- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Wadau Mkoani Kagera Waweka Mikakati ya Kutoa Chanjo Mpya ya Saratani ya Mlango wa Kizazi Kwa Wasichana Waliotimiza Umri wa Miaka 14
Wadau wa wa Chanjo Mkoani Kagera wafanya kikiao cha kujadili namna bora ya kuanzisha na kutekeleza kwa ufanisi chanjo mpya ya Saratani ya Mlango wa Kizazi kwa wasichana wenye umri miaka 14 ambapo mkoa unatarajia kuchanja jumala ya wasichana 35,917 katika vituo vya kutolea huduma za Afya 1,182.
Akifungua kikao hicho Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Mhe. Deodatus Kinawilo kwaniaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera aliwasisitiza wajumbe wa kikao kuhakikisha wanawahamasisha wananchi hasa wazazi kuwaruhusu watoto wao wasichana wenye umri wa miaka 14 kupata chanjo hiyo ambayo ni muhimu sana kwao na inatolewa bure bila malipo yoyote.
Mkuu wa Mkoa alisema kuwa Saratani ya Mlango wa Kizazi ni ugonjwa wa kwanza Tanzania unaowaua akinamama wengi ukifuatiwa na Saratani ya Matiti, ambapo aliwasisitiza wajumbe wa kikao kuhakikisha wanawahamasisha wazazi katika maeneo yao ili watoto wao wapate chanjo hiyo na kupunguza vifo kwa akina mama hapo mbeleni.
“Serikali ya mkoa imejipanga vizuri katika kutoa chanjo ya Saratani ya Mlango wa Kizazi kwa wasichana 35,917 katika mkoa wetu. Aidha, chanjo hiyo itatolewa katika vituo 1,182 vya kutolea huduma za afya vya Serikali na visivyokuwa vya Serikali pamoja na baadhi ya shule zitakazokuwa zimeainishwa,” Alitoa Msisitizo Mhe. Kinawilo.
Naye Dk.Siliacus Mtabuzi mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) akitoa salaam za Shirika hilo aliupongeza Mkoa wa Kagera kwa kufanya vizuri katika chanjo mbalimbali na kusema kuwa ni matarajio yake kuwa katika Chanjo hii mpya ya Kizazi cha Saratani ya Mlango wa Kizazi kwa wasichana wenye umri wa miaka 24 Mkoa wa Kagera utafanya vizuri zaidi kwa kuwafikia walengwa wote.
Katika hatua nyingine Dk. Mtabuzi alisema kuwa Shirika la Afya Duniani (WHO) kama mdau Mkuu wa Afya litaendelea kushirikiana kwa karibu sana na Mkoa wa Kagera ili kuhakikisha lengo la mkoa linafikiwa na wasichana wenye umri wa miaka 14 ambao ni akinamama wa kesho wasidhurike na Saratani ya Mlango wa Kizazi.
Mganaga Mkuu wa Mkoa Dk. Thomas Rutachunzibwa alifafanua namna chanjo hiyo itakvyotolewa katika Mkoa wa Kagera kwa kusema kuwa chanjo itaanza kutolewa tarehe 23 Aprili, 2018 na lengo likiwa ni kuwafikia wasichana 35,917 waliotimiza miaka 14 ambao walizaliwa kipindi cha Januari hadi Aprili 2004 na baada ya hapo zoezi litakuwa endelevu kwa wasichana watakaokuwa wanatimiza miaka 14 kila mwezi watakuwa wanapewa chanjo hiyo.
Kwa niaba ya Wakuu wa Wilaya Mkuu wa Wilaya ya Muleba Mhandisi Richard Luyango alitoa rai kwa wananchi ambao watajaribu kupotosha utoaji wa chanjo hiyo kuwa Kamati za Ulinzi na Usalaama zitamshughulikia kwa kuwachukulia hatua kali za kisheria mahala popote atakapokuwa.
Dalili za ugonjwa wa Saratani ya Mlango wa Kizazi ni kuishiwa damu, figo kushindwa kufanya kazi, kuvimba miguu, kutokwa na usaha wa rangi ya kahawia katika sehemu za siri za mwanamke. Aidha, visababishi vya ugonjwa huo ni kuanza mapenzi katika umri mdogo, kuwa na wapenzi wengi, na kuvuta sigara.
Ili kujikinga na ugonjwa wa Saratani ya Mlango wa Kizazi ni muhimu sana wasichana wakazingatia kutojihusisha na visababishi vilivyotajwa hapao juu. Pia Katika Mkoa wa Kagera kuna vituo vipatavyo 56 vinavyohusika na uchunguzi wa awali wa ugonjwa wa Saratani ya Mlango wa Kizazi ambapo mkoa unatoa wito kwaakina mama kuwahi mapema katika vituo hivyo pale wanapohisi dalili hizo ili kufanyiwa uchunguzi mapema.
Kikao cha wadau wa chanjo Mkoani Kagera kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera Aprili 18, 2018 kiliwahusisha Wakuu wa Wilaya, Wenyeviti wa Halmashauri za Wilaya, Waganga Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri, Maafisa Elimu wa Wilaya, Wadau wa Maendeleo wa Afya wa Mkoa wa Kagera, Wataalamu mbalimbali kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa na na Wataalamu wa Afya kutoka katika Halmashauri za Wilaya.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa