- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Rais Magufuli na Museveni Wazindua Rasmi Kituo Cha Forodha Cha Huduma Kwa Pamoja Katika Mpaka wa Mtukula Kagera
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Uganda Yoweri Kaguta Museveni wazindua rasmi Kituo cha Forodha cha Huduma kwa Pamoja (OSBP) pande zote mbili Mtukula mpakani mwa Tanzania na Uganda leo Novemba 9, 2017.
Mara baada ya kupokelewa na mwenyeji wake Rais Yoweri Kaguta Museveni na kupigiwa mizinga 21 na kuzindua Kituo cha Forodha cha Huduma kwa Pamoja upande wa Tanzania Rais Magufuli akiongea na wananchi katika mpaka wa Mtukula alisema kuwa lengo la kituo hicho ni kupunguza muda mwingi uliokuwa unapotezwa wakati wasafiri wakivuka mpaka kutoka nchi moja kwenda nchi nyingine.
Rais Magufuli alisema kuwa baada ya vituo hivyo kujengwa faida nyingi zimepatikana ambapo malori 400 hadi 700 yanayobeba chakula cha msaada kuelekea katika nchi ya Sudani Kusini hupita mpaka wa Mtukula kwa mwezi kwasababu taratibu za kuvuka mpaka zimerahisishwa zaidi.
“Kabla ya vituo hivi kujengwa abiria alikuwa anachukua dakika 10 hadi 30 kuvuka lakini sasa abiria mmoja anatumia dakika 2 hadi 3 kuvuka, kabla ya vituo hivi lori moja lilikuwa linatumia siku nzima kuvuka lakini kwasasa lori moja linatumia dakika 30 hadi saa moja,” alisistiza Rais magufuli.
Pia Rais Magufuli alifafanua kuwa Kituo cha Forodha cha Huduma kwa Pamoja(OSBP) kimepunguza rushwa iliyokuwa kubwa mpakani na kuikosesha Serikali ya Tanzania Mapato lakini kwasasa baada ya kituo hicho kuanza kufanya kazi tangu Agosti 2015 mapato yameongezeka mfano nchi ya Uganda mapato yameongezeka kwa asilimia 110%
Vilevile Rais Magufuli alisema kituo hicho kimeongeza Taasisi za Serikali zinazofanya kazi kwa pamoja kutoka Taasisi 6 hadi 16, pia fedha zinazokusanywa na TRA pamoja na Uhamiaji zinaingia mojakwamoja katika mfuko mkuu wa Serikali ikiwa ni pamoja na taasisi zilizokuwa hazikusanyi mapato mfano TBS kwasasa wanankusanya mapato na tayari wamekusanya milioni 380.5 toka Novemba 2015 hadi sasa.
Mwisho Rais Magufuli alitoa shukrani kwa Serikali ya Uingereza waliotoa fedha za kutekeleza mradi wa ujenzi wa vituo hivyo viwili kupitia Kampuni ya Trade Mark East Afrika, na ujenzi huo uligharimu shilingi bilioni 7.16 Pia alimshukuru Rais Mseveni kwa kukubali bomba la mafuta lenye urefu wa kilometa 1,415 kupita Tanzania na kuwataka Watanzania kuchangamkia fursa ya ajira katika ujenzi wa bomba hilo.
Katika Hatua nyingine Rais wa Jamhuri ya Uganda Yoweli Kaguta Museveni alimkaribisha Rais Magufuli na kumpongeza kwa kukubali mwaliko wake wa kwenda kuzindua bomba la Mafuta nchini Uganda pia na kukubali kushirikiana katika masuala mbalimbali ya kukuza uchumi wan chi mbili.
Rais Museveni alisema kuwa yeye kuja Tanzania kufanya uzinduzi wa Kituo cha Forodha cha Huduma kwa Pamoja(OSBP) ni hija ya ukombozi kwake. Kwani alisema kuwa hapo mwanzo alikuwa anakuja kwa siri ili kupanga mipango ya ukombozi wa nchi yake lakini sasa anakuja kuzindua miradi ya maendeleo wakati nchi yake ikiwa imekombolewa.
“Uwepo wa mpaka wa Mtukula na Vituo vya Forodha vya kutolea Huduma kwa Pamoja (OSBP) ni Ustawi wa Sekta (‘akabodo’ kwa kiganda) za Uchumi ambapo ili wananchi watajirike na kupata ajira lazima Sekta nne zizingatiwe moja ikiwa ni Kilimo na kufuga kisasa, Pili ni Uchumi wa Viwanda, Tatu ni Huduma za jamii, na Nne ni Tehama. Hapo wananchi watapata ajira na kutajirika,” Alifafanua Rais Museveni.
Mwisho Rais Museveni alimshukuru Rais Magufuli kwa kukubali kuwapatia nishati ya umeme wananchi wa eneo la Nyangoma lililopo Wilayani Missenyi na kukwamua mradi wa umeme wa Mulongo Wilayani Kyerwa ambapo mradi huo sasa unajengwa ili kuanza kuzalisha umeme.
Rais Magufuli na Rais Museveni wameelekea nchini Uganda kwenye sherehe za uzinduzi wa Bomba la mafuta kutoka Hoima Nchini Uganda hadi Tanga Tanzania. Aidha Rais Magufuli amehitimisha Ziara yake ya kikazi ya siku nne Mkoani Kagera leo Novemba 9, 2017
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa