- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Watuhumiwa wawili Mwalimu Respicius Patrick Mtazangira na Mwalimu Herieth Gerald wa mauji ya Mwanafunzi Sperius Eradius (13) aliyekuwa akisoma Shule ya Msingi Kibeta Manispaa ya Bukoba wamefikishwa Mahakama ya Wilya ya Bukoba leo Septemba 3, 2018 na kusomewa shitaka la mauaji linalowakabili mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi John Kapogoro.
Katika kesi hiyo ya Mauaji Namba 18 ya Mwaka 2018 watuhumiwa hao wawili Mwalimu Respicius Patrick na Mwalimu Herieth Gerald hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa Mahakama ya Wilaya haina mamlaka ya kusikiliza kesi yao bali Mahakama Kuu, mara baada ya kusomewa shitaka linalowakabili walirudishwa Mahabusu.
Kesi hiyo Namaba 18 ya Mwaka 2018 ilihairishwa hadi tarehe 17 Septemba, 2018 kwaajili ya kukamilisha taratibu za Kimahakama ili iweze kuhamishiwa Mahakama Kuu kwa ajili ya kusikilizwa. Hakimu Mkazi Mfawidhi John Kapogoro mara baada ya watuhumiwa kusomewa shitaka alimuru warudishwe mahabusu kwani shitaka linalowakabili halina dhamana.
Akitoa ufafanuzi wa kesi hiyo Kaimu Wakili wa Serikali Mfawidhi Athuman Matuma Kirati alisema kuwa ushaidi wa kesi hiyo umekamilika kwa asilimia 100% na ofisi yake inaendelea na utaratibu wa kufungua jarada la kesi hiyo Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba ambapo alisema kuwa leo mchana Septemba 3, 2018 jarada la kesi hiyo litaweza kufunguliwa katika Mahakama Kuu.
Wakili wa Serikali Matuma alisema kuwa katika kesi hiyo ya mauji Namba 18 ya mwaka 2018 kulingana na ushahidi uliokusanywa na kukamilika kwa asilimia 100% unaonesha kuwa mauaji ya Mwanafunzi Sperius Eradius yalikuwa ni mauaji ya kukusudia kutokana na siraha alizoshambuliwa nazo mwanafunzi huyo.
“Ushahidi wetu unaonesha kuwa Mwalimu Respicius Mtazangira alikuwa anamshambulia Mwanafunzi Sperius Eradius kwa vipande vya kuni vilivyokuwa vimekusanywa na wanafunzi wa darasa la saba kwaajili ya kupikia chakula chao, Pili pamoja na Marehemu Sperius Eradius kupiga kelele sana kuwa anauwa akiomba msaada kwa wanafunzi wenzake waende kumnusuru bado Mwalimu Mtazangira aliendelea kumpiga mwanafunzi huyo.” Alieleza Wakili Matuma.
Pamoja na ushahidi huo lakini Wakili wa Serikali Matuma alieleza kuwa baadhi ya Walimu walimwendea Mwalimu Respicius Mtazangira kumuomba aache kumpiga mwanafunzi huyo lakini aliendelea kumpiga jambo ambalo linaonesha alikusudia kumuua mwanafunzi Sperius Eradius.
Marehemu Sperius Eradius alifariki dunia Agosti 27, 2018 muda mchache baada ya kupigwa shuleni Kibeta na Mwalimu Respicius Patrick Mtazangira aliyekuwa Mwalimu wa nidhamu katika shule hiyo kwa kutuhumiwa kuiba mkoba (pochi) ya Mwalimu Herieth Gerald. Marehemu Sperius Eradius alizikwa Agosti 31, 2018 nyumbani kwa baba yake Mzazi Kata Mubunda Kijiji Kitoko Wilayani Muleba.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa