- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Mkoa wa Kagera waanza kuchukua hatua za dhati za usimamizi wa rasilimali madini zinazopatikana mkoani humo kwa kuweka mfumo thabiti wa kuhakikisha kila mdau aliyeko kwenye mnyororo wa thamani ya madini na kuwajibika ipasavyo ili madini hayo yawanufaishe wananchi na kuinua pato la mkoa na taifa kwa ujumla.
Hatua zinazoendelea kuchukuliwa ni pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti kufanya ziara katika machimbo ya madini ya bati Nyaluzumbura Wilayani Kyerwa na kuzungumza na Wachimabaji Wadogo juu ya changamoto mbalimbali wanazokutana nazo katika uchimbaji na kufanya biashara ya madini.
Mkuu wa Mkoa Gaguti akieleza lengo la kutembelea machimbo hayo Februari 3, 2019 alisema kuwa baada ya kufanya kikao cha wadau wa madini cha Taifa chini ya Rais John Pombe Magufu Januari 22, 2019 Jijini Dar es Salaam iliazimiwa kuwa kila mkoa uhakikishe unasimamia kikamilifu rasilimali madini na kuondoa kero na vikwazo vyote vinavyopelekea madini kuuzwa kimagendo na nchi kukosa mapato.
Mkuu wa Mkoa Gaguti alitoa nafasi kwa Wachimbaji Wadogo wa Mdini ya Bati kumweleza changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo katika uchimbaji na biashara ya madini ya Bati. Wachimbaji hao wadogo walimweleza Mkuu wa Mkoa kuwa changamoto kubwa ni bei ya madini ya bati kuwa ndogo, Utoroshaji wa madini hayo na kuuuzwa nchi jirani, Mitaji midogo ya kununulia vifaa vya kisasa vya uchimbaji.
Mara baada ya kusikiliza changamoto hizo Mkuu wa Mkoa aliyeongozana na Kamati ya Ulinzi na Usalaama ya Mkoa aliwaeleza Wachimabji Wadogo kuwa changamoto hizo tayari mkoa umezitafutia ufumbuzi ambao kama wao watatoa ushirikiano zitaisha kwa muda mfupi na wataanza kuneemeka na uchimbaji wa madini hayo lakini pia mkoa utakuza pato lake aidha na taifa kwa ujumla.
“Tofauti na ilivyo sasa sisi Serikali ya Mkoa tumeamua kuanzisha mfumo sahihi katika sekta ya madini, tumeamua kuweka mfumo wenye utaratibu mzuri wa uchimbaji, pili mfumo wa kuyatunza madini ghafi ya bati baada ya kuchimbwa kabla ya kuuzwa, na mwisho ni mfumo sahihi wa kuuza mdini hayo na soko lake yakiwa yameongezewa thamani ndani ya Wilaya ya Kyerwa.” Alifafanua Mkuu wa Mkoa Gaguti.
Ili kuhakikisha Madini ya Bati hayatoroshwi na kuuzwa nchi jirani tayari Serikali imewapata wawekezaji wa kuongeza thamani madini ya bati ambapo tayari mmoja amejenga kiwanda cha kuongeza thamani madini hayo naye ni TANZAPLUS na kiwanda chake kipo Wilayani Kyerwa. Wa pili ni Africa Top Minerals Limited (ATM) ambaye anaendelea na mazungumzo na Serikali ili kuanza kuongeza thamani Madini ya Bati.
MAAGIZO
Mkuu wa Mkoa Gaguti alimwagiza Afisa Madini wa Mkoa wa Kagera Mhandisi Lucas Mlekwa kuhakikisha anaanza utekelezaji wa kuanzisha maghara ya kuhifadhi madini ghafi mara baada ya kuchimbwa, pili kuwasimamia wachimbaji wadogo kujiunga katika vikundi ili watambuliwe na kupatiwa mikopo. Tatu ni kuhakikisha madini yote yatakayochimbwa Kyerwa yaongozewe thamani Wilayani hapo na soko lake liwe humo.
Maagizo hayo yanatakiwa kuwa yametekelezwa ifikapo mwishoni mwa mwezi Februari 2019 ili Waziri wa Madini aweze kualikwa mwanzoni mwa Mwezi Machi 2019 kuzindua mfumo rasmi wa uchimbaji, uongezaji thamani na uuzaji wa Madini ya Bati Mkoani Kagera ambao utakuwa unawanufaisha wadau wote waliopo kwenye mnyororo wa thamani ya madini hayo.
Madini ya Bati Nyaluzumbura Wilayani Kyerwa yalianza kuchimbwa tangu mwaka 1924 na katika machimbo hayo kwa sasa yanachimbwa Madini ya Bati kwa wastani wa nusu tani (Kilo 500) kila mwezi na idadi ya Wachimbaji Wadogo katika mgodi huo ni 1,350.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa