- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti ashukuru na kutoa vyeti vya ushiriki kwa Waandishi wa Habari na vyombo mbalimbali vya Habari Mkoani Kagera(Redio za Mkoani Kagera) kwa namna vilivyojitoa katika kuhakikisha Wiki ya Uwekezaji inafanikiwa kwa kiwango kikubwa.
Akizungumza na Waandishi, Wahariri na baadhi ya wamiliki wa Vyombo vya habari Mkoani Kagera ofisini kwake Agosti 29, 2019 Mhe. Gaguti alisema anatoa shukrani kubwa kwa kila mwandishi na vyombo vyote vilivyoshiriki Wiki ya Uwekezaji Kagera kwa kujitoa kikamilifu kuitangaza wiki hiyo na kuhakikisha inafanikiwa.
“Kupitia fursa hii nawashukurua sana wote lakini niseme tu kuwa sasa kazi ndiyo imeanza kwani baada ya kufungua milango na madirisha ya mkoa wetu katika uwekezaji tutakuwa na mipango mingi ya kukaa na wawekezaji kuona namna gani uwekezaji unafanyika niombe tuendelee kushirikiana na kutangaza kwa nguvu zaidi juhudi hizi ili tufikie tunapopahitaji.” Alishukuru na kusisitiza Mhe. Gaguti
Naye Katibu wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoani Kagera na Mwandishi wa Gazeti la Mwananchi Bw. Phinias Bashaya kwaniaba ya waandishi waliohudhuria alimshukuru Mkuu wa Mkoa na uongozi wote kwa kuwashirikisha waandishi wa habari kuanzia maandalizi hadi kilele cha Wiki ya Uwekezaji Kagera ikiwa ni pamoja na waandishi kupatiwa banda maalum la kuchakatia habari zao wakati wote wa Wiki ya Uwekezaji Kagera.
Bw. Bashaya pia alsema kuwa kupitia Wiki ya Uwekezaji Kagera Waandishi wa habari walipata fursa mbalimbali ikiwemo fursa ya kwenda katika Mgodi wa STAMIGOLD Wilayani Biharamulo kupata mafunzo ya siku tatu kujifunza namna Mgodi huo pekee nchini unavyoendeshwa na Watanzania Wazalendo baada ya kuendeshwa na wazungu kipindi cha miaka ya nyuma.
Mkoa wa Kagera tayari umeanza kunufaika na Wiki ya Uwekezaji iliyofanyika tarehe 12 hadi 17 Agosti, 2019 kwani Kampuni ya Chai ya Kagera Tea imepata soko la chai nchini Rwanda, Kampuni ya Hirwa Group Ltd ya utengezaji wa Akandi Beverages imepata soko la kuuza bidhaa hizo tani 10 kila mwezi nchini Rwanda, Wafanyabiashara wa Dagaa Wilayani Muleba wamepata soko la kusafirisha tani 30 za dagaa kila mwezi nchini Rwanda.
Fursa nyingine ni ujenzi wa masoko ya kimkakati na maghara katika mipaka ya Rusumo na Kabanga Wilayani Ngara ambapo Mohamed Dewij na Kampuni yake ya Mohamed Enterprises tayari wameonesha nia, Muhoja Kabaru wa Kahama Oil Mills Company Ltd tayari ameonesha nia ya kuanzisha kilimo cha alizeti na kujenga kiwanda cha kusindika alizeti hizo pia na wawekezaji wengine wengi wanaendelea kuonesha nia katika fursa mbalimbali, Kagera inasonga mbele.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa