- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Mikoa Kumi na Moja Yakutana Kagera Kuweka Mikakati ya Kuimarisha Ulinzi na Usalama na Kukuza Uchumi wa Wananchi Katika Mikoa Hiyo
Wakuu wa Mikoa kumi na moja pamoja na Kamati za Ulinzi na Usalama kutoka Kanda ya Magharibi na Kanda ya Ziwa wakutana Mkoani Kagera Manispaa ya Bukoba kufanya mkutano wa pamoja wa ujirani mwema ili kujadili kwa pamoja changamoto za Ulinzi na Usalama na jinsi ya kukabiliana na vitendo vya uharifu vilevile kubadilishana uzoefu wa masuala mbalimbali ikiwa ni apmoja na fursa za uwekezaji katika mikoa hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora ambaye ni Mwenyekiti wa mkutano huo Mhe. Aggrey Mwanri akifungua mkutano alisema kuwa lengo kuu la kukutana mikoa kumi na moja ni kuweka mkakati wa pamoja katika masuala ya Ulinzi na Usalama na kubadilashana uzoefu wa kudhibiti vitendo vya kihalifu katika mikoa ya Kanda ya Ziwa na Kanda ya Magharibi.
“Hii mikoa kumi na moja ndiyo mikoa ambayo ipo karibu na Makao Makuu ya nchi Dodoma, kama sisi hatutaweka vizuri mikoa yetu uhalifu ukaanzia kwetu Dodoma hakuwezi kuwa salama. Pili, sisi mnatuona hapa tulipewa jukumu kubwa na Waziri Mkuu wa Jamhauri ya Muungano wa Tanzania kusimamia zao la pamba na kuhakikisha hii mikoa inakuwa wazalishaji wakubwa ambapo sasa tutajadili kwa kina na kuweka mikakati ya pamoja ya kuinua zao la pamba,” Alisisitiza Mhe. Mwanri.
Naye Makamu Mwenyekiti ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum M. Kijuu akiwakaribisha wajumbe wa Mkutanao huo alisema kuwa Mikutano ya ujirani mwema imesaidia sana kwani kabla ya mikutano hiyo kufanyika operesheni mabalimbali zilikuwa zikifanyika ambapowaharifu walikuwa wakitoka mkoa mmoja na kuhamia mkoa mwingine na na kuweka ugumu wa kuudhibiti uharifu huo.
“Kutokana na umuhimu wa mikutano hii sisi Mkoa wa kagera tumeweza kufanya operesheni na kufanikiwa kuiondoa mifugo katika Mapori yetu ya Akiba na Hifadhi za Misitu na sasa wanyamapori wamerejea kwa kasi na kuanza kuzaliana sana. Katika mapori hayo waharifu walikuwa wakijificha kwenye mwavuli wa ufugaji lakini tumefanikiwa kuwatokomeza na sasa tunawakaribisha wawekezaji mbalimbali kuja kuwekeza katika mahoteli ya kitalii ili kuwavutia watalii katika Maporui hayo.
Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Adam Kigoma Malima ambaye ni mjumbe wa mkutano huo alisema kuwa mkutano wa ujirani mwema ni muhimu sana kwani kunakuwa na mada mbalimbali zajinsi ya kukuza na kuinua uchumi wa wananchi katika mikoa husika. Alitoa mfano kuwa katika mkutano wa Kagera kuna mada ya zao la Vanilla ambalo linalimwa Kagera pekee na lina bei kubwa ambapo alisema kuwa amekuja kujifunza ili akaipeleke fursa hiyo katika Mkoa wa Mara.
Akiongea kwa niaba ya Makamanda wa Jeshi la Polisi wenzake Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanaza Ahmed Msangi alisema kuwa kufanya mikutano ya ujirani mwema, kupeana na kubadilishana mbinu za kiusalama wameweza kuwadhibiti wahalifu ambapo alisisitiza kuwa wahalifu walikuwa wakifanya uhalifu kwa kuhama kutoka mkoa mmoja na kwenda mkoa mwingine lakini kwasasa hawawezi kutokana na mikakati ya pamoja.
Mkutano huo wa ujirani mwema umefanyika Desemba 15, 2017 katika Manispaa ya Bukoba katika Hoteli ya ELCT Bukoba Mkoani Kagera na mikoa iliyoshiriki mkutano huo ni Kagera, Tabora, Shinyanga, Mara, Mwanza, Katavi, Geita, Simiyu, Singida, Rukwa na Kigoma. Wakuu wa Mikoa waliohudhuria ni pamoja na Mwenyekiti Mhe. Aggrey Mwanri na Makamu Mwenyekiti Meja Jenerali Mstaafu Salum M. Kijuu.
Wengine ni Mhe Adam Kigoma Malima Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mhe. Anthony Mtaka Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhandisi Robert Gabriel Mkuu wa Mkoa wa Geita, Wakuu wa mikoa wengine waliwakilishwa katika Mkutano huo. Aidha, Makatibu Tawala wa Mikoa na wajumbe wa Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa yote kumi na moja walihudhuria katika mkutano huo wa ujirani mwema .
Mkutano huu wa ujirani mwema ni mkutano wa nne kufanyika ambapo mkutano wa kwanza ulifanyika Mkoani Tabora mwezi Januari 2017, Mkutano wa pili ulifanyika mwezi Machi 2017 Mkoani Kigoma, Mkutano wa tatu ulifanyika Mkoani Singida mwezi Juni 2017 na Mwezi huu Desemba 2017 Mkutano wa Ujirani Mwema umefanyika Mkoani Kagera.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa