Kyerwa.
Mradi wa Tija Tanzania unaofadhiliwa na Shirika la Mapinduzi ya Kijani Afrika (AGRA) unajikita katika mazao matatu yaliyotajwa hapo juu (Maharage, Mahindi na Mihogo) katika kuahakikisha kwamba mkulima kupitia mazao hayo anafundishwa na kuelekezwa kuzalisha kwa ufanisi ili kuongeza uhakika wa chakula, lakini pia kuunganishwa na masoko ya uhakika ili kuuza ziada kwa faida na kuongeza kipato kwenye kaya.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum M. Kijuu akizindua mradi huo rasmi Juni 27, 2018 katika Hoteli ya Bukoba ELCT alilishukuru Shirika la AGRA kwa kufadhili mradi wa Tija Tanzania na kusema kuwa sasa utakuwa mradi wa Tija Kagera kwa kuongeza uzalishaji na uhakika wa chakula pia na kuinua kipato cha mkulima wa Mkoa wa Kagera.
“Uzalishaji wetu Kagera kwa mazao ya Mahindi, Maharage na Mihogo bado ni mdogo ambapo tija ya uzalishaji kwa hekta kwa mazao hayo ni wastani wa tani moja ya maharage, tani 2.5 za mahindi na tani 10 za mihogo. Uzalishaji huo ni mdogo mno ukilinganisha na fursa ya kilimo inayopatikana katika mkoa wa Kagera, hivyo tunapopata fursa ya kuwa na mradi kama Tija Tanzania ni lazima tuitumie vizuri.” Alisisitiza Mhe. Kijuu
Naye Bwana Thiery Ngonga mwakilishi wa Rais wa AGRA kutoka Nairobi nchini Kenya alisema nchi ya Tanzania ni moja wapo kati ya nchi kumi na moja zinazofadhiliwa na Shirika la Mapinduzi ya Kijani Afrika (AGRA) lakini bado Tanzania ilikuwa haifanyi vizuri katika kilimo na kusema kuwa sasa wameweka mkakati wa kuhakikisha Tanzania inafanya vizuri katika mazao ya Mahindi, maharage na Mihogo kupitia Mkoa wa Kagera.
Mradi wa Tija Tanzania tangu uanze Mkoani Kagera sasa umetimiza miezi sita na unatarajia kuwafikia wakulima 200,000 ambapo Mkuu wa Mkoa Mhe. Kijuu alisema mradi huo ni lazima kuwafikia wakulima zaidi ya hao kwa kuwapatia mbegu za kisasa za Mahindi, Maharage na Mihogo ili kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao hayo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa