- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum M. Kijuu amewaapisha wajumbe wanne wapya wa Baraza la Aardhi na Nyumba la Bukoba na kukamilisha wajumbe sita wanaotakiwa katika Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya ili kuongeza ufanisi katika baraza na kuondoa migogoro ya ardhi mkoani Kagera.
Akiwaapisha ofisini kwake Mkuu wa Mkoa Mei 4, 2017 aliwaasa wajumbe hao kuzingatia miiko ambayo imo katika Kanuni za Mahakama za Migogoro ya Ardhi, Tangazo la Serikali namba 174 ya mwaka 2003 ambazo ni; Moja, Mjumbe wa Baraza awe mtu mwenye kujishimu na heshima yake ionekane kwake na kwa Baraza.
Pili, Aishi na aonekane kuwa ni mtu asiye na upendeleo wa aina yoyote na waadawa (Pande zinazoshitakiana) wakimuona waondoe shaka kuwa ni mtu mwenye kuweza kupendelea. Tatu, Asishiriki kutoa maamuzi au kusikiliza kesi yoyote inayomhusu yeye binafsi au mtu yeyote katika familia yake. Nne, Ajue mipaka ya kazi yake na kwa namna yoyote asijaribu au kuonyesha umma kuwa yeye anafanya kazi za Mwenyekiti.
Tano, Mjumbe wa Baraza wakati wote awe msiri kuhusiana na kesi ambazo bado kutolewa uamuzi. Harusiwi kusema nje ya Baraza, chochote kinachohusu undani wa kesi ambayo bado haijaamuliwa. Sita, Hairuhusiwi kuwa na urafiki na upande wowote katika kesi inayoendelea kusikilizwa. Saba, Ajiepushe kuzungumza au kufanya mawasiliano yoyote na wadaawa katika eneo la Baraza na kwa hali yoyote haruhusiwi kutoka nje ya jengo la Baraza na kwenda kuzungumza na wadaawa au jamaa zao kabla au baada ya saa za kazi.
Nane, Mjumbe haruhusiwi kuwa wakili wa upande wowote katika kesi, haruhusiwi kutoa ushauri au kuwaandikia wadaawa kitu chochote.Tisa, Awahi na kuhudhuria katika vikao kama itakavyokuwa imepangwa na Mwenyekiti na asikose kuhudhuria mfululizo wa vikao kwa kipindi kinachozidi mwezi mmoja bila sababu ya kuridhisha.
Kumi, Mjumbe asimshawishi Mwenyekiti wa Baraza ili apangiwe kuketi katika kesi fulani. Kumi na Moja, Baada ya kukamilika kesi yoyote, mjumbe atatoa maoni yake kwa maandishi bila kuchelewa. Mwisho Mjumbe asipokee au kuomba zawadi kama hongo au takrima kutoka upande wowote wa waadawa.
Akitoa shukrani Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Bukoba Mheshimiwa Rogate Assey alimshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kuwaapisha wajumbe pia aliwasistiza wajumbe hao walioapishwa kuzingatia miiko na kuzingatia viapo vyao katika kutekeleza majukumu yao.
Mhe. Assey alimweleza Mkuu wa Mkoa kuwa Mkoa wa Kagera ni mkoa wenye migogoro mingi ya ardhi lakini kutokana na umakini katika utendaji wa Baraza la ardhi na Nyumba la Bukoba umeimarika na kupitia Baraza hilo migogoro mingi ya ardhi imetatuliwa kwa kiwango kikubwa, mlundikano wa Kesi umepunguzwa sana aidha, malalamiko na kero za wananchi kuhusu ardhi zimetatuliwa.
Pia alitoa rai kwa wajumbe kuwa hawaruhusiwi kushawishi kwa njia yoyote isipokuwa watekeleze wajibu wao kulingana na kanuni na taratibu za sheria na kuzingatia miiko waliosomewa na Mkuu wa Mkoa.
Wajumbe walioapishwa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera ni Bw. Nestory Makwaya, Bw. Henry Mutayanga, Bi Fortunata Rutabanzibwa na Bi Leonada Mpanju. Katika Mkoa wa Kagera kuna Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya Manne ambayo ni Bukoba, Muleba, Ngara na Karagwe. Aidha Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya Karagwe linahudumia pia Wilaya ya Kyerwa. Wajumbe wa Mabaraza hayo wanachaguliwa na kudumu kwa kipindi cha miaka mitatu na wanaruhusiwa kuteuliwa zaidi ya muhula mmoja.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa