- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Rais Magufuli Kuwasili Mkoani Kagera Novemba 6, 2017
Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Joseph Pombe Magufuli atarajia kufanya ziara Mkoani Kagera kuanzia tarehe 06 hadi 09 Novemba, 2017.
Dhumuni la ziara ya Mhe. Rais Magufuli ni kuwatembelea wananchi wa Mkoa wa Kagera pia kutembelea na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo Mkoani hapa. Vilevile Mhe. Rais Magufuli atapata fursa ya kuongea na wananchi kwenye Mkutano wa Hadhara Uwanja wa Ndege wa Bukoba.
Mhe. Rais Magufuli atawasili Mkoani Kagera tarehe 06.11.2017 siku ya Jumatatu mchana na atapokelewa na viongozi mbalimbali wa Mkoa. Aidha Mhe. Rais Magufuli ataanza ziara yake siku hiyo ya tarehe 06.11.2017 katika Manispaa ya Bukoba kwa kuzindua Uwanja wa Ndege wa Bukoba saa 08:00 mchana. Aidha, mara baada ya uzinduzi Mhe. Rais ataongea na wananchi katika Mkutano wa Hadhara.
Tarehe 07.11.2017 siku ya Jumanne Mhe. Rais Magufuli ataelekea Wilayani Karagwe katika eneo la Nyakahanga na kuzindua Barabara ya Kyaka Bugene majira ya 03:00 Asubuhi na mara baada ya uzinduzi huo Mhe. Rais atasalimia wananchi.
Vilevile Mhe. Rais Magufuli ataendelea na ziara yake Mkoani hapa tarehe 8.11.2017 siku ya Jumatano kwa kutembelea kiwanda cha Kagera Sukari Wilayani Missenyi ambapo atapata fursa ya kukagua mashamba ya miwa pia na kuongea na Wafanyakazi, Uongozi na Menejimenti ya Kiwanda hicho.
Mhe. Magufuli atahitimisha ziara yake Mkoani Kagera tarehe 9.11.2017 siku ya Alhamisi katika Wilaya ya Missenyi kwa kuzindua Kituo cha Pamoja cha Forodha katika eneo la Mtukula mpakani mwa Tanzania na Uganda akiwa na Rais wa Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Mseveni. Baada ya uzinduzi Ma-Rais wote watawasalimia wananchi.
Mkuu wa Mkoa wa Kgera Meja Jenerali Mstaafu Salum M. Kijuu anatoa wito kwa wananchi wote wa Mkoa wa Kagera kujitokeza kwa wingi kumpokea na kumshangilia Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sehemu zote atakazopita kuanzia Nyakabango Wilayani Muleba mpakani mwa Mkoa wa Geita na Kagera pia na maeneo yote yaliyotajwa atakapokuwa anatembelea, anazindua miradi ya maendeleo, na atakapokuwa anaongea na wananchi.
Pia Mhe. Kijuu anawasisitiza wananchi wote kudumisha utulivu, amani na mshikamano pamoja na upendo kama ilivyo kawaida na desturi ya wananchi wa Mkoa wa Kagera wakati wanapotembelewa na wageni hasa ugeni mkubwa kama wa Mhe. Rais.
Aidha, Mhe. Kijuu anawahakikishia wananchi wote kuwa Vyombo vya Ulinzi na Usalama vipo imara na vinaendelea na kazi yake ya kudumisha amani na utulivu. Pia anatoa rai kuwaasa wananchi wote kujiepusha na vitendo vyote vya uvunjifu wa amaniambapo anasema kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayethubutu kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa