- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti azindua rasmi msimu wa Kahawa wa mwaka 2020/2021 ikiwa ni pamoja na kutangaza bei ya malipo ya awali shilingi 1200 kila kilo ya kahawa ya maganda kwa Vyama Vikuu vya Ushirika vya KCU 1990 Limited, KDCU Limited na Ngara Farmers.
Mkuu wa Mkoa Gaguti akitangaza ufunguzi wa msimu katika Chama cha Msingi cha Mabira Wilayani Kyerwa Juni 9, 2020 alisema kuwa jukumu kuu la Serikali ni kuhakikisha mkulima analindwa haki zake asipunjwe katika bei pia muda wa kupata malipo yake uwe mfupi kutoka wiki moja hadi masaa 48 tangu mkulima kufikisha kahawa yake katika Chama cha Msingi.
Mkuu wa Mkoa Gaguti alitumia fursa hiyo kurudia kauli yake kuwa kama kuna mfanyabaiashara yeyote ambaye yupo tayari kununua kahawa kwa wakulima kwa bei nzuri ajitokeze na kutangaza bei yake ili akapatiwe kahawa. “Kufikia tarehe 8.06.2020 tumepokea maombi ya wafanyabiashara wanane na kati ya hao wawili tu waliwasilisha maombi kwa barua na mmoja ndiye aliomba kununua kahawa kwa shilingi 1100 tu.” Alieleza Mkuu wa Mkoa Gaguti.
Mkuu huyo wa Mkoa pia alitoa rai kwa wakulima kuhakikisha wanatunza ubora wa kahawa yao kabla ya kuipeleka katika Vyama vya Msingi ili kuhakikisha kahawa kutoka Mkoani Kagera inafika kwenye soko ikiwa na ubora unaotakiwa ambapo katika msimu huu 2020/2021 zinatarajiwa kukusanywa takribani kilo milioni 60 juu ya kiasi cha msimu uliopita ambapo zilikusanywa kilo milioni 52.
Naye Mtendaji Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) Bw. Japhet Justine katika hafla hiyo ya ufunguzi wa msimu wa kahawa mwaka 2020/2021 alisema kuwa Vyama Vikuu vya Ushirika Mkoani Kagera vimekuwa viaminifu tangu mwaka 2018 benki ya TADB ilipoanza kuvipa mkopo ambapo msimu wa mwaka 2018 Benki hiyo ilitoa bilioni 30 na zililipwa zote, msimu 2019 Benki ilitoa bilioni 23 na zote zililipwa.
“Aidha, msimu huu wa 2020/2021 tayari tumeweka shilingi bilioni 7.7 katika akaunti za Vyama Vikuu vya KDCU Limited na KCU 1990 Limited kwaajili ya kukusanya kahawa ya wakulima na bila kuchelewesha malipo yao. Ndiyo maana baada ya kuona uaminifu wa vyama hivyo vikuu tumeamua kupunguza riba kutoka asilimia 12 na mwaka huu tunatoa mkopo kwa asilimia tisa tu (9%).” Alifafanua Bw. Japhet
Kuanzia Juni 9, 2020 wakulima wa zao la kahawa Mkoani Kagera wanahamasishwa kuanza kukusanya kahawa katika Vyama vyao vya Msingi na fedha ya malipo ya awali ipo tayari kwaajili ya kuwalipa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa