- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Maadhimisho ya Wiki ya Maziwa Kitaifa Mkoani Kagera Yazinduliwa Rasmi na Naibu Waziri Ole Nasha Kyakailabwa Manispaa ya Bukoba
Maadhimisho ya Wiki ya Maziwa Kitaifa Mkoani Kagera yazinduliwa rasmi Mei 28, 2017 na Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Mhe. Tate William Ole Nasha katika Viwanja vya Kyakailabwa Manispaa ya Bukoba na kuzinduzia rasmi uhamasishaji wa unywaji wa Maziwa kwa wananchi wote ili kupunguza udumavu na kuongeza viinilishe muhimu mwilini. Kaulimbiu ikiwa ni “Kunywa Maziwa, Furahia Maisha”
Katika uzinduzi huo Naibu Waziri Ole Nasha alisema kuwa kwa sasa Serikali imeamua kuja na mkakati wa wa uhamasishaji wa wananchi wote kunywa maziwa nchini kwani maziwa yana viinilishe ambavyo hupunguza udamavu kwa watoto pia viinilishe hivyo havipatikani katika vyakula vingine ispokuwa maziwa tu ambavyo pamoja na kupunguza udumavu lakini huongeza uwezo akili kufanyakazi.
“Unywaji wa maziwa umekuwa ukisistizwa kwa watoto tu na si kwa watu wazima lakin imegundulika kuwa kila mtu anatakiwa kunywa maziwa kwa wastani angalau wa kitaifa lita 47 kwa mwaka ili kuongeza viinilishe na kupunguza udumavu kwa watoto wadogo hasa kwa Mkoa wa Kagera ambapo una udumavu wa watoto ni asilimia 52.” Alisistiza Naibu Waziri Ole Nasha .
Tanzania inazalisha maziwa takribani lita bilioni 2.1 kwa mwaka ambapo maziwa mengi asilimia 70 huzalishwa na ng’ombe wa asili ambao uzalishaji wao ni kati ya lita 1 hadi 3 kwa siku. Lakini kuna ng’ombe wachache wa maziwa wanaokadiririwa kuwa 782,000 ambao huzalisha kati ya lita 8 hadi 20 kwa siku.
Aidha, maziwa yanayoingia viwandani kusindikwa kati ya maziwa yanayozalishwa nchini ni asilimia 3 tu ambapo hapa nchin tunavyo viwanda 75 vya kusindika maziwa vyenye uwezo wa kusindika lita 640,000 kwa siku, lakini kwa sasa ni viwanda 65 tu vinavyofanya kazi na vinasindika lita 167,070 kwa siku ambayo ni sawa na asilimia 26 ya uwezo wote uliopo.
Katika Mkoa wa Kagera mtu mmoja anakunywa wastani wa lita 16 kwa mwaka chini ya kiwango cha Kitaifa ambapo mtu mmoja anakunywa lita 47 chini ya kiwango cha Kimaitaifa ambapo mtu mmoja anatakiwa kunywa wastani wa lita 200 kwa mwaka. Kiwango cha wastani wa lita 200 kwa mwaka kilipendekezwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirika la Chakula na Kilimo (FAO).
Mkoa wa Kagera unazalisha maziwa takribani lita 46,858,481 za maziwa kwa mwaka. Uzalishaji huo unatokana na ng’ombe 550,070 ambao kati yao ng’ombe 21, 438 ni wa maziwa. Wanakagera wanatakiwa kuyatumia maadhimisho haya kujifunza mbinu za ufugaji bora na namna ya kusindika maziwa na bidhaa zake.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenelari Mstaafu Salum M. Kijuu alitembelea maadhimisho hayo na kukagua mabanda mbalimbali ya wadau ambao ni wafugaji, wenye viwanda na wasindikaji wa bidhaa mbalimbali zinazotokana na maziwa. Akiwa katika maadhimisho hayo Mhe. Kijuu alitoa msistizo juu ya Elimu kuhusu unywaji wa maziwa kwa wananchi wa Mkoa wa Kagera ambao wanahitaji sana elimu hiyo.
Katika Banda la Bodi ya Maziwa Tanzania Mkuu wa Mkoa aliutaka uongozi wa Bodi ya Maziwa Tanzania kuhakikisha unatoa elimu ya kutosha juu ya usindikaji na unywaji wa maziwa kwani wananchi walio wengi hawana uelewa kuhusu unywaji wa maziwa na elimu hiyo haitolewi mara kwa mara kuonesha umuhimu wa wananchi kunywa maziwa na faida zake.
Ili kuhakikisha Maadhimisho ya Wiki ya Maziwa inafanikisha lengo lake kwa wananchi kunywa maziwa na kufuhia maisha Mhe. Naibu Waziri Ole Nasha wakati wa uzinduzi alizindua unywaji wa Maziwa kwa wananchi ambao ni watu wazima na watoto pia.
Aidha Mkuu wa Mkoa Mhe. Kijuu naye tarehe 29.05.2017 alitoa maziwa kwa Makundi maalum ambayo ni Kituo cha makao ya Wazee Kiilima na shule ya Msingi Mugeza Mseto ambapo wazee wa Kiilima na wanafunzi hao waligawiwa maziwa na kunywa kama uhamasishaji wa unywaji wa maziwa .
Kaimu Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania Bw. Nelson Kilongozi alisema katika maadhimisho hayo kuwa uongozi wa Bodi ya Maziwa uliamua kuleta maadhimisho ya Wiki ya Maziwa Mkoani Kagera Ili kuhamasisha na kutoa elimu kwa wananchi wa Mkoa wa Kagera juu ya umuhimu wa kunywa maziwa, kusindika maziwa na bidhaa zake pia kutoa elimu kwa wadau kuwekeza katika sekta ya maziwa ikiwa ni pamoja na ufugaji bora wa ng’ombe wa maziwa ambao wanao uwezo wa kuzalisha maziwa kwa wingi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa