- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Rais Magufuli Afanya Mazungumzo na Rais wa Burndi Nkurunziza na Kukubaliana Kufufua Fursa za Kiuchumi Kati ya Nchi Mbili
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli afufua rasmi mazungumzo ya Kiuchumi na Nchi ya Burundi baada ya kukuta na Rais wa Jamhuri ya Burundi Pierre Nkurunziza Wilayani Ngara Mkoani Kagera na kufanya naye mazungumzo ya kuanzisha ushirikiano wa kibiashara baina ya Tanzania na nchi ya Burundi.
Rais Dkt. Magufuli akiongea na wananchi baada ya kufanya mazungumzo na mgeni wake Rais Nkurunziza alisema mwaka 2013 yalifanyika mazungumzo kati ya nchi za Tanzania na Burundi ambapo Mawaziri wa fedha wa nchi hizo walikutanana na kuanzisha mazungumzo ya kibiashara kati ya nchi mbili ambapo kwasasa wamezungumza kufufua upya mazungumzo hayo ili kuanzisha ushirikiano wa kibiashara .
“Kwa takwimu za mwaka 2016 zinaonyesha kuwa biashara zilizokuwa zinafanyika kati ya Tanzania na Burundi zilikuwa zina thamani ya shilingi bilioni 116.5 ambazo biashara hizo ni kidogo sana ukilinganisha na watu milioni 50 Watanzania na watu zaidi ya milioni 12 Warundi, kwahiyo kuna haja ya kukuza na kuimarsha biashara kati ya nchi zetu mbili.” Alifafanua Rais Dkt. John Magufuli.
Aidha, Rais Dkt. Magufuli alimpongeza Rais Nkurunziza kwa juhudi zake za kuendelea kuimarisha amani na usalama na kuwataka Wakimbizi kutoka nchi ya Burundi kurudi kwao kuijenga nchi yao kwani tayari kuna amani na utulivu . Pia aliyakemea Mashirika ya kuwahudumia Wakimbizi kuacha kuwapotosha Wakimbizi hao kuwa kwao hakuna amani aidha, alisema kuwa tayari anajua kuwa Mashirika hayo ya Kimataifa yanatumia mwanya huo kuwatumia Wakimbizi kama Biashara.
Rais Dkt. Magufuli pia alimwagiza Waziri wa Mambo ya Ndani kuacha kutoa uraia kwa wakimbizi kuwa hicho kinaweza kuwa kivutio kwa Wakimbizi kuendelea kuingia nchini Tanzania hata kama kwao hakuna vita. Vilevile aliwataka Warundi kuishi kwa mshikamano kama Tanzania ambapo alisema kuwa hapo awali Tanzania ilikuwa na makabila 121 lakini kwa sasa kuna makabila 123 mawili yameongezeka ambao ni Wahutu na Watutsi wapatao 200,000 waliopewa uraia kuwa Watanzania.
Naye Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ya Tanzania Mwigulu Nchemba alipewa nafasi na Rais Dkt. Magufuli na kusema kuwa kwasasa Wakimbizi kutoka nchi ya Burundi waliopo Tanzania ni 247,000 na tayari kuna Wakaimbizi 150,000 waliondoka kwa hiari yao na tayari wengine 5000 wamejiandikisha kurudi kwao kwa hiari.
Rais wa Jamhuri ya Burundi Pierre Nkurunziza akiwasalimia wananchi wa Wilaya ya Ngara na Watanzania kwa ujumla aliishukuru nchi ya Tanzania kwa ushirikiano mkubwa pamoja na nchi yake ya Burundi. Pia alisema kuwa katika mazungumzo yake na Rais Dkt. Magufuli yamefungua mwanzo mpya wa fursa za kibiashara baina ya nchi mbili.
Vile vile Rais Nkurunziza alitoa wito kwa Watanzania kuanza kufanya biashara na nchi yake ya Burundi na alisema kuwa anaona kuwa hapo mbele mambo yatakuwa sawasawa kati ya nchi hizi mbili na watoto wa nchi hizo mbili watakuwa na mambo mazuri hapo mbeleni.
Aidha, Rais Nkurunziza alitoa wito kwa Wakimbizi Warundi walioko nchini Tanzania kurudi kwao Burundi kwenda kushirikiana kuijenga nchi yao kwani amani imerejea kwa sasa hakuna vita tena. “Nawaomba Warundi wenzangui walipo mrudi nyumbani ili tukaijenge nchi yetu na kukuza uchumi na tuweze kunufaika kwa pamoja na watoto wetu. Alisistiza Rais Pierre Nkurunziza.
Katika Hatua nyingine Rais Dkt. John Pombe Magufuli aliwaeleza wananchi wa Wilaya ya Ngara na taifa kwa ujumla kuwa Serikali yake inaendelea kuwaletea maendeleo katika Sekta mbalimbali, mfano Katika Afya Serikali tayari imenunua vitanda vyenye thamani ya Bilioni 33 na itavigawa katika Hospitali zote za Serikali nchini.
Aidha, Serikali imenunua vifaa vya mahabara na na kuvigawa katika shule 1900, na imetenga shilingi bilioni 483 kwaajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya Juu. Vilevile Serikali inatarajia kujenga upya barabara ya Nyanazi hadi Ngara ambayo ina mashimo mengi kwasasa na kujenga barabra ya Nyakahura Rulenge kilometa 92 kwa kiwango cha rami.
Katika Siku yake ya pili Rais Dkt. Magufuli Mkoani Kagera alimpokea kwa heshima zote za kitaifa Rais wa Jamhuri ya Burundi Pierre Nkurunziza katika uwanja mpira wa Lemela Wilayani Ngara majira ya saa 5:00 asubuhi na Rais Nkurunziza alipigiwa mizinga ya heshima 21 na kukagua Gwaride. Aidha, baada ya kukamilisha ziara yake na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Burundi Pierre Nkurunziza alirudi nchini Burundi.
Katika Mapokezi ya Rais wa Jamhuri ya Burundi Pierre Nkurunziza Rais Dkt. Magufuli aliambata na Mawaziri wa Wizara za Mambo ya Ndani Mwiguru Nchemba, Wizara ya Fedha Dk. Philip Mpango, Wizara ya Ulinzi Dkt. Hussein Mwinyi, Wizara ya Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbalawa, na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Naibu Wazi Dkt. Suzan Kolimba pamoja na Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama Kitaifa.
Rais Dkt. Magufuli amemaliza ziara yake ya siku mbili Mkoani Kagera na anatarajia kuelekea Mkoani Kigoma Juni 21, 2017 kuendelea na ziara yake ya kazi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa