- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Mkoa wa Kagera waendelea juhdi za kupambana na wahujumu uchumi wanaosafirisha Kahawa kwa njia za magendo kwenda nchi jirani huku wakikwepa kulipa za kodi za Serikali zinazotumika kuleta maendeleo ya wananchi katika Mkoa.
Ni baada ya Jeshi la Polisi Mkoani hapa usiku wa kuamukia Agosti 31, 2018 kukamata Magari mawili aina ya FUSO yenye namba T 182 ARG na T 424 AMY yakiwa yamepakia Kahawa zilizokobolewa zaidi ya tani 10 katika Kijiji cha Katarabuga Kata Bwanjai yakiwa barabara kuu ya kuelekea Katoma hadi Kanyigo Wilayani Missenyi mpakani mwa Tanzania na Uganda.
Akikagua Kahawa hizo zilizokamatwa Septemba Mosi, 2018 katika Kijiji cha Katarabuga Kata Bwanjai Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Marco E. Gaguti alilipongeza Jeshi la Polisi Mkoani Kagera kwa kutekeleza wajibu wake ipasavyo pamoja na ushirikiano kutoka kwa wananchi ambao kwa kiasi kikubwa walisaidia katika ukamatwaji wa Kahawa hizo.
Mkuu wa Mkoa Gaguti alisema kuwa katika Mkoa wa Kagera haitawezekana kuruhusu wahujumu uchumi kuendelea na vitendo vya biashara ya magendo na katika kuhakikisha hilo halifanyiki alisisititiza Kamati za Ulinzi na Usalama za Kata na Vijiji kuhakikisha zinatimiza wajibu wake ipasavyo kwa kuwashirikisha wananchi katika maeneo yao ili wawadhibiti watu kama hao.
“Katika Mkoa wetu mwaka huu 2018 tumelenga kukusanya tani 81,000 za Kahawa lakini kwa vitendo hivi vya utoroshaji Kahawa kimagendo bila kufuata utaratibu wa kulipa kodi hatuwezi kufikia lengo. Sisi Serikali ya Mkoa hatuwezi kurusu ardhi yetu itumike bure alafu mchana tunashangilia maendeleo ya nchi kumbe usiku kuna watu wanafanya biashara haramu tena kwa kutumia miundombinu yetu iliyogharamiwa na kodi za wananchi wakati wao wanakwepa kodi hizo, hiyo haikubaliki.” Alisisitiza Mhe Gaguti.
Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera Augustne Olomi alisema kuwa Jeshi hilo linawashikilia watuhumiwa wanne kutokana na tukio hilo. Aidha, Kamanda Olomi alisema baada ya taratibu zote kukamilika Kahawa hizo zilizokamatwa zaidi ya tani 10 zitauzwa kwa njia ya mnada na fedha zikazopatikana zitaingizwa kwenye mfuko wa mapato ya Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.
Wananchi au wafanyabiashara ya Kahawa wanashauriwa kuachana na biashara ya magendo bali wauze Kahawa yao kwa mfumo sahihi uliowekwa na Serikali ili kodi husika zilipwe. Kama kuna mwanachi au mfanyabiashara anataka kuuza kahawa yake nje ya nchi ni shariti kufuata utaratibu uliopo na kulipa kodi zote za Serikali na ataruhusiwa kuuza Kahawa yake popote pale nje ya nchi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa