- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Waziri Ndalichako Akabidhiwa na Majengo na Shule na Unicef Awaagiza TBA Kulipa Madeni na Kumaliza Mradi wa Ihungo Sekondari
Katika Siku yake ya pili Mkoani Kagera Waziri Ndalichako alipokea majengo yaliyojengwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la UNICEF katika Shule ya Msingi Mgeza Mseto ambapo pia alikabidhi majengo hayo kwa Mkuu wa mkoa wa Kagera Mhe. Kijuu naye pia aliyakabidhi majengo hayo kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba.
Katika hafla hiyo fupi Prof. Ndalichako aliwashukuru UNICEF kwa kuitikia wito wake baada ya Tetemeko lililotokea Septemba 10, 2016 ambapo aliwaomba kutoa msaada katika Sekta ya Elimu kwani miundombinu mingi ilikuwa imeadhirika, na UNICEF walikubali kutoa milioni 700 kwaajili ya Shule ya Msingi Mugeza Mseto.
UNICEF imejenga Madarasa 3, Jengo 1 la kuwapumzisha wanafunzi watakaokuwa wanaumwa, Mabweni 4 yenye uwezo wa kubeba wanafunzi 190, Vyoo 2. Pia wametekeleza mradi wa maji wenye thamani ya milioni 107 na kujenga matundu ya vyoo yenye thamani ya milioni 500 katika shule mbalimbali ndani ya Manispaa ya Bukoba.
Waziri Ndalichako pia aliwashukuru wadau wengine ambao walichangia katika Shule ya Msingi Mgeza Mseto. Wadau hao ni Rotary Club waliotoa milioni 80 kwaajili ya kununulia magodoro, makabati na mashuka kwa ajili ya watoto wenye ulemavu ambao wanalala katika mabweni yaliyojengwa na UNICEF.
Bi Cecilia Baldeh Mwakilishi wa UNICEF anayeshughulikia masuala ya elimu kwa Watoto aliyemwakilisha Mwakilishi Mkazi wa UNICEF Tanzania akiongea na wanafunzi na wananchi waliohudhuria katika hafla hiyo fupi alisema kuwa UNICEF iliguswa na uhuhitaji wa shule hiyo baada ya Tetemeko kutokea mwaka 2016 na ndiyo maana waliamua kutoa fedha ili kupunguza changamoto katika shule hiyo yenye mahitaji maalum.
Pia Bi Cecilia alisema kuwa anatambua kuwa bado kuna changamoto katika shule ambapo hakuna njia za kutembelea (walka way), usafiri wa wanafunzi, nyumba za watumishi wanaowalea watoto, uzio na vifaa vya michezo ambapo alitoa wito kwa mashirika ya Kimataifa kuguswa kuchangia ili watoto hao wenye uhuhitaji maalum waishi kwenye mazingira bora zaidi.
Shule ya Msingi Mgeza Mseto ilianza mwaka 1950 ikiwa Middle School na baadae ilibadilishwa kuwa shule watoto wenye mahitaji Maalum miaka ya 1960 katika shule hiyo kuna watoto wenye mahitaji maalum 150. Manispaa ya Bukoba inazo Shule zenye mahitaji maalum 3, Shule ya Msingi Tumaini, Shule ya Msingi Mgeza Viziwi na Shule ya Msingi Mgeza Mseto.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera aliwashukuru UNICEF pamoja na Waziri Ndalichako kwa ufadhili wao wa kuhakikisha miundombinu ya shule hiyo inaimarishwa na kuonesha moyo wa kusaidia mara baada ya Tetemeko kutokea mwaka 2016 ambapo alisema kuwa wananchi wa Kagera walifarijika na wataendelea kufarijika kwa kuona miundombinu ya shule zao inarejeshwa na inaimarishwa zaidi kuliko hata mwanzo.
Ihungo Sekondari, Mara baada ya Hafla ya Makabidhiano Shule ya Msingi Mugeza Mseto Waziri Ndalichako alitembelea Shule ya Sekondari Ihungo kuona maendeleo ya ujezi wa shule hiyo ambapo aliridhishwa sana na kiwango cha ujenzi wa shule hiyo na kuwapongeza wajenzi Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kwa kujenga shule hiyo kwa viwango vya hali ya juu sana.
Pamoja na pongezi hizo Waziri Ndalichako aliwataka TBA kuhakikisha wanakamilisha ujenzi huo mara moja ili wanafunzi waweze kurejea katika shule yao na kuendelea na masomo yao. Pia Waziri Ndalichako alisema kuwa Wizara yake tayari imetoa bilioni 9.13 kati ya bilioni 10.48 fedha za kutekeleza mradi mzima wa Ihungo Sekondari.
Waziri Ndalichako alisema hayo baada ya kupokea taarifa ya Meneja wa TBA Mkoa wa Kagera Mhandisi Salum Chanzi kuhusu mradi huo na kusikia kuwa kuna wazabuni , vibarua na mafundi wanaodai fedha zao baada ya kutoa huduma za vifaa mbalimbali vya ujenzi na huduma katika ujenzi huo wa Ihungo.
Wizara yangu tayari imetoa kiasi kikubwa cha fedha bilioni 9.13 na tumebaki tunadaiwa milioni 715 tu na fedha iliyobaki ni asilimia 5% itakayolipwa baada ya kujihakikishia kuwa kila kitu kimekamilika. Nawataka TBA kumaliza mradi pia kuhakikisha wanawalipa wanaowadai na siyo mapaka wamalize mradi kwani fedha wanayo wao, Alisistiza Prof. Ndalichako.
Shule Sekondari Nyakato, Waziri Ndalichako pia alipata wasaa wa kutembelea Shule ya Sekondari Nyakato kuona maendeleo ya ujenzi wa shule hiyo ambapo mjenzi ni SUMA JKT na ujenzi umefikia asilimia 60% kwa sasa baada ya kuanza Septemba 21, 2017 na unatarajia kukamilika Septemba 20, 2018.
Waziri Ndalichako aliwapongeza SUMA JKT kwa kujenga majengo ya shule hiyo kwa viwango lakini pia kwa kwenda na muda ambao ujenzi unatarajia kukamilika. Ujenzi wa Shule ya Sekondari Nyakato utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 2.2 Ikumbukwe kuwa Shule za Sekondari Ihungo na Nykato ziliathiriwa vibaya na Tetemeko la Ardhi mwaka 2016 na zinajengwa upya na Serikali.
Waziri Ndalichako pia alizitembelea Shule za Sekondari Omumwani Rugambwa na kuongea na wanafunzi na uongozi wa shule hizo huku akisistiza wanafunzi kuongeza bidii katika masomo yao.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa