- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Rais Magufuli Azindua Rasmi Barabara ya Kagoma Rusahunga Mkoani Kagera
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuri katika siku yake ya kwanza ziarani Mkoani Kagera azindua rasmi barabara ya Kagoma Rusahunga yenye Kilometa 154 ambayo imejengwa na kukamilika kwa kutumia fedha za ndani bila wafadhili ambapo jumla ya shilingi bilioni 190.4 zimetumika.
Akiongea na wananchi kabla ya uzinduzi wa barabara ya Kagoma Rusahunga Wilayani Biharamulo Rais Magufuli alisema barabara hiyo ilizinduliwa mwaka 2013 na Rais Jakaya Kikwete lakini wakati yeye akiwa Waziri wa Ujenzi na Serikali iliamua kujenga barabara hiyo kwa fedha zake za ndani baada ya miaka ya 1990 kumfukuza Mkandarasi ambaye hakukidhi viwango na Kupelekea Benki ya Maendeleo ya Afrika kujiondoa katika ufadhili wa barabara hiyo baada ya Mkandarasi kufukuzwa.
Rais Magufuli aliwapongeza wananchi kwa kuitikia kulipa kodi na kusema kuwa hayo ndiyo matunda ya ulipajia kodi. “Kodi mnazolipa wananchi zinajenga barabara kama hizi ambazo zinafungua fursa za kukuza uchumi kwa wananchi na ndiyo maana nimekuwa nikisistiza sana wananchi kulipa kodi kwa hiari ili Serikali iweze kuwaletea maendeleo.” Alisistiza Rais Magufuli.
Ulipaji wa Kodi kwa Mashine za Kielekroniki
Rais Magufuli ametoa siku 14 kwa wamiliki wa vituo vya mafuta nchini kuhakikisha wanafunga Mashine za Kielekroniki (EFD) katika vituo vyao, aidha, mfanyabiashara yeyote atakaye kiuka agizo hilo Waziri wa Fedha na Waziri wa Viwanda wameagizwa kuchukua hatua za kuvifungia vituo hivyo mara moja na ikiwezekana visifunguliwe tena.
“Katika nchi hii tumekuwa tukiwatoza sana kodi wananchi wanyonge pamoja na wafanyakazi tu lakini wafanyabiashara wamekuwa wakifanya biashara bila kulipa kodi na kupata faida kubwa wakati wale wanaotakiwa kutozwa kodi tunawaacha tu. Jambo hili haliwezi kuendelea katika Serikali ya Awamu ya Tano.” Alikemea Rais Magufuli
Kodi za Kero kwa Wakulima
Rais akiwahutubia wananchi wa Wilaya ya Biharamulo aliwaambia kuwa Serikali yake imeamua kuondoa kodi za kero kwa wananchi wanaojishughulisha na kilimo ambapo tozo zaidi ya 80 zimefutwa na mkulima anayesafirsha mazao yake yasiyozidi tani moja kutoka Halimashauri ya wilaya moja kwenda nyingine hatakiwi kubugudhiwa na aina yoyote ya ushuru.
Aidha, Rais Magufuli alisema kuwa Serikali imeamua kufuta kodi za kero kwa zao la kahawa ambao aliwaagiza Mkuu wa Mkoa na Wakuu wa Wilaya kusimamia wananchi wasibugudhiwe tena na kodi zenye kero. Katika mifugo Rais Magufuli alisema kuwa kwenye minada kumekuwa utozaji wa ushuru wa hovyo hadi ushuru wa kwato ambapo aliagiza kuwa mifugo isiyofikia idadi ya mitano haitakiwi kutozwa ushuru.
Kuhusu Operesheni ya Mifugo Kagera
Rais magufuli aliwaambia wananchi kuwa operesheni iliyofanyika Mkoani Kagera kuondoa Mifugo katika Mapori ya Akiba, Vyanzo vya Maji na Misitu ya hifadhi aliagiza yeye Rais ifanyike kutokana na wafugaji kuvamia maeneo hayo ya hifadhi na kufanya uharibifu mkubwa hasa katika Mapori ya Akiba ambapo wanyamapori walikuwa wametoweka kabisa.
“Serikali haiwezi kuvumilia vitendo hivyo, wafugaji mnatakiwa kupunguza mifugo yenu kwa kuivuna na kufuga kisasa, hata mimi juzi nimevuna ng’ombe wangu na kuuza kwasababu nimeona siwezi tena kuwafuga wote. Kwanini nyinyi wafugaji msiwavune hao ng’ombe wenu mkajenga na nyumba? Mnawakaribisha wafugaji kutoka nje lakini kwao wanatunza mazingira yao, hatuwezi kuvumilia kadhia hiyo.” Aliwaonya wafugaji Rais Magufuli.
Rais Magufuli alimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Kagera na Wakuu wa Wilaya kwa kutekeleza na kusimamia vizuri zoezi la Operesheni Ondoa Mifugo Kagera na kuwataka kuendelea kusimamia kwa karibu mifugo isirudi katika maeneo ya hifadhi pia aliagiza mtumishi wa idara ya Wanyamapori aliyekuwa amesimamishwa kazi kurudishwa kazini mara moja na kupandishwa cheo kwani alikuwa anatekeleza majukumu yake ipasavyo.
Wachimbaji wadogo
Rais magufuli aliwaambia wananchi kuwa wachimbaji wadogo wamekuwa wakinyanyaswa mara baada ya kugundua sehemu zenye madini kama dhahabu ambapo aliagiza Wizara ya Nishati na Madini kuhakikisha wachimbaji wanapewa leseni katika maeneo waliyoyagundua wao na kuacha kuwanyanyasa kwa kuwafukuza na kuwapa wawekezaji kutoka nje.
Afya na Elimu
Rais Magufuli aliwaambia wananchi kuwa Serikali yake sasa imeongeza bajeti afya kutoka bilioni 31 hadi bilioni 250 na Serikali imeanza kununua dawa yenyewe ambapo bei za dawa zinatarajia kushuka zaidi kwani Serikali itakuwa inaziuza yenyewe kwa bei ndogo. Aidha, alisema Serikali inaendelea kutekeleza Elimu Bure kwa wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari.
Katika hatua nyingine Rais Magufuli alitoa siku 10 kwa Mkandarasi anayetekeleza mradi wa Maji Biharamulo na Msimamizi wake Mamlaka ya Maji Saji na Maji Taka Bukoba (BUWASA) kuhakikisha maji yanaanza kutoka katika mji wa Biharamulo. Rais Magufuli ataendelea na ziara yake katika Wilaya ya Ngara tarehe 20 Julai, 2017 ambapo anatarajia kuongea na wananchi katika mkutano wa hadhara
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa