- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Wananchi Wajitokeza Kwawingi Kunufaika na Huduma za Madaktari Bingwa Mkoani Kagera
Uongozi wa Mkoa wa Kagera wafanikisha zoezi la kutoa huduma ya afya ya Madaktari Bingwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa mjini Bukoba na kuwahudumia wananchi 3146 waliokuwa na magonjwa yaliyowasumbua kwa muda mrefu na yalihitaji huduma za kibingwa.
Katika huduma hiyo iliyokuwa imekusudiwa kutolewa kwa siku saba kuanzia tarehe 18 hadi 24 Septemba, 2017 kutokana na wingi wa wananchi wenye matatizo iliongezwa siku hadi tarehe 28 Septemba, 2017 ambapo wananchi walikuwa na matatizo mablimbali ya kiafya 5700 walijitokeza kuhudumiwa.
Akitoa taarifa mara baada ya zoezi hilo Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Kagera Dk. John Mwombeki alisema wananchi walijitokeza kwa wingi juu ya makadirio yao ya awali jambo ambalo lilipelekea baadhi ya wagonjwa zaidi ya 2000 waliojiandikisha kutowaona Madaktari Bingwa.
Dk. Mwombeki alisema kati ya wananchi 5700 waliojiandikisha ni 3146 walioonwa na Madaktari Bingwa na kuhudumiwa katika maganjwa ya Makoromeo, Sikio na Pua, Macho, Meno, Magonjwa ya wakinamama, Magonjwa ya ndani, Mifupa, Magonjwa ya watoto na Magonjwa ya mfumo wa mkojo kwa wanaume.
Aidha, kati ya wagonjwa 3146 walioonwa na Madaktari Bingwa wagonjwa 446 walifanyiwa upasuaji mkubwa. Gharama za kuwaona Madaktari Bingwa hao ilikuwa ni Shilingi 5000 kujiandikisha na shilingi 30,000 kwa wagonjwa ambao walishauriwa kufanyiwa upasuaji.
Akizungumzia zoezi hilo lilivyofanikishwa Mganga Mkuu wa Mkoa Dk. Thomas Rutachunzibwa alisema zoezi hilo lilifanikiwa kutokana na kufunga mfumo wa mapato katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera na kuanza kukusanya kiasi kikubwa cha fedha ambazo zilizopelekea kusogeza huduma hiyo karibu na wananchi wa Mkoa wa Kagera.
Pia katika zoezi hilo lililofanyika kwa siku kumi kiasi cha shilingi milioni 34,886,338 taslimu zilikusanywa pamoja na wagonjwa 1,010 kati ya 3,146 walipata huduma za matibabu na kulipia huduma hizo kwa njia ya Bima ya Taifa (NHIF) na Bima za Mashirika mengine kama AAR, TANESCO, NSSF na STRATEGES.
Katibu Tawala Mkoa wa Kagera Kamishina Diwani Athumani akizungumzia zoezi hilo alisema kuwa jukumu la Serikali ni Kusogeza huduma za kijamii karibu na wananchi, pia alisema kuwa baada ya kupokea ombi la kuleta huduma za Madaktari Bingwa Mkoani Kagera kutoka kwa Mganga Mkuu wa Mkoa alihakikisha kuwa vifaa na miundombinu yote iliyohitajika inakamilika ili Madaktari Bingwa hao waweze kutekeleza majukumu yao ipasavo.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum M. Kijuu mara baada ya kukagua zoezi hilo la Madaktari Bingwa wakiwahudumia wagonjwa alisema kuwa zoezi hilo linatakiwa kuwa endelevu ili wananchi waweze kuhudumiwa kwa gharama ndogo na uhuhitaji wa wananchi ni mkubwa sana.
“Zoezi hili linatakiwa kwenda mpaka katika ngazi ya Halmashauri za Wilaya kwasababu kuna wananchi wengi ambao hawakupata fursa ya kufika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera na wana matatizo makubwa kama tulivyoona hapa.” Alisistiza Mkuu wa Mkoa Kijuu.
Naye Jovinus Rweikiza kutoka katika Kijiji cha Kasharu Bukoba Vijiji aliyefanyiwa upasuaji wa tezidume na Madaktari Bingwa hao akiwa wodini alitoa ushuhuda jinsi alivyokuwa amehangaika katika Hospitali mbalimbali ili aweze kupata huduma na kupewa rufaa za kwenda Hospitali ya Rufaa ya Bugando lakini ilikuwa inashindikana kutokana na gharama kubwa za matibabu hayo.
Serikali ya Mkoa wa Kagera inatoa rai kwa wananchi waliokuwa wamejiandikisha na kulipa fedha zao ili kuonana na Madaktari bingwa lakini hawakufanikiwa kuonana nao kutokana na wingi wa wagonjwa na muda wao kuwa mfupi, zoezi hilo litakapofanyika tena watapewa kipaumbele na kupewa huduma hiyo bila kulipia tena shilingi 5000 za kujiandikisha kwani tayari mafaili yao yapo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa