- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Tangu Awamu ya Tano kuingia Madarakani mwaka 2015 Rais wa Jamuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Joseph Magufuli amekuwa akisisitiza Uchumi wa Viwanda ili nchi ya Tanzania ifikapo mwaka 2025 iwe na uchumi wa kati.
Katika kutekeleza Sera hiyo ya Serikali ya Awamu ya Tano ya Uchumi wa Viwanda Mkoa wa Kagera haujabaki nyuma unatekeleza kikamilifu Sera hiyo kwa kuanzisha, kujenga na kundesha viwanda vya aina mbalimbali lakini pia kuendelea na juhudi za kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na kuwakaribisha wawekezaji mbalimbali kuja Kagera kuwekeza katika viwanda vya aina mbalimbali.
Leo katika makala hii fupi mbali nakuujua Mkoa wa Kagera kuwa umejikita katika uchumi mkubwa wa viwanda vya Kahawa lakini pia Mkoa huo unafanya maajabu katika Nyanja ya viwanda vingine kikiwemo kiwanda cha kuchenjua madini ya bati kinachojulikana kwa jina la TANZAPLUS kilichopo Wilayani Kyerwa.
Kiwanda cha TANZAPLUS kilichopo Kijiji cha Kagenyi Kata ya Kyerwa Wilayani Kyerwa kimeleta mapinduzi makubwa ya uzalishaji wa madini ya bati hasa kwa kuongeza samani ya madini hayo yanayochimbwa katika Kata ya Kyerwa na kuuuzwa kwa bei stahiki lakini kuongeza ajira kwa wachimabaji wadogo kwa kuwa madini hayo sasa yana soko linaloaminika hapo hapo Wilayani Kyerwa.
Kwa miaka mingi madini ya bati yanayochimbwa Wilayani Kyerwa yalikuwa yakitoroshwa na kuuzwa katika nchi jiarani ya Rwanda tena kwa bei ndogo sana jambo ambalo lilikuwa likiinufaisha nchi hiyo wakati madini yanachimbwa hapa nchini katika Mkoa wetu wa Kagera.
Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa Bw. Rashid Mwaimu akitembelea kiwanda hicho kuonesha jinsi Wilaya ya Kyerwa inavyotekeleza Sera ya Tanzania ya Viwanda alisema kuwa TANZAPLUS imekuwa mkombozi sana kwa vijana ambao ni wachimbaji wadogo kujihusisha zaidi na uchimbaji wa madini ya bati kwani sasa wamepata soko ambapo wanauza madini yao wakiwa ndani ya nchi na madini hayo yanachenjuliwa Wilayani hapo kwa ajili ya kuuzwa nje ya nchi yakiwa tayari yameongezwa thamani.
“Tumekuwa tukinyonywa sana hasa katika Wilaya yetu ya Kyerwa madini haya ya bati yanachimbwa hapa lakini yalikuwa yakiuzwa nje ya nchi tena hapa kwetu walikuwa wananunua kilo moja shilingi 15,000/= hadi 18,000/= tu lakini madini hayo hayo yakivushwa tu mpaka na kupelekwa nchini Rwanda yanauzwa hadi shilingi 48,000/= kwa kilo moja unaweza kuona unyonyaji ulivyo tene bila kulipa kodi ya Serikali.” Alieleza Mkuu wa Wilaya Rashid Mwaimu.
Mwekezaji Mzalendo ambaye ni Mtanzania Bw. Salim Mhando amabye ndiye Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanda cha TANZAPLUS alisema kuwa pamoja na kuchenjua madini ya bati lakini kiwandani hapo lakini wameanza kutengeneza nyaya ambazo zinatumika katika matengenezo ya Kompyuta, Mashine za X ray, kutengeneza vipuli vya Tansfoma za kufua umeme, pia kutengenzea nyaya za kuyeyuesha katika uchomeleaji wa vifaa vya electronics (zijulikanazo kama risasi)
Bw. Salim alisema kuwa Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi sana kununua vifaa vinavyotengenezwa na madini ya bati kutoka nchi za nje lakini kwa kuanzisha kiwanda cha TANZAPLUS vifaa hivyo vitakuwa vinapatikana Mkoani Kagera Wilayani Kyerwa ambapo sasa wameanza majaribio ya kutengeneza vifaa hivyo na kuvipeleka katika majaribio kuona kama vitakidhi mahitaji.
Kuwepo kwa kiwanda cha TANZAPLUS Wilayani Kyerwa kutaongeza ajira kwa vijana lakini pia kubadilisha mtazamo wa wananchi wa Wilaya hiyo katika kunufaika na madini yanayochimbwa katika Wilaya yao pia Mkoa wa Kagera nao unakua kiuchumi kwa kuongeza ajira kwa vijana na kuzalisha bidhaa kutoka Kagera.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti akizungumzia Sera ya Tanzania ya Viwanda na Kagera ya Viwanda anasema kuwa Mkoa wa Kagera umepiga hatua kubwa katika viwanda ambapo hadi kufikia Mwezi Oktoba 2018 Mkoa ulikuwa na viwanda 502 ambapo kati hivyo viwanda vikubwa ni tisa (9), vya kati ni 16 na viwanda vidogo ni 477.
Aidha, Mkuu wa Mkoa Gaguti anasema kuwa Mkoa unaendelea na juhudi za kuwakaribisha wawekezaji wa ndani naje nchi kuja Kagera kuwekeza ambapo tayari uongozi umetenga maeneo ya uwekezaji na ujenzi wa viwanda yenye ukubwa wa Hekta 58,000 katika maeneo mbalimbali kupitia kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Unaweza kuona Mkoa wa Kagera unavyozidi kujipanga vyema kuimarisha uchumi wake na kutoa ajira kwa wananchi kupitia Kagera ya Viwanda. Msomaji wetu tutakuwa tukikuletea makala kama hizi za Uchumi wa Viwanda Mkoani ili uone Mkoa ulivyojidhatiti katika Viwanda. Je ni Kiwanda kipi unahisi tutakuletea na hutegemei kama kiwanda hicho kinaweza kuwa katika Mkoa wetu wa Kagera? Usikose kufuatilia.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa