- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Rais Magufuli Azindua Rasmi Uwanja Wandege wa Bukoba na Kuagiza Fedha za Fidia Omukajunguti Zihamishiwe Katika Uwanja Huo
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli katika siku yake ya kwanza ziarani Mkoani Kagera azindua rasmi Uwanja wa Ndege wa Bukoba na kumuagiza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbalawa kuhamisha shilingi Bilioni 9 za kulipa fidia kwa wananchi ili kupisha ujenzi wa uwanja mpya wa Omukajunguti Wilayani Missenyi.
Rais Magufuli akiwahutubia wananchi katika Uwanja wa Ndege wa Bukoba aliouzindua leo Novemba 6, 2017 alisema kuwa ili kuutendea haki uwanja huo wenye urefu wa kilometa 1.5 na upana wa meta 30 na jengo zuri la abiria ambalo ni la tatu ukiacha majengo ya abiria ya Dar es Salaam na Kilimanjaro, Rais magufuli alisistiza kuwa lazima uwanja huo upanuliwe ili wananchi wa Kagera wafanye biashara.
“Kujenga uwanja mmoja wa ndege ni gharama kubwa mno ni mabilioni fedha, ili Mkoa huu ukue kiuchumi lazima tuupanue huu ambao umekamilika kwa kiwango kikubwa ili samaki zinazosindikwa hapa Bukoba zipakiwe hapa pamoja na ndizi na mazao mengine vilevile na watalii wapiti hapa kwenda Burigi kutalii kuona wanyama na utalii uliopo Kagera.” Alifafanua Rais Magufuli.
Rais Magufuri akifafanua zaidi alisema fedha zilizotengwa kwenye bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano mwaka huu wa fedha 2017/2018 shilingi bilioni 9 kwa ajili ya fidia za wananchi Omukajunguti zinatosha kufanya upanuzi wa uwanja huo na kama zikipungua yeye ataongeza ili uwanja upanuliwe na ndege kubwa za mizigo ziweze kutua na kupakia mizigo uwanjani hapo kuliko kuanza ujenzi wa uwanja mpya ambao matumaini yake ya kukamilika ni madogo sana.
Aidha, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini Bw. Richard Muyongera alisema kuwa Uwanja wa Ndege wa Bukoba umejengwa na kukamilika kwa jumla ya gharama ya shilingi bilioni 31.95 ambapo Serikali ya Tanzania ilichangia shilingi bilioni 6.35 na fedha zilizobaki zaidi ya Bilioni 25 zilitolewa na Benki ya Dunia kama mkopo nafuu.
Bw. Muyongera alisema ujenzi wa uwanja huo ulihusisha ukarabati na upanuzi wa barabara ya kurukia ndege kwa urefu wa kilometa 1.5 na upana wa meta 30, Ujenzi wa maegesho ya ndege ambapo ndege tatu zinaegeshwa kwa wakati mmoja, Ujenzi wa jengo la abiria lenye uwezo wa kuhudumia abiria 500,000 kwa mwaka.
Ambapo jengo hilo limefungwa mifumo ya kisasa ya kuhudumia mizigo, mfumo kamera za usalama, maegesho ya magari 67 kwa pamoja , kituo cha kufua umeme na kuhamisha Shule ya Msingi Tumaini ambayo imejengwa upya kwa gharama ya shilingi bilioni 2.6 na imejengwa kisasa zaidi ya ile ya awali.
Naye Mwakilishi wa wa Benki ya Dunia Bw. Andre Bald alisema Benki ya Dunia iliamua kufadhili ujenzi wa Uwanja wa Bukoba kwa manufaa ya wananchi wa Bukoba ambapo alisema kuwa Shule ya Msingi Tumaini ilikuwa inahudumia Elimu Maalum na yeye aliguswa na ndiyo maana Benki ya Dunia iliamua kugharamia ujenzi wa Shule mpya katika eneo la Mafumbo Manispaa ya Bukoba.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbalawa amewahasa wananchi wa Bukoba kuutunza Uwanja wa Ndege wa Bukoba na akayakaribisha Mashirika mengine ya Ndege kuanza safari zake Bukoba , kwasasa mashirika yanyofanya kazi uwanjani hapo ni Air Tanzania, Precision Air, na Auric Air.
Katika hatua nyingine Rais Magufuli amewahakikishia wananchi wa Bukoba kuwa tayari fedha za kununua meli mpya tayari zimepatikana na kutengwa ambapo tenda imeishatangazwa na Mkandarasi wa ujenzi wa meli mpya ni Nchi ya Korea Kusini na Mwezi Desemba 2017 au Januari 2018 Mkataba wa ujenzi wa meli mpya utasainiwa ili ujenzi uanze rasmi.
Pia Rais Magufuli aliwahakikishia wakulima wa zao la kahawa kuwa sasa zao hilo litapanda bei kwani tayari Serikali imefuta kodi 17 na sasa zao la kahawa linatakiwa kuwa na bei ya kuridhisha. Vilevile Rais Magufuli amewataka wananchi wa Kagera kuhakikisha wanatumia fursa ya Bomba la mafuta kutoka Uganda kujipatia ajira
Rais Magufuli ataendelea na ziara yake Mkoani Kagera Kesho Novemba 7, 2017 ambapo ataelekea Wilayani Karagwe kuzindua Barabara ya Kyaka Bugene na kuongea na wananchi wa Wilaya Karagwe.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa