- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Dhahabu ya kijani (vanilla) Mkoani kagera sasa yawekewa mikakati imara ya kuwanufaisha wakulima na kuinua uchumi wa mkoa badala ya wananchi kutegemea mazao kama ndizi na kahawa tu ambayo yamekuwa yakilimwa kwa mazoea lakini bila kumnufaisha mkulima kulingana na anavyokuwa amewekeza hadi kuuza sokoni.
Mikakati hiyo imefikiwa baada ya Mkuu wa Mkoa Kagera Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti kuitikia wito wa wakulima wa mazao ya vanilla, kakao, na chia na kufanya kikao nao katika Shule ya Sekondari KADEA Kanyigo Wilayani Missenyi na kusikia kilio chao cha wizi wa vanilla changa pamoja na marando yake.
Mara baada ya kutembelea na kukagua shamba la vanilla la Mwalimu Jovin Mbanga Mkuu wa Mkoa Gaguti alikutana na wakulima na kusikiliza kilio chao cha wizi wa vanilla changa na marando katika mashamba yao ambapo wizi huo mara baada ya kufanyika vanilla hizo huuzwa nchi jirani ya Uganda.
Wakimweleza Mkuu wa Mkoa wakulima wa vanilla walisema kuwa changamoto kubwa ni wizi wa vanilla ambapo wanalazimika kulala mashambani wakilinda kila siku zisiibiwe. Wizi huo hufanywa na baadhi ya Watanzania wasiokuwa wazalendo wakishirikiana na wafanyabiashara kutoka nje nchi kwa kupewa mitaji ya kununulia vanilla za wizi.
Pia wakulima hao mbale ya Mkuu wa Mkoa walitoa changamoto zao kuwa ni kutokuwa na masoko rasmi ya kuuza vanilla zao mara baada ya kukomaa aidha, wanunuzi wanaojishughulisha na ununuzi wa vanilla kutosajiliwa na kutambulika Kiserikali ili mwananchi akiwa na vanilla zake aweze kuziuza katika soko na kwa mnunuzi maalum.
Baada ya Mkuu wa Mkoa Gaguti kusikiliza kwa makini malalamiko ya wakulima hao alitoa maelekeza mahususi kuhusu zao la vanilla katika Mkoa wa Kagera Kwanza; Aliagiza kuanzia tarehe ya kikao Aprili 15,2019 vanila itakuwa na muda maalum wa kuvunwa mashambani na kutakuwa na vituo maalum kama masoko ya kununulia vanilla hizo ambapo wafanyabiashara ni marufuku kwenda moja kwa moja kwa wakulima.
Akitoa ufafanuzi zaidi Mkuu wa Mkoa Gaguti alisema kwa mwananchi yeyoyote atakayekamatwa na vanilla kabla ya tarehe ya kuvunwa kutangazwa atachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani na kufunguliwa kesi ya uhujumu uchumi.
Pili; Wakulima wa Vanila wajiunge katika ushirika wa vyama vya msingi ambapo itakuwa rahisi katika kubainisha wezi, kuwa na soko la uhakika lakini pia kuuza vanilla ambazo tayari zimeongezwa thamani ili kupat bei nzuri zaidi na kuweka urahisi zaidi wa Serikali kuwasimamia kama ushirika kuliko mwananchi mmoja mmoja.
Tatu; Wafanyabiashara wote au makampuni yote yanayojihusisha na ununuaji wa vanilla wanatakiwa kujisajili na kupewa leseni ya kununua vanilla kuliko ilivyo sasa. Pia kwa Taasisi au Makampuni ambayo yanatoa ruzuku kwa wakulima wanunue vanilla kwa wakulima kulingana na bei ya soko na si kuwanyonya wakulima.
Aidha, Mkuu wa Mkoa alitoa rai kwa Watendaji wa Vijiji na Kata kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa kikamilifu kama wanataka kuendelea kubaki kazini hasa jukumu la ulinzi na usalama kwa mfumo wa Nyumba Kumi Bora za Usalama ambapo wezi wa vanilla watabainika kirahisi kila eneo.
Mkuu wa Mkoa Gaguti pamoja na kufanya kikao na wakulima wa vanilla pia alichoma zana haramu katika mwalo wa Kabindi Kashenye Kanyigo Wilayani Missenyi na kutangaza rasmi kuwa mwaka huu wa 2019 atakikisha anatokomeza magendo yote iwe ya uvuvi, kahawa au vanilla na kuwataka wananchi wanaojishughulisha na biashara hiyo haramu kuacha mara moja.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Missenyi Kanali Denice Mwila aliwataka wananchi wa Missenyi hasa Wakulima wa Vanila Kanyigio kubadilika kwani alisema kuwa wizi mwingine wa vanilla unatokea ndani ya familia na alitoa mfano kwa kusema kuwa unakuta shamba ni la baba na akitoka kwenda pengine Bukoba Mjini kufanya shughuli zake mama au mtoto anavuna vanilla haraha haraka na kuziuza lakini baba akirudi anaambiwa vanilla zimeibwa.
Katika kuchukua hatua kwa baadhi ya watuhumiwa ambao waliwahi kutajwa katika mikutano ya hadhara au kupigiwa kura Mkuu wa Mkoa alimwagiza Mkuu wa Wilaya ya Missenyi Kanali Denice Mwila kuwa watu hao walipoti mara moja ofisini kwake na hatua zianze kuchuuliwa ambapo Mkuu huyo wa Wilaya alitekeleza agizo hilo mara moja kwa kuondoka na Mzee George Lubale aliwahi kutuhumiwa kujihusisha na wizi wa vanilla.
Vanila ni zao ambalo linaonekana kutaka kuukomboa mkoa wa Kagera, zao hili linalimwa katika sehemu yenye kivuli hasa kwenye migomba au kwenye miti na linahitaji mwanga sawa na kivuli asilimia 50% kwa 50%. Vanila inapandwa marando ambapo yanapandwa na kuwekewa mti aina ya jatrofa ili kukua kwa kupanda mti huo na mazao yake ni kama maharage. Bei kwa sasa sokoni tena kwa vanila changa ni kati ya shilingi 20,000/= hadi 30,000/= kwa kilo moja.
Mwaka 2017/18 bei ya vanilla mkoani kagera ilifikia kati ya shilingi 100,000/= hadi 150,000/= na siku za nyuma vanilla iliwahi kuzalishwa Mkoani Kagera hadi kufikia tani 103 lakini kwa sasa zinazalishwa tani 10 hadi 12 ambapo zao hili limekuwa likingiiza zaidi ya shilingi milioni 800,000/= Vanila inastawi au inalimwa na kukomaa kwa miezi tisa tu tayari unavuna na kuuaga umasikini milele badala ya kutegemea zao moja la kahawa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa