- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Maagizo Sita ya Mkuu Wa Mkoa wa Kagera Kuurudisha Mkoa Katika Enzi za Nshomile
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum M. Kijuu atoa maagizo makuu sita kuhakikisha kiwango cha Elimu kinaboreka zaidi na kuufanya mkoa huo unaongoza tena katika Sekta ya Elimu kama ulivyofahamika hapo awali ambapo uliitwa Mkoa wa “Nshomile” (Mkoa wa wasomi).
Maagizo hayo yalitolewa na Mhe. Kijuu katika kikao cha Wadau cha nusu mwaka cha kutathmini mwenendo wa Elimu Mkoani Kagera kilichofanyika Wilayani Muleba Juni 1, 2018 wakati matatizo makubwa yanayoikwamisha elimu ni pamoja na utoro wa wanafunzi na mimba shuleni.
Katika kikao hicho Afisa Elimu Mkoa Bw. Aloyce Kamamba alitoa takwimu za mimba shuleni kwa miaka mitano kuanzia 2014 hadi mwaka huu 2018 ambapo jumla ya wananfunzi waliopata mimba kwa kipindi hicho ni 231. Wanafunzi 41 Shule za Msingi na wanafunzi 190 Shule za Sekondari.
Aidha, Wadau wa Elimu katika kikao hicho walibainisha kuwa pamoja na sababu nyinginezo zinazowafanya wanafunzi wawe watoro shuleni lakini pia kuna tatizo la umbali kwa wanafunzi hao jambo linalowafanya wasafiri mwendo mrefu kuitafuta elimu mbali na makazi yao.
Baada ya kujadili kwa kina Mhe. Kijuu alitoa Maagizo Makuu sita ili kuhakikisha changamoto zote zinatatuliwa mara moja. Agizo la kwanza, Wakuu wa Wilaya kwa kushirikiana na Vyombo vya Ulinzi na Usalama wadhibiti utoro wa wanafunzi shuleni kwa kila Wilaya na Kuchukua hatua kwa wanafunzi watoro.
Pili, Wakuu wa Wilaya kwa kushirikiana na Wazazi waweke mpango madhubuti wa wanafunzi kupata chakula au uji shuleni ili waweze kumudu vyema masomo yao wakiwa wameshiba. Tatu, Wakuu wa Wilaya kwa kushirikisha wazazi na wadau wa Elimu kwenye Wilaya zao wajenge mabweni katika Shule za Sekondari ili wanafunzi wa kike waishi karibu na shule na kupunguza vishawishi njiani vinavyowafanya wapate mimba.
Nne, Vikao vya Wadau wa Elimu vifanyike kila Wilaya ili kujadili changamoto mbalimbali zinazoitatiza Sekta ya Elimu na utatuzi wa changamoto hizo ziwasilishwe kwenye kikao cha Wadau wa Elimu cha Mkoa. Tano, Madarasa ya Mitihani (Darasa la Nne na Saba Shule za Msingi, Kidato cha Pili na Nne kwa Sekondari) yafanye mitihani ya mazoezi kila siku asubuhi ili wanafunzi wauzoee mtihani.
Mwisho, Mkuu Mkuu wa Mkoa Mhe. Kijuu alisisitiza kila Wilaya kufanya vikao vya tathmini vya Wadau wa Elimu ili kuhakikisha wanafunzi wanafanya vizuri katika masomo yao na Mkoa wetu wa Kagera kurudi katika enzi zake za Nshomile.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa